Serikali na Waasi Sudan Kusini walaumiana

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Serikali na waasi wa Sudan kusini wamekuwa wakilaumiana kila mmoja kwa kukiuka makubaliano mapya ya amani ya nchi hiyo yaliyosainiwa wiki iliyopita.

Jeshi limekuwa likiwalaumu waasi kumuunga mkono Makamu wa Rauis wa zamani Riek Machar kwa kuanzisha mashambulizi katika jimbo la Upper Nile ambako raia 18 waliuawa.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Lul Ruai Koang amesema waasi walishambulia mji wa Maban ulioko katika jimbo la Upper Nile karibu na mpaka wa Sudan, siku ya Jumapili.

Amesema majeshi yao yalijibu mashambulizi na katika mapigano waasi waliwaua raia 18 na kuwajeruhi wengine 44. Miongoni mwa waliokufa ni raia watatui wa Ethiopia na wawili kutoka Sudan.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema hali bado ni ya wasiwasi katika eneo la tukio. Huku watu bado hakihofia kurudi katika makaazi yao.

Hata hivyo waasi wamekuwa wakikanusha kuua raia na kusema kuwa serikali wameanzisha mapigano katika maeneo yao.

Kwa upande wake Msemaji msaidizi wa waasi Lam Paul Gabriel amesema wapiganaji wao walishambuliwa vibaya na majeshi ya serikali kwenye eneo la Maban na kukanusha pia taarifa zao wao kuwashambulia raia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi wa Sudan Kusini

Mzozo usiomalizika Sudan Kusini

Mzozo wa Sudan ya kusini umedumu sasa kwa miaka mitano, hali ambayo imesababisha robo ya watu nchini humo kuyakimbia makaazi yao na karibu robo tatu ya watoto kuacha shule.

Sudan kusini ilitumbukia katika mapigano mwaka 2013 baada ya kutokea kutoelewana kisiasa kati ya Rais wa nchi hiyo Salva Kiir na Makamu wake wa Rais Riek Machar.

Mapigano nchini humo yameathiri sana uzalishaji wa mafuta na kuvuruga uchumi wa nchi.

Makubaliano yaliyofikiwa wiki iliyopita yalikuwa ni jaribio la pili linalofanywa na wasuluhishi wa kikanda kujaribu kumaliza vita baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya awali ya mwaka 2015.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii