Kurejea kwa Bemba DRC kutakuwa na maana gani?

Jean Pierre Bemba
Image caption Jean Pierre Bemba

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC itatoa uamuzi wake kuhusu kesi ya aliyekuwa makamu wa rais nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo Jean-Pierre Bemba leo Jumatano.

Bemba alikutwa na hatia ya kuwahonga mashahidi kwenye kesi ya uhalifu wa kivita.

Jean-Pierre Bemba amekuwa gerezani huko Hague kwa kipindi cha miaka 10 na hukumu yake ya kwanza iliyotokana na mashtaka ya uhalifu wa kivita ilikuwa moja ya mafanikio ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC.

Ndiyo mara ya kwanza mahakama ya ICC iliangazia suala la ubakaji kuwa silaha ya vita, na mara ya kwanza mshukiwa alihukumiwa kwa makosa ambayo yalifanywa na watu waliokuwa chini ya uongozi wake.

Lakini kesi hiyo ilibatilishwa mwezi uliopitaa wakati Bemba aliondolewa mashtaka baada ya kukata rufaa. Mawakili walitambua dosari kwenye kesi iliyohusu uhalifu uliofanywa na wapiganaji wake kutoka kundi la MLC nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwaka 2007 mawakili wake walikata rufaa kupinga hukumu yake na kuwahonga mashahidi wakidai kulikuwa na dosari katika kesi hiyo. Lakini mwezi Machi mwaka huu rufaa hiyo ilitupiliwa mbali.

Mambo Makuu

Jean-Pierre Bemba alizaliwa mwaka 1962 kwenye mkoa wa kaskazinia magharibi wa Equateur, Baba yake, bilionea Bemba Saolona alikuwa rafiki wa karibu wa Mobutu Sese Seko.

Baba wa watoto watano amemuoa binti wa Mobutu na kusababisha kupewa jina "Mobutu Mdogo" kwa sababu ya uhusiano wake wa karibu na kiongozi huyo wa zamani wa DRC.

Novemba mwaka 1998 Bemba alibuni kundi la waasi MLC kwenye mkoa wake wa nyumbani wa Equateur.

Vikosi vyake baadaye vilihusika kwenye mzozo kati ya mwaka 2002 na 2003 kwenye nchi jirani ya DRC, vikipagana kwa ushirikiano na vikosi vilivyokuwa watiifu kwa aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ange-Felix Patasse, ambaye alikuwa akipingwa na aliyekuwa mkuu wake wa majeshi wakati huo Francois Bozize.

Agosti mwaka 1999, MLC ilisaini mkataba wa amani wa Lusaka ambao ulinuia kufikisha kikomo mapigano nchini DRC.

Aligeuza MLC kutoka kundi la waasi na kuwa chama cha kisiasa kufuatia kusainiwa makubaliano ya amani ya mwaka 2002.

Bemba alihudumu kama mmoja wa makamu wanne wa rais nchini DRC kwenye serikali ya umoja kati ya mwaka 2003 na 2006.

Kama mgombea mkuu wa chama chake aliwania urais mwaka 2006 lakini akashindwa na rais wa sasa Joseph Kabila, kwenye marudio.

Mwaka 2007, mapigano kati ya wapiganaji watiifu kwake na jeshi yalizuka mjini Kinshasa na kusababisha vifo vya takriban watu 100.

Bemba alikimbilia nchini Afrika Kusini akidai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini. Baadaye alikimbilia uhamishoni na familia yake.

Mwezi Mei mwaka 2008 alikamatwa na mahakama ya ICC mjini Brussels, Ubelgiji kujibu mashtaka ya uhalifu uliotendwa na vikosi vyake nchini Jamhuri ya Afrika ya kati.

Wengine wanasemaje

Mwandishi wa BBC aliye mjini Kinshasa amezungumza na baadhi wa wafuasi wa Bemba ambao wemeelezea hamu yao ya kutaka arudi nyumbani ili apate kuendelea na shughuli zake za siasa.

Akizungumzia kufutwa kwa mashtaka ya Bemba, kiongozi wa upinzani nchini DRC ambaye pia anatarajiwa kugombea urais Moise Katumbi, alisema, "kufutwa hukumu hiyo ni ishara kuwa ukweli kawaida hubainika."

"Kufutwa kwa hukumu ya Bemba kunaonyesha kuwa ICC haina msimamo, alisema Felix Tshisekedi.

Akizungumzia hatma ya kisia ya Bemba, naibu katibu mkuu wa chama cha MLC, Fidele Babala, alisema: "Miaka kumi ya mtu ni mingi sana na atajijenga... ombi letu ni kwamba atarejea shughuli zake alikoachia. Hakuna kitu kitazuia hilo."

Matamshi hayo pia yaliungwa mkono na wakili wa Bemba ambaye alisema; "hajakufa moyo katika malengo yake ya kisiasa."