Utafiti wa Twaweza: Asilimia 65 ya watanzania hawako tayari kuandamana

Je watanzania hawapendi kushiriki kwenye masuala yanayowahusu?
Image caption Je watanzania hawapendi kushiriki kwenye masuala yanayowahusu?

Asilimia 65 ya wananchi watanzania wanasema hawako tayari kutumia njia ya maandamano kuishinikiza serikali katika mambo yasiyowaridhisha.

Kwa upande mwingine, mwananchi mmoja kati ya wanne (27%) ana uwezekano wa kushiriki kwenye maandamano.

Wakati huo huo serikali imekanusha dhana kwamba umaarufu wa Rais John Pombe Magufuli unapungua kama taasisi hiyo ya kiserikali inayojihusisha na utafiti nchini humo ya Twaweza inavyodai kwenye ripoti yake ya leo.

Msemaji na katibu mwenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Bwana Humphery PolePole amesema Rais Magufuli bado ni maarufu sana nchini Tanzania kutoka na sera zake.

Ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2016, idadi ya wanaosema wana uwezekano wa kushiriki imeshuka kidogo sana (kutoka 29% mpaka 27%) wakati ambao wanasema hawana uwezekano wa kushiriki imeongezeka (kutoka 50% mpaka 65%).

Ripoti hii ni kwa mujibu wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na utafiti nchini Tanzania ya Twaweza ambayo imezindua ripoti kuhusu ushiriki ,maandamano na siasa nchini humo. ripoti hiyo ikitaja mambo tisa muhimu yaliyotazamwa na utafiti huo.

Je, huenda watanzania hawapendi kushiriki katika masuala yanayowahusu?

Hili ni moja kati ya masuala muhimu kuibuliwa kwenye utafiti huu. Wananchi wachache kwa hiari wametaja maandamano kama njia ya kufikisha malalamiko yao kwa serikali. Idadi kubwa ya wananchi

wanasema hawako tayari kushiriki kwenye maandamano kuhusu jambo lolote lisilowapendeza.- ikiwemo idadi kubwa ya wafuasi wa vyama vya upinzani. Na wananchi wengi zaidi wanaunga mkono serikali kukataza mikutano na maandamano ya kisiasa kuliko wale wanaopinga.

Haki miliki ya picha Ikulu Tanzania
Image caption Raisi wa Tanzania Dokta John Magufuli

Utafiti wa Twaweza unaona wazi kuwepo kwa sababu kadhaa za kutofanyika maandamano ya tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 2018 kama yalivyokuwa yamepangwa.

Kuna sababu kadha wa kadha ambazo wananchi walizitoa za kutojitokeza kwenye maandamano:

Hofu: iliyotajwa na wananchi kuwa maandamano yangeweza kusababisha vurugu na kwa kushiriki kwao kungeweza kuhatarisha maisha yao. Hata hivyo, taasisi ya twaweza ilisisitiza kutiliwa maanani kwani maoni hayo yanatoa mwanga kuhusu changamoto iliyopo ya kuandaa maandamano nchini Tanzania.

Kwanza, kuhamasisha idadi kubwa ya watu si jambo rahisi. Ni 6% pekee ya wananchi ambao walikuwa na taarifa za uhakika kuhusu maandamano yaliyopangwa, na 2% pekee waliweza kumtambua kwa usahihi Mange Kimambi kama mhamasishaji.

Katika muktadha huu, kuandaa maandamano kutumia mitandao ya kijamii inaonekana imeathiri uwezekano wa maandamano kufanyika kiuhalisia.

Image caption Wachangiaji na wadau mbalimbali wameshiriki kuchambua Utafiti uliotolewa na Twaweza

Pili, utafiti huu umebaini kuwepo kwa tofauti kati ya ufahamu wa maandamano yaliyopangwa na uungaji mkono wa maandamano hayo.

Wanawake, watu masikini na wale wanaoishi maeneo ya vijijini wote walikuwa na uwezekano mdogo wa kufahamu kuhusu maandamano hayo kuliko wanaume, wasiokua masikini na wale waishio maeneo ya mijini. Lakini wale ambao hawakuwa wakifahamu sana kuhusu maandamano hayo ndiyo waliokuwa tayari zaidi kusema wangeyaunga mkono.

Kwa maneno mengine, makundi kwenye jamii ambayo hayako karibu sana na vyombo vya habari

(ikiwemo mitandao ya kijamii) ni makundi ambayo yangekuwa na uwezekano mkubwa wa kushiriki kwenye maandamano iwapo wangepata taarifa.

Tatu, sababu kubwa ambayo wananchi wanataja ya kupinga au kutotaka kushiriki kwenye maandamano kwa ujumla na maandamano ya Aprili 26 - ni ''hofu ya vurugu'' Ikiwemo hofu binafsi ya kukamatwa na kutaka kudumisha amani na utulivu.

Twaweza imesema takwimu zilizowasilishwa hapa pia zinaonesha dhahiri wananchi wanaunga mkono sababu za Mange Kimambi na wafuasi wake za kuhamasisha maandamano. ''Uungaji mkono wa maandamano ya April 26 mwaka 2018, ni mkubwa mara mbili zaidi ya ule wa maandamano ya UKUTA Agosti mwaka 2016'', ilieleza ripoti hiyo.