Kenya: Dawa ya HIV inayosababisha kasoro kwa watoto walio tumboni yapigwa marufuku

mama mjamzito Haki miliki ya picha Getty Images

Wizara ya Afya nchini Kenya imezishauri serikali za kaunti nchini humo dhidi ya kuwapatia wagonjwa aina ya dawa za HIV ambazo imesema zinasababisha kasoro miongoni mwa watoto walio tumboni.

Kupitia Mkurugenzi wa huduma za matibabu nchini humo Jackson Kioko, wizara hiyo imewashauri Wakurugenzi wa afya katika kaunti hizo kuhakikisha kuwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha ambao walikuwa wakitumia dawa aina ya kwanza ya Dolutegravir (DTG), waendelee kutumia dawa hiyo hadi watakapomaliza kunyonyesha.

Lakini akina mama wajawazito walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 49 ambao wamekuwa wakitumia dawa hiyo wanapaswa kupewa matibabu ya kwanza ya Efavirenz.

Katika taarifa kwa wakurugenzi hao Dkt. Kioko alisema kuwa dawa hiyo iliozinduliwa nchini Kenya mwaka uliopita haifai kutumiwa na wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha kutokana na data chache za usalama wake zilizopo.

Pia ameongezea kwamba kulingana na taarifa ya mwaka 2017, watu wazima wanaotumia dawa ya kwanza ya ARV wataanza kutumia DTG.

Hatahivyo mwenyekiti wa bodi ya madaktari nchini Kenya tawi la magharibi Dkt Anthony Akoto amesema kuwa wizara ya afya inapaswa kutoa sababu za hatua hiyo zikiandamana na ushahidi.

Akizungumza na BBC, Dkt Akoto anasema kuwa kufikia sasa hakuna ushahidi wowote kwamba dawa hiyo ina madhara na akivitaka vitengo muhimu vya serikali katika wizara ya Afya kama vile Kemri, Shirika linalosimamia udhibiti wa ugonjwa wa ukimwi NASCOP, na shirika la ubora wa bidhaa KBS kutoa ushahidi unaothibitisha dawa hiyo haifai kupewa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha.

''Tunataka watupatie sababu zitakazoandama na ushahidi kutoka kwa na vitengo vya wizara ya afya kama vile Kemri na Nascop," alisema Dkt Akoto.

''Wanafaa kutupatia maelezo na watuambie tuwapeleke wapi wagonjwa hawa'', aliongezea.

Haki miliki ya picha Reuters

Agizo hilo la wizara ya afya limeongezea kwamba wale wote wanaotoa matibabu wanapaswa kuwa waangalifu katika kutambua na kuripoti kuhusu athari mbaya za dawa zinazohusiana na ARVs.

Wadhibiti wa kimataifa, Shirika la chakula nchini Marekani na utawala wa kusimamia dawa pamoja na kitengo cha dawa barani Ulaya mwezi uliopita walionya kwamba utafiti mpya unaonyesha kuwa wanawake wanaotumia dawa za HIV wakati wa kushika mimba wako katika hatari ya kujifungua watoto walio na kasoro.

Dawa hiyo iliidhinishwa yapata miaka minne iliopita na shirika la afya duniani WHO linashauri kwamba haifai kutumiwa wakati ya ujauzito ama hata kunyonyesha kutokana na data chache za usalama na maelezo hayo hayajabadilika.

Dawa ya Dolutegravir iliidhinishwa nchini Marekani 2013 na katika muungano wa Ulaya 2014.

Dawa hiyo inafanya kazi kwa kuzuia Enyme za HIV ili kuzuia virusi hivyo kuzaana hivyobasi kupunguza idadi ya virusi hivyo mwilini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii