Makubaliano ya nyuklia ya Korea Kaskazini: Pyongyang yadai 'kujutia' tabia za Marekani.

waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo amuaga Kim Yong-chol katika uwanja wa ndege wa Pyongyang

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mike Pompeo na Kim Yong-chol wakiambia kwaheri

Korea ya Kaskazini imesema kwamba mtazamo wa Marekani katika mazungumzo ya hivi karibuni kuhusu mpango wake wa nyuklia ni wa kusikitisha" na "kutisha ".

Taarifa hiyo iliotolewa na afisa wa wizara ya kigeni asiyejulikana , ilikanusha taarifa iliotolewa na waziri wa maswala ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo saa chache kabla.

Alikuwa amesema kuwa hatua zilipigwa katika mazungumzo hayo ya siku mbili mjini Pyongyang.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa waziri huyo kuzuru Korea Kaskazini tangu mkutano wa Donald Trump na mwenzake Kim Jong un nchini Singapore.

Taarifa hiyo ya Korea Kaskazini iliorushwa hewani na chombo cha habari cha kitaifa nchini Korea Kaskazini KCNA ilisema kuwa Marekani ilikiuka mwenendo wa mkutano huo kwa kulishinikiza taifa hilo kufutilia mbali mpango wake wa silaha za kinyuklia.

''Tulitarajia kwamba upande wa Marekani utawasilisha wazo zuri , tukitaraji kwamba pia nasi tutakubaliana'' , taarifa hiyo ya Korea Kaskazini ilisema.

Lakini kupitia mazungumzo hayo ya ngazi ya juu, maelewano kati ya DPRK na Marekani yanaelekea hatarini ambapo uamuzi wetu wa kusitisha mipango ya kinyuklia huenda ukagonga mwamba..

'Hatua kubwa iliopigwa'

Lengo muhimu la ziara ya siku mbili ya Mike Pompeo ilikuwa kupata hakikisho kutoka kwa Korea Kaskazini kwamba itasitisha mpango wake wa kinyuklia

Alikuwa amekutana na Kim Yong chol-anayejulikana kama mwandani wa karibu wa rais Kim Jong Un

Baadaye , Pompeo hakufichua yaliozungumzwa , lakini alisema kuwa walizungumzia kwa kina kuhusu muda wa kusitisha mpango huo wa kinyuklia ikiwemo uharibifu wa mashine ya kufanyia majaribio silaha hizo.

''Haya ni maswala tata, lakini tulifanikiwa kupiga hatua kuhusu kila swala muhimu, mambo mengine tulipiga hatua kubwa zaidi huku mengine yakitarajia kazi zaidi kufanywa'' , alisema kabla ya Korea Kaskazini kutoa taarifa yake kuhusu mkutano huo.

Kim Jong-un ameahidi kufanyia kazi mpango wa kusitisha mpango wake wa nyuklia , ijapokuwa maelezo kuhusu vile mpango huo utakavyoafikiwa hayajulikani.

Baada ya mkutano wa Singapore , ambao Marekani pia ilitoa hakikisho la usalama kwa Korea Kaskazini na kuahidi kusitisha mazoezi yake ya kijeshi na Korea Kusini, rais Trump alitangaza kuwa Korea Kaskazini sio tishio la Kinyuklia.

Hatahivyo rais huyo ameimarisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini , huku maafisa wa upelelezi wa Marekani wakisema kuwa kuna ushahidi kwamba Korea Kaskazini inaendelea kuimarisha miundo mbinu ya mpango wake wa silaha zake za kinyuklia.