George Jonas: Mtanzania aliyechangia kuunda ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner ya Air Tanzania

Ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner

Wakati ndege mpya ya shirika la ndege la ACTL ya Boeing 787-8 ilipotua katika uwanja wa mwalimu Julius Nyerere siku ya Jumapili, ni wachache ambao wangedhania kwamba Mtanzania ni miongoni mwa wale walioitengeneza ndege hiyo.

Hatahivyo ukweli ni kwamba bwana George Jonas anayetoka katika mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa maafisa wa kiufundi aliyehusika katika utengenezaji wa ndege hiyo yenye viti 262, kwa jina Boeing 787-8 Dreamliner.

Injini za ndege hiyo zimejengwa kwa njia maalumu ili kupunguza sauti ndani na pia nje ya ndege kwa hadi asilimia 60 huku madirisha yake yakiwa makubwa kuliko yale ya ndege zingine za ukubwa kama huo kwa asilimia 30.

Jonas ambaye babaake alikuwa mwanajeshi wa Tanzania aliambia The Citizen nchini humo kwamba amekuwa akihusika katika uundaji wa ndege hiyo tangu 2015 akiwa mfanyikazi wa kampuni ya Boeing, kutoka Marekani ambayo huunda, kutengeza na kuuza ndege, roketi, Setlaiti na makombora.

Habari ya mwana huyo wa bi na bwana labani Mwanjisya inaanzia wakati alipokuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya Ubungo.

Hiyo ilikuwa kati ya mwaka 1985 na 1991, alisema akiongezea kwamba baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya msingi alijiunga na shule ya upili ya Azania mjini Dar es Salaam kwa masomo ya kawaida kabla ya kuelekea shule ya upili ya IIboru mjini Arusha kwa masomo tangulizi ya shule ya upili.

''Nikiwa IIboru, nilisomea sayansi na kushirikisha masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati'', alisema.

Alichaguliwa na kundi moja la raia wa Marekani waliokuwa wakitafuta kijana wa Tanzania aliyekuwa na maono ili kufanya kazi kwa miezi mitatu nchini Marekani.

''Nilijiona kuwa mwenye bahati. Sikujua mtu yeyote wakati huo na wazazi wangu hawakuwa na fedha za kunipeleka ng'ambo kusoma'', alisema bwana Jonas, akiongezea kuwa babake alikuwa akifanya kazi katika jeshi la Tanzania.

Masomo yake

Akiwa nchini Marekani, alituma maombi ya kutaka kusoma katika chuo kikuu na akafanikiwa kusajiliwa na chuo kikuu cha Wichita ambapo alisomea shahada ya uhandisi wa mitambo ya kielektroniki pamoja na hesabati.

Masomo hayo yalitarajiwa kumpeleka katika kampuni ya Bombardier, kampuni ya uchukuzi wa ndege ya Canada ilioko katika mji wa Montreal, Quebec.

Alifanya mafunzo yake katika tawi la Bombaridier lililopo Wichita 2005, huku akihusika na utengezaji wa ndege za watu binafsi pamoja na zile za kijeshi.

Alifanya kazi katika kampuni hiyo kwa miaka minne kabla ya kujiunga na Boeing 2011 kama muhandisi wa kielektroniki wa mitambo ya ndege za kibiashara.

Alihusika na mifumo yote ya kuendesha ndege hiyo.

Wakati mmoja alipokuwa katika mtandao akapata tangazo la Boeing na kuamua kujaribu kutuma ombi.

''Siku moja nilipokuwa kazini nilipokea simu kutoka Boeing, ikinielezea kwamba nilikuwa miongoni mwa watu 50 walioorodheshwa katika mahojiano ya kazi. Walinitumia nauli ya ndege. Nilienda katika mahojiano hayo, nikiwa sina wasiwasi, kwasababu tayari nilikuwa nimeajiriwa na Bombadier'', alisema.

Baadaye alipatiwa habari njema kwamba amepata kazi na kwamba alifaa kuhamia katika jimbo la Seattle kufanya kazi na Boeing.

Akiwa huko alijifunza mambo mengi .

Mwaka 2015, alisomea shahada ya uzamili katika uhandisi wa mitambo katika chuo kikuu cha Washington. Mbali na mafunzo hayo pia alijifunza kuhusu usalama wa ndege . Pia anamiliki cheti cha usimamizi wa miradi kutoka chuo kikuu cha Stanford, alisema.

Nchini Tanzania , ameanzisha mradi kwa jina STEM. Maana ya STEM ni Sayansi, Teknolojia, Uhandisi{Engineering} na Hesabati{ Mathematics} kwa lengo la kuimarisha mafunzo kwa msingi wa mradi huo na kujumuisha mafunzo hayo katika mtaala wa sayansi na hesabati.

Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya aina gani?

Ndege hiyo ya Tanzania ilisafiri kutoka uwanja wa Paine mjini Seattle, Washington safari ya umbali wa saa 22.

Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya kisasa ambayo hutumia injini ya kisasa zaidi aina ya Trent 1000 TEN. Bei yake inakadiriwa kuwa $224.6 milioni.

Injini hiyo inatumiwa katika ndege zote mpya aina ya Boeing 787 na huhifadhi mafuta, ambapo huwa inachoma mafuta kwa kiwango cha asilimia tatu chini ukilinganisha na ndege za aina hiyo na kuyatumia vyema zaidi.

Hilo huiwezesha kupunguza matumizi ya mafuta ukilinganisha na ndege nyingine za ukubwa kama wake kwa asilimia 20-25, aidha hupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kiwango sawa na hicho.

Aidha, huwa haipigi kelele sana. Ni ndege ambayo imechukua uwezo na kasi ya ndege kubwa aina ya 'jet' na kuuweka kwenye ndege ya ukubwa wa wastani.

Ina uwezo wa kubeba abiria 262 ni ya kisasa zaidi kuwahi kumilikiwa na serikali ya Tanzania. Mataifa mengine kama vile Kenya na Ethiopia hata hivyo yamenunua ndege kama hizo kadha.

Ndege hii ina uwezo wa kusafiri kiilomita 13,620 kwa wakati mmoja na urefu wake ni mita 57. Upana wa mabawa yake ni mita 60. Urefu wake kutoka chini hadi juu ni mita 17.

Rais Magufuli aligusia hilo aliposema: "Ndege hii ni ya kisasa na kote walikopita walikuwa wana uwezo wa kunipigia simu na kuongea nao angani."

Ethiopia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kando na Japan kuanza kutumia ndege aina ya Boeing 787-8 Agosti 2012.