COSTECH:Tumesikitishwa na kuvuja kwa barua iliyokusudiwa TWAWEZA

Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH, Dokta Amos Nungu amesema taarifa ya utafiti huo haikuwafikia
Image caption Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH, Dokta Amos Nungu amesema taarifa ya utafiti huo haikuwafikia

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania ( COSTECH) imesikitishwa na kuvuja mitandaoni kwa mawasiliano ya barua iliyoiandikia Taasisi ya utafiti isiyo ya Kiserikali ya TWAWEZA.

Barua hiyo kuhusu kulitaka Twaweza litoe maelezo ndani ya siku saba kuhusu utafiti ulioifanya wa Sauti za Wananchi bila ya kibali, ambao umeonesha pia kushuka kwa uungaji mkono wa wananchi kwa wawakilishi waliowachagua.

Twaweza: Umaarufu wa Rais Magufuli umeshuka

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo Dokta Amos Nungu amesema wameshangazwa kuona mawasiliano halali ya kiofisi yamesambazwa mitandaoni hata kabla ya kupata majibu rasmi.

Matokeo hayo ya utafiti, ndiyo yaliyoifanya Tume ya Sayansi na Teknolojia, ambayo ndiyo yenye jukumu la kuratibu, kufanya tathmini na ufuatiliaji wa tafiti, kuiandikia barua taasisi hiyo ya TWAWEZA, inayoonesha pia kwamba taasisi hiyo awali iliwasilisha maombi ya vibali vya kufanya utafiti nchini, lakini utafiti huo wa Sauti ya Wananchi haukujumuishwa.

Maelezo ndani ya barua hiyo imeitaka taasisi hiyo pia kutoa maelezo ndani ya ndani ya siku Saba.

Haki miliki ya picha TWAWEZA
Image caption Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya utafiti ya TWAWEZA

''Mtafiti akija kutoa matokeo ya utafiti kwenye vyombo vya habari pia tunaona kuwa utafiti ulifanyika, huu utafiti tunakiri kuwa hatuna taarifa yake sababu mtafiti anaposajiliwa mwishoni anapoondoka na taarifa zake lazima ripoti ibaki COSTECH.Tumewaomba wiki moja watupe maelezo'' Dokta Amos Nungu, Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia.

Wakenya wakasirishwa na safari ya wabunge Urusi

Kwa Picha: Magufuli akutana na marais wa zamani, na Lowassa

Na kuhusiana na hatua gani watakazochukua juu ya mawasiliano hayo ya ndani kusambaa mitandaoni, amesema hilo ni jukumu la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

''tume inasikitika kuwa mawasiliano halali ya kiofisi yanapelekwa mitandaoni tumeziachia mamlaka kufanya kazi yake''.Alieleza Dokta Nungu

TWAWEZA imekiri kupokea barua kutoka COSTECH ''tumeipokea na tunaifanyia kazi. Twaweza haijasambaza, na haihusiki na usambazaji wa barua hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Barua yoyote inayofika Twaweza inagongwa muhuri wa kupokelewa mbele ya mjumbe aliyeleta barua hiyo. Barua inayosambaa mtandaoni hatuitambui kwa sababu haina muhuri wetu wa kuipokea Twaweza. Tunaheshimu na kuthamini sana mawasiliano yetu na wadau wetu''Alieleza Aida Eyakuze Mkurugenzi mtendaji wa TWAWEZA

Hatua ya COSTECH kuhoji uhalali wa ripoti ya TWAWEZA imezua mjadala mkali mitandaoni nchini Tanzania.

COSTECH pekee ndio chombo cha kutoa ushauri katika masuala yote yanayohusu sayansi, teknolojia na uvumbuzi na moja ya majukumu yake ni kusajili na kutoa vibali vya tafiti zote za muda mfupi na mrefu zinazofanywa nchini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii