Aliko Dangote: Mtu tajiri zaidi barani Afrika asema hana wakati wa kutafuta mke

Aliko Dangote Haki miliki ya picha AFP

Baadhi ya watumiaji wa mtandao wa Twitter wamewasilisha maombi yao ya kutaka kuolewa na mtu tajiri zaidi barani Afrika Aliko Dangote, baada ya gazeti la Uingereza Financial Times kuripoti kwamba anatafuta mke.

''Umri wangu haupungui. Miaka sitini sio mzaha.... Lakini haiingii akilini kwenda kutafuta mtu iwapo huna muda huo'', bwana Dangote aliambia gazeti hilo.

''Hivi sasa sina wakati kwa sababu tuna kiwanda cha kusafishia mafuta, tuna kemikali za mafuta, tuna mbolea, tuna bomba la kusafirishia gesi," bwana Dangote alisema, akiongezea: Nahitaji kutulia kidogo.

Lakini baadhi ya watu walikasirishwa na lengo la mahojiano na tajiri huyo kuhusu maisha yake ya kibinafsi.

Dangote amewahi kuwaoa wanawake wengi ingawa habari kuwahusu wanawake wanaohusishwa naye huwa vigumu kuzithibitisha.

Hata hivyo, inafahamika kwamba aliwapa talaka wake wawili.

Ana watoto watatu walioorodheshwa rasmi, maarufu akiwa ni Halima Dangote aliyefunga ndoa mapema mwaka huu katika sherehe ya harusi iliyohudhuriwa na watu mashuhuri duniani akiwemo mwanzilishi wa Microsoft bwanyenye Bill Gates na Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete. Watoto hao wengine ni Fatima na na Mariya.

Yeye ni Mwislamu na dini yake inamruhusu kuwaoa wake wengi. Hata hivyo, licha ya kuwa na wake wengi taarifa zinasema hajawahi kuwa na zaidi ya mke mmoja kwa wakati mmoja. Kwa sasa, watu wamekuwa wakimchukulia kuwa asiye na jiko.

Aliko Dangote ni nani?

Aliko Dangote ndiye mtu tajiri zaidi mweusi duniani na mtu tajiri zaidi Afrika.

Alianzisha kampuni ya Dangote Cement na bado ndiye mwenyekiti wa kampuni hiyo. Dangote Cement inaongoza kwa kutengeneza saruji Afrika.

Dangote pia anamiliki kampuni za sukari, chumvi na za kusaga unga.

Kampuni yake ya Dangote Group inajenga kiwanda cha kusafisha mafuta karibu na Lagos, Nigeria ambacho kitakapomaliza kujengwa mwaka 2019 kinatarajiwa kuwa kikubwa zaidi cha aina yake duniani. Kiwanda hicho kitagharimu $9bn.

Dangote amehifadhi taji la kuwa mtu mweusi tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa takriban $14.1 bilioni.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii