Unai Emery: Mkufunzi wa Arsenal Emery anataka 'manahodha watano' katika klabu hiyo

Chanzo cha picha, Getty Images
Unai Emery (kulia) alimrithi Arsene Wenger, ambaye aliondoka baada ya kuongoza timu hiyo kwa miaka 22
Mkufunzi mpya wa Arsenal Unai Emery anasema kuwa anataka manahodha watano katika timu yake huku akijaribu kuwajua zaidi wachezaji wake.
Raia huyo wa Uhispania , ambaye alimrithi Arsene Wenger mwezi Mei , alisema kuwa Laurent Kolscieny atasalia kuwa nahodha wa timu hiyo.
''Wazo langu ni kumjua kila mchezaji na kwa undani. Tunataka kuweka heshima miongoni mwa wachezaji hao , kutafuta nahodha na kumchagua vizuri mchezaji bora kwa hilo''.
Beki wa kati wa Ufaransa Koscielny, 32, anatarajiwa kuhudumia jeraha hadi mwezi Disemba , sababu iliomfanya kukosa kushiriki katika kombe la dunia
Beki Stephan Lichtsteiner, ambaye ni mmojawapo wa wachezaji watano waliosajiliwa na Emery aliiongoza Switzerland nchini Urusi msimu huu.
"Wazo langu la kwanza ni kuwa na manahodha watano katika timu yangu, Emery aliongezea. Lakini kwa sasa siwajui majina yao. Tunajaribu kutazama wachezaji ambao wana tabia nzuri zaidi''
Kuondoka kwa Wilshere hakukusababishwa na majeraha
Emery pia alisema kuwa kuondoka kwa kiungo wa kati Jack Wilshere, ambaye aliondoka mwezi uliopita baada ya miaka 17 na amejiunga na West Ham haikuwa kutokana na majeraha yake.
Mchezaji huyo wa Uingereza ,26, alishiriki mara 25 katika msimu yake mitatu ya mwisho katika ligi ya Uingereza akiichezea Arsenal.
''Ulikuwa uamuzi wa busara na wa kiufundi'', alisema Emery. ''Nilimwelezea kuhusu wazo langu na vile nilivyotaka kujenga timu hiyo na nikamwambia kwamba sina uhakika iwapo atashiriki katika kikosi cha kwanza cha timu''.
''Najua kwamba mchezaji huyu ni mzuri kwa mashabiki na alikulia Arsenal, lakini sitampatia fursa katika kikosi cha kwanza na hiyo ndio sababu aliamua kuondoka hapa na naheshimu uamuzi wake''.
'Tuliwasajili wachezaji tuliohitaji'
Arsenal pia imemsajili kipa wa Ujerumani Bernd Leno na beki wa Ugiriki Sokratis Papastathopoulos, pamoja na kiungo wa kati wa Uruguay Lucas Torreira na kiungo wa kati Matteo Guendouzi, ambaye anaichezea timu ya Ufaransa ya wachezaji wasiozidi miaka 20.
Mkufunzi huyo wa zamani wa PSG na Sevilla alisema kuwa huenda usajili huo ndio wa mwisho.
''Pengine tunaweza kuleta mchezaji mmoja iwapo kuna sababu mwafaka za kutusaidia, lakini klabu hii imefanya kazi nzuri ya kuwasajili wachezaji wapya na tunafurahi''.
''Tuliwasaini wachezaji tuliowahitaji . Tutamsajili mchezaji mwengine mwezi ujao iwapo ni mchezaji mzuri sana''.