Fiat: Wafanyikazi wagoma baada ya mmiliki wa kampuni hiyo kulipa €112m kumnunua Ronaldo

Cristiano Ronaldo

Chanzo cha picha, AFP

Wafanyikazi katika kampuni ya kuunda magari ya Fiat Chrysler nchini Itali wanatarajiwa kugoma baada ya mwekezaji wake mkuu kuamua kulipa €112m (£99.2m) kumsajili Cristiano Ronaldo katika klabu ya Juventus.

Klabu hiyo na kampiuni hiyo ya kutengeza magari zinadhibitiwa na familia ya Agnelli kupitia kampuni yao ya uwekezaji.

Kulingana na muungano wa wafanyikazi wa USB, uamuzi huo unamaanisha kwamba Fiat imekosa mahala pa kuwekeza.

Umesema kuwa badala ya kampuni hiyo kuwahakikishia wafanyikazi wake hatma yao ya siku za baadaye, kampuni hiyo imeamua 'kumtajirisha mtu mmoja'.

Muungano huo umeongezea kwamba haitakubalika kwa kuwa wafanyikazi wa Fiat Chrysler wamekuwa wakijitolea kiuchumi huku mamilioni ya Yuro yakitumika kumnunua mchezaji mmoja.

Mkataba wa miaka minne wa kumvutia Ronaldo ulitangazwa siku ya Jumanne huku kukiwa na wasiwasi kwamba Juventus huenda ilimlipa zaidi mshambuliaji huyo wa miaka 33.

Hatahivyo mtaalam wa maswala ya kifedha katika kandanda Rob Wilson, kutoka chuo kikuu cha Sheffield Hallam, alisema kuwa Juventus inapaswa kupokea fedha zaidi ya malipo hayo ya Ronaldo ili kusimamia gharama za kifedha za uhamisho na mshahara wake.

Aliongezea: Mauzo ambayo Juventus itafanya yatakuwa muhimu sana. Yakiongezwa hapo kuna uwezekano mkubwa kwamba ataimarisha timu hiyo , inaonekana kuwa wazi kwamba watafanikiwa kwa kiwango kikubwa nyumbani na kufuzu katika kombe la vilabu bingwa Ulaya. Hatua hiyo ina inamaanisha kwamba watavutia fedha nyingi zaidi kutoka kwa runinga na fedha zaidi za kushinda mataji.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Tisheti za Ronaldo tayari zimeanza kuuzwa mji wa klabu ya Juventus

Akiwa mzaliwa wa kisiwa cha Ureno kwa jina Madeira, ambapo uwanja wa ndege umejengwa na kupewa jina lake , Ronaldo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa , akiifungia Real Madrid mabao 450 katika mechi 438.

Kama nahodha wa timu ya taifa ya Ureno katika kombe la dunia la 2018 World Cup, alifunga magoli manne , ikiwemo hat-trick dhidi ya Uhispania.

Ureno ilifuzu katika robo fainali ikilinganishwa na Itali ambayo ilishindwa kufuzu kwa kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu 1958.

'Mgomo hautakuwa na athari kubwa'

Ijapokuwa Juventus na Fiat Chrysler huendeshwa na kama kampuni tofauti, zote zinadhibitiwa na Exor, kampuni ya uwekezaji ya familia ya Agnelli.

Muungano wa USB umeitisha mgomo katika kiwanda hicho cha eneo la Melfi kusini mwa Itali, ambacho hutengeneza magari ikiwemo gari la Fiat Punto na 500X.

Wanachama wake watagoma siku ya Jumapili na kusalia katika mgomo hadi Jumanne itakayofuata.

Hatahivyo athari za mgomo huo hazitakua kubwa . Kiwanda hicho ni kimojawapo cha viwanda saba vya Fiat Chrysler na kwamba muungano huo hauwakilishi wafanyikazi zaidi.