Noura Hussein aliyehukumiwa kwa kumuua mumewe aliyembaka akata rufaa aachiliwe huru Sudan

Noura Hussein alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela

Chanzo cha picha, AMNESTY INTERNATIONAL

Maelezo ya picha,

Noura Hussein alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela

Mawakili wa msichana wa Sudan aliyemuua mume wake anayemtuhumu kumbaka, wamekata rufaa katika mahakama ya juu zaidi kutaka aachiliwe huru bila ya masharti yoyote.

Mwezi uliopita majaji walimuondolea Noura Hussein mwenye umri wa miaka 19 hukumu ya kifo na badala yake wakamhukumu miaka mitano gerezani .

Majaji pia waliagiza kuwa familia ya marehemu mume Abdulrahman Mohamed Hammad ilipwe $18,600.

Hukumu ya awali ya kifo ilizusha hasira kubwa, na nyota wa kimataifa kama mwanamitindo wa Marekani Naomi Campbell na muigizaji Emma Watson waliounga mkono kampeni iliyoanzishwa katika mitandao #JusticeforNoura, kutaka msichana huyo aachiwe huru.

Katika taarifa yake, Faiza Mohamed, mkurugenzi wa Afrika wa kundi la kutetea haki za wanawake Equality Now, amesema:

Noura ameteseka vya kutosha! Hakuna anayestahili kuolewa akiwa mtoto, abakwe na pia atakiwe kutumikia kifungo gerezani na alipe faini juu ya hayo yote.

Kwa hivyo, rufaa hii ni muhimu ili kuweza kusema - imetosha! Ukiukaji unapaswa kusita hapa na haki ni lazima itendeke."

Mnamo Mei, mahakama ilimhukumu Bi Husein kifo kwa kunyongwa, kufuatia kupatikana na hatia ya kutekeleza mauaji ya kupanga ya mumewe.

Bi Hussein amesema mumewe aliwaita jamaa zake wanaotuhumiwa kumshikilia kwa nguvu huku akim'baka.

Na wakati alipojaribu kuregelea kitendo hicho siku ya pili, alimuua kwa kumrukia na kumchomeka kisu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ndoa yake Noura Hussein

Mnamo 2015, Noura alipokea pendekezo la kuolewa kutoka jamaa wa familia yake mwenye umri wa miaka 32, Abdulrahman Mohamed Hammad. Noura alikuwa na umri wa miaka 16.

Mamake anasema kuwa Noura hakuonekana kuchukukizwa na wazo hilo, lakini aliomba aruhusiwe aendelee na masomo. Alipendekeza pia ndoa hiyo iahirishwe hadi mamake - ambaye alikuwa mja mzito wakati huo - ajifungue.

Lakini shinikizo la familia zikaongezeka - zikiwemo kutoka babake-Hussein.

"Wasichana wengi eneo hilo walikuwa wakipachikwa mimba na kupata watoto nje ya ndoa," anasema Hussein.

Hussein anaongeza kuwa hakutaka Noura naye akutwe na hali hiyo na asalie bila mume.

Licha ya kushiriki kwenye sherehe ya awali ya ndoa, ilibainika wazi kuwa Noura alikuwa anapinga wazo hilo.

Alitoroka hadi kwa shangaziye mji wa Sinnar, ulioko kilomita 350 na kusalia naye kwa siku mbili.

Alishawishiwa arejee nyumbani akifahamu kuwa ndoa hiyo haitakamilishwa.

Hata hivyo, alipofika tu, sherehe ilikuwa imekamilika. Lakini hakuhitajika kuishi na mumewe. Miaka miwili iliyofuata aliishi na familia yake.

Abdulrahman alipomtembelea ,alikuwa akimueleza wazi hakutaka kufunga ndoa naye.

Licha ya hayo, wazee wa familia walianza kusisitiza Noura na mumewe wahalalishe uhusiano wao na kuishi kama wanandoa.

Kulingana na mila yao, sauti ya wazee zilisikika na ndio waamuzi wa masuala muhimu.

Heshima na taji la familia ni mojawapo ya masuala muhimu kwenye tamaduni zao.

Babake Noura, Hussein anasema hakuona sababu ya bintiye kukataa uhusiano huo.

Familia ilikuwa na subra kwa miaka kadhaa.

Kwa lazima, Noura alikubali kuishi na Abdulrahman mwezi Aprili 2017.

Kulingana na taarifa zilizotibitishwa na CNN, Noura anasema kuwa alikataa kushiriki tendo la ndoa na mumewe wiki ya kwanza.

Alilia. Alikataa kula. Abdulrahman alipolala, alijaribu kuondoka chumbani, lakini ilifungwa.

Siku ya tisa, Abdulrahman aliwasili chumbani pamoja na jamaa wa familia waliorarua vazi lake na kumzuia sakafuni huku mume huyo akimbaka.

Siku iliyofuata, Abdulrahman alijaribu tena. Awamu hii Noura alichukua kisu alichomweleza mamake kuwa angekitumia kujiondoa uhai.

Noura alikamatwa na kuhukumiwa kwa mauaji ya kupangwa.