Faru 8 waliokuwa katika hatari ya kupotea, wafariki Kenya

Takwimu zinaashiria kuwa kuna faru chini ya 5,500 duniani

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Takwimu zinaashiria kuwa kuna faru chini ya 5,500 duniani

Faru wanane wanaripotiwa kufariki katika hali za kutatanisha kwenye mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Tsavo Mashariki nchini Kenya.

Duru ya siri aliyenukuliwa na shirika la habari la AP, ameshutumu kutowajibika kwa maafisa husika kwa vifo vya wanyama hao.

Faru hao 8 walikuwa kati ya wengine 14 waliosafirishwa kutoka mbuga za kitaifa za wanyama Nairobi na ziwa Nakuru kama njia ya kuwahifadhi, wiki mbili zilizopita.

Mradi huo uliendeshwa kwa ushirikiano kati ya shirika la huduma kwa wanyama pori Kenya KWS na shirika la kimataifa la uhifadhi (WWF).

Waziri wa Utalii Najib Balala amesitisha shughuli hiyo ya uhamisho wa faru kufuatia taarifa za vifo hivi.

Katika taarifa ya wizara ya Utalii, uchunguzi wa awali wa maafisa wa shirika la wanyama pori KWS umetaja kuwa vifo hivyo vimetokana na faru hao kunywa maji yaliokuwa na kiwango kikubwa cha chumvi walipofika katika maeneo mapya.

Mhifadhi maarufu wa mazingira nchini Kenya, Paula Kahumbu wa shirika la WildlifeDirect amateja vifo hivyo kuwa 'pigo kubwa'.

"Faru zimefariki, ni lazime tuseme wazi pindi ajali inapofanyika, sio kuripoti wiki, mwezi mmoja baadaye," alisema.

"Lazima kuna kosa lilitendeka mahali na tunataka kujua kosa lenyewe."

"Uhamishaji wa wanyama hawa kimo hiki imejaa changamoto na haikosi hatari. Hata hivyo faru weusi wamo hatarini zaidi kutokana na uwindaji haramu kwa hivyo juhudi hizi za kuwaokoa kutoka hatari kama vile kuwahamisha ni muhimu kwa vizazi," WWF ilianika kwenye taarifa iliyotoa ijumaa

Safari ya wanyama hawa huhusisha kudungwa sindano za kupooza wakiwa safarini kabla ya kufufuliwa tena baadaye katika njia moja hatari.

Faru 70 wanahifadhiwa katika mbuga ya ziwa Nakuru eneo la bonde la Ufa Kenya

Kulingana na shirika la Save the Rhinos takriban faru weusi 5,500 wamesalia duniani wote wakiwa barani Afrika.

Wakati huo huo, shirika la uhifadhi WWF limeripoti kuwa faru weusi nchini Kenya wamesalia 750.

Idadi hiyo inatrajiwa kupungua kwani tayari shirika la Wanyama pori KWS, limesema faru tisa waliuawa mwaka uliopita nchini .