Hezron Mogambi: Ziara ya Obama ya sasa ina maana gani kwa Kenya?

Marekani

"Kenya iko kwenye njia panda," alionya Rais wa zamani wa Amerika Barack Obama mnamo Julai 2015 alipokuwa anamaliza ziara yake nchini Kenya.

"Mnaweza kuamua kuchukua njia ya maendeleo, lakini hili lahitaji kuchukua baadhi ya hatua muhimu."

Yamkini matamshi haya ndiyo nguzo ya ziara ambayo anaifanya Rais mstaafu wa Marekani Obama nchini Kenya huku ziara za kiongozi huyu mstaafu wa Marekani na viongozi wengine wa nchi nyingine tangu kutoka afisini zikikosolewa na wengine.

Tangu kutoka uongozini amekutana na kufanya mazungumzo na pamoja na kiongozi wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, Rais wa Uchina Xi Jinping, Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, Rais wa Argentina Mauricio Macri na Waziri mkuu wa India, Narendra Modi.

Katika ziara hizi zote, Obama amekuwa akizungumzia kuhusu masuala kuhusu kujenga mazingira bora ya kibiashara yanayolenga kuwafaidi vijana, uchumi, uhifadhi wa mazingira, uvumbuzi na uongozi bora.

Ni katika muktadha huu ndio ziara ya siku moja ya Obama nchini Kenya inaweza kuangaliwa.

Haki miliki ya picha UHURU KENYATTA/TWITTER
Image caption Bw Obama (kati), dada yake Bi Auma Obama na Rais Kenyatta baada ya rais huyo wa zamani wa Marekani kuwasili Nairobi

Aidha, ziara ya sasa ya Rais Obama nchini Kenya inatokea katika mazingira tofauti ya kisiasa na ambayo yanapigia upatu lengo lake. Alipozuru Kenya mwaka wa 2015, Serikali na upinzani zilikuwa katika hali ya kutoelewana kuhusiana na masuala mbalimbali ya kitaifa.

Uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 ulizidisha uhasama baina ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na upinzani ukiongozwa na Raila Odinga. Hata hivyo, baada ya muafaka wa tarehe 9 Machi mwaka huu baina ya kinara wa upinzani Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, kumekuwepo na utulivu nchini Kenya.

Hata hivyo, bado kuna mjadala na hisia nchini Kenya kuwa changamoto zinahusiana na uongozi bora, ufisadi, suala la vijana na ajira na jinsi ya kujumuisha jamii katika uongozi katika ngazi mbali mbali.

La mno ziaidi, Rais Kenyatta ameanzisha vita vipya na vinavyoonekana na wengi kuwa na mashiko dhidi ya ufisadi ambavyo vimeshika kasi na kuhusisha taasisi mbali mbali nchini na nje ya nchi.

Ufisadi umekuwa donda ndugu nchini Kenya huku wakuu wa mashirika ya serikali wakikashifiwa kwa kushiriki kula mlungula katika mashirika wanayoongoza na serikali kushtumiwa kwa kutochukua hatua yoyote.

Ni juma lililopita tu ambapo Rais wa Uswizi Alain Berset alizuru nchi ya Kenya ambapo nchi hizi mbili zilitia saini makubaliano ya kurejesha mali yote yaliyoibwa kutoka Kenya na kufichwa nchini Uswizi.

Katika makubaliano haya, mali itakayolengwa kwanza ni pesa zilizopoibwa kutokana na kashfa ya Anglo-Leasing na ambazo zimefichwa nchini Switzerland.

Huwezi kusikiliza tena
Obama akiondoka afisi yake White House mara ya mwisho

Mwaka uliopita, Switzerland ilieleza kwamba ilikuwa imefungia Sh200 million ambazo zilikuwa zimefichwa nchini humo kutoka na kashfa hiyo. Wakati huo huo, nchi hiyo ilikuwa imerudisha kima cha $1.2 billion nchini Nigeria—$722 milioni mwaka wa 2005 na $322 milioni kati ya mali zilizoibwa wakati wa uongozi wa dikteta Sani Abacha, kama njia ya kusafisha jina la taifa linalotumika kuficha mali ya umma iliyoibwa kutoka mataifa mbali mbali.

Obama alihoji kwamba viongozi walihitaji kujikakamua zaidi na kuhakikisha kuwa wanafikia maono ambayo viongozi waanzilishi wa Kenya wakati wa uhuru waliokuwa nayo: kupigana dhidi ya ujinga, umaskini na magonjwa.

Alipozuru Kenya mwaka wa 2015, Obama alizieleza sababu zizi hizi; kwamba ufisadi unashamiri kwa sababu ya uongozi mbaya, kutojali hali ya taifa na wananchi, utendakazi mbaya miongoni mwa maafisa wa serikali, kukosa uvumilivu, ukabila, na siasa mbaya kama mambo ambayo yamelifanya taifa la Kenya kutofikia azma yake tangu uhuru.

Kulingana takwimu ambazo hazijadhibitishwa, ufisadi nchini Kenya huwanyima vijana nafasi za kazi zipatazo robo milioni. Uchunguzi na utafiti uliofanywa na tume ya maadili na ufisadi chini Kenya mwaka wa 2016 ulionyesha kwamba takriban Wakenya 8 kati ya 10 waliamini kuwa hali ya ufisadi ilikuwa juu sana. Takwimu rasmi za Serikali ya Kenya zinaonyesha kuwa ufisadi huchukua angalau Kshs. 700Bilioni kutoka kwa bajeti ya Kenya kila mwaka ilhali katika bajeti ya taifa la Kenya ya takriban shilingi 3 trillioni, nchi ya Kenya bado hutegemea usaidizi wa karibu Shs 500Bilioni. Hii inamaanisha kwamba, ulipaji wa madeni unachukua zaidi ya asilimia 45 ya ushuru wote unaokusanywa nchini Kenya.

Huwezi kusikiliza tena
Urais wa Obama ulivyobadilisha Kogelo, Kenya

Ziara hii itakuwa ya kwanza baada ya kuondoka afisini kama Rais wa Marekani Januari 20, mwaka uliopita, Obama amewahi kuzuru Kenya mara tatu mnamo 1987, 1992 na ziara ya mwaka wa 2015 wakati wa hatamu yake ya pili akiwa Rais wa Marekani.

Duru zimearifu kwamba Obama ambaye ana ushawishi na uungwaji mkono serikalini na katika upinzani, atakutana na viongozi wa upinzani kama njia moja ya kuhakikisha kuwa ujumbe wake ziarani unaeleweka na kutiliwa maanani zaidi.

Jumapili tayari alikutana na kiongozi mkuu wa upinzani Kenya Raila Odinga.

Haki miliki ya picha RAILA ODINGA/TWITTER

Alipozuru Kenya mwaka wa 2015, Obama alieleza kwamba angependa kuzuru Kenya baada ya kutoka afisini kama Rais wa Marekani. Nchi ya Kenya ina maana kubwa kwa Obama - hapa ni kama kurudi nyumbani - na hapa ana kukumbuka misingi ya uhai wake na babake.

"Ninajua kuna sehemu zingine za kuvutia za nchi hii ambazo sijazitembelea.

Nitahakikisha kuwa nitarudi tena na sio tu Kenya lakini nchi za karibu kama Uganda hadi Tanzania. Kuukwea mlima Kilimanjaro yaonekana kama jambo ambalo linafaa kuwa katika mambo ambayo ningependa kuyafanya baada ya kutoka uongozini," alieleza mnamo 2015.

Hata hivyo, kulingana na jinsi safari yake ilivyopangwa wakati huu, huenda asiweze kuzuru maeneo mengi alivyoahidi mwaka wa 2015 kwani atakuwa nchini Kenya kwa siku moja tu.

Siku ya Jumatatu, Julai 16, atazindua kituo cha Sauti Kuu Sports, Resources and Vocational Training Centre ambacho kinasimamiwa na dadake, Dkt. Auma Obama. Baadaye, ataelekea Afrika Kusini ambako anatarajiwa kutoa hotuba maalum Julai 17, 2018 yenye kichwa "Renewing the Mandela Legacy and Promoting Active Citizenship in a Changing World."

Ujumbe wa Obama hapa utahusiana na haja ya vijana kujihusisha zaidi na uongozi ambapo atawazungumzia viongozi chipukizi wapatao 200 ambao wameteuliwa kujiunga na Obama Foundation Leaders ambalo ni shirika lake linalohimiza uongozi bora na demokrasia duniani.

Kutokana na hali iliyoko nchini Kenya na hotuba yake inayotarajiwa nchini Afrika kusini, ni wazi kwamba Rais Obama atalenga ujumbe wa kuhimiza demokrasia zaidi na usawa katika jamii, na haja ya kufanya kazi pamoja badala ya migawanyiko katika jamii.

Obama atatoa hotuba yake katika kile wengi nchini Afrika Kusini wanakiona kama sherehe ya miaka 100 ya siku ya kuzaliwa kwa Nelson Mandela, Rais wa Kwanza wa Afrika kusini ambaye pia anajulikana kama shujaa wa usawa na ukombozi ulimwenguni kote. Mandela aliaga dunia mwaka wa 2013 akiwa na umri wa miaka 95.

Ni mazingira kama haya ya Kenya na Afrika kusini ndipo Rais Obama atapopata muktadha mzuri wa kuhutubia na kuwahimiza viongozi kuhusiana na haja ya kuvumiliana, kujali na kufanya kazi na wengine na pia kupanua demokrasia hasa wakati kuna changamoto nyingi kuhusiana na ukumbusho wa maisha ya Nelson Mandela na yale aliyoyapigania si Afrika Kusini tu, bali kote duniani.

Prof. Mogambi ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi@yhaoo.co.uk

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii