Dereva aliyetumia gari la kuwabebea wagonjwa kusafirishia mirungi Tanzania akamatwa

Mirungi imepigwa marufuku nchini Tanzania licha ya kuuzwa nchini Kenya na Somalia

Dereva wa ambalensi nchini Tanzania anazuiliwa na maafisa wa polisi baada ya kunaswa akisafirisha mifuko ya mirungi akitumia gari hilo la kusafirishia wagonjwa kuelekea mjini Mwanza.

Siku zake zilikuwa zimefika kwani licha ya kutumia king'ora kukwepa msongamano wa magari na maafisa wa polisi, hakufanikiwa.

Jarida la AFP limenukuu Gazeti la Mwananchi lililomtaja dereva wa gari hilo kukataa ombi la kumfikisha mgonjwa hospitalini huku akidai gari hilo 'halikuwa na uwezo' na kuongeza kuwa alikabidhiwa na masuala ya kifamilia.

Maafisa wa serikali Tanzania walimnasa jamaa huyo baada ya kugundua kuwa 'mgonjwa' wake alikuwa mirungi

Gari hilo lilipatikana limesimama eneo tofauti na kusababisha wasiwasi kwamba lilikuwa na mipango fiche.

Mihadarati hiyo ilikuwa inasafirishwa kutoka Kenya kutumia mpaka wa Sirari eneo la Tarime.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Mara, Juma Ndaki, wahusika wa sakata hilo wamekamatwa huku uchunguzi ukiendelea juu ya mpango huo wa kutumika kwa gari la kuitumikia jamii.

Hata hivyo mmoja wa wasimamizi wa hospitali ya Tarime, amejitenga na sakata nzima huku akilitaja tukio hilo kuwa lenye maudhi.

Mirungi maarufu Khat imepigwa marufuku Tanzania licha ya majani hayo kuvuma sana mataifa ya Kenya na Somalia.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii