Magufuli: Wafungwa wafanyishwe kazi usiku na mchana na wazembe wapigwe mateke

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimvalisha cheo Phaustine Martin Kasike kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania, Ikulu jijini Dar es Salaam.Julai 14,2018 Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Dkt Magufuli akimvalisha cheo Phaustine Martin Kasike kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa wafungwa wanapaswa kufanyishwa kazi usiku na mchana na kwamba wafungwa wazembe wanafaa 'kupigwa mateke'.

Magufuli alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa afisa mkuu mpya wa Magereza nchini humo .

Amesema kuwa ilikuwa aibu kwa Tanzania kuendelea kuwaachilia huru wafungwa na kwamba watu hao wanapaswa kulima chakula chao katika shamba.

Anasema kuwa kutofanyishwa kazi kwa wafungwa kumesababisha kuwepo kwa wapenzi wa jinsia moja na matumizi ya mihadarati katika jela.

Ametoa wito wa kusitishwa kwa wanawake au wanaume kutembelea wake zao au waume zao jela.

Dkt Magufuli alimtaka Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) mpya Phaustine Martin Kasike kurekebisha dosari zilizopo katika Jeshi la Magereza, zikiwemo Serikali kubeba mzigo wa kuwalisha wafungwa badala ya wafungwa kufanya kazi za uzalishaji wa chakula, udhibiti mbaya wa wafungwa ambao unasababisha baadhi yao kufanya uhalifu wakiwa magerezani.

Maslahi ya askari wa magereza

Alimtaka pia Bw Kasike kushughulikia suala la maslahi duni ya Maafisa na Askari Magereza yanayosababishwa na kutopandishwa vyeo.

Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Magufuli akizugumza na Maafisa mbalimbali kutoka Jeshi la Magereza Tanzania

"Nataka kuona Askari Magereza wawe na hali nzuri, wapandishwe vyeo, walipwe maslahi yao na waishi katika makazi bora" alisema Rais Magufuli.

Makundi ya wanaharakati yamemshutumu kiongozi huyo kwa kushindwa kuwavumilia wapinzani wake wa kisiasa , makundi ya wapenzi wa jinsia moja na makundi mengine.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii