Trump asema ana matumaini kidogo kuhusu mkutano wake na Putin

Viongozi hao wanaripotiwa kuwa watazungumzia masuala kuhusu uhusianno wa nchi zao na masuala ya usalama siku ya Jumatatu
Maelezo ya picha,

Viongozi hao wanaripotiwa kuwa watazungumzia masuala kuhusu uhusianno wa nchi zao na masuala ya usalama siku ya Jumatatu

Rais wa Marekani Donald Trump amesema ana ''matumaini madogo'' kuhusu mkutano wake na Rais wa Urusi Vladmir Putin utakaofanyika Finland siku ya Jumatatu

Lakini amekiambia kituo cha habari cha CBS kuwa ''hakuna kilichoharibika'' na ''labda kutaibuka jambo zuri''kutokana na mkutano huo.

Amesema pia kuwa ataibua suala la maafisa 12 wa intelijensia wa urusi walioshutumiwa kufanya udukuzi katika uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Urusi inakana shutuma hizo.

Wito umekuwa ukitolewa nchini Marekani ukimtaka Trump kuahirisha mkutano wake na Putin kutokana na shutuma zilizotolewa siku ya Ijumaa na naibu mwanasheria wa serikali ya Marekani Rod Rosenstein.

Urusi imesema mazungumzo haya wanategemea kuwa chachu ya kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Trump aliiambia nini CBS?

Alisema ''anaamini katika mikutano'' akasema mikutano yake na viongozi wa Korea Kaskazini na China ilikuwa ni ''kitu kizuri sana''.

''Nafikiri ni jambo zuri kukutana.Ninaamini katika mikutano, naamini kuwa kuwa na mkutano na Kim ni jambo zuri,nafikiri kuwa na mkutano na Rais wa China lilikuwa jambo zuri.hivyo kuwa na mkutani na Urusi, Cina na Korea Kaskazini , ninaamini kwenye hayo, hakuna jambo baya litakalojitokeza kutokana na kukutana kwetu, labda ''jambo zuri litajitokeza''.Alisema Trump

''Siwezi kusema nini kitatokea, lakini naweza kukwambia ninachokiombea, na tutaona kama kuna jambo litatokea''.

Trump alirudia kauli yake ya kukosoa utawala wa Obama,ambaye alikuwa madarakani wakati vitendo vinavyodaiwa kuwa vya udukuzi vilipofanyika.

''hili lilikuwa wakati wa utawala wa Obama, walikuwa wanafanya chochote walichokuwa wanakitaka wakati wa utawala wa Obama''.Alisema

Shutuma zinadai kuwa Raia hao wa urusi walianza mashambulizi ya mtandaoni mwezi Machi mwaka 2016 kwenye anuani za barua pepe za wafanyakazi waliokuwa katika Kampeni za urais za Hillary Clinton.

Wanashutumiwa kutumia mfumo uitwao Keystroke kumpeleleza Mwenyekiti wa chama cha DNC na kuingia kwenye Kompyuta za chama hicho.

Maelezo ya picha,

Wanaandamanaji nchini Finland wamekuwa wakimtaka Trump kutazama masuala ya haki za binaadamu atakapokuwa nchini humo

Viongozi wakuu wa Democrat akiwemo mwenyekiti wa chama Tom Perez amemtaka Trump kuachana na mazungumzo hayo akidai kuwa Putin ''si rafiki wa Marekani''.

Kwa upande wa Republican, Seneta John Mccain amesema mkutano ''usiendelee'' isipokuwa tu kama Rais ''amejiandaa kumuwajibisha Putin''.

Mwanasheria Robert Mueller anachunguza yale yaliobainishwa na intelijensia ya Marekani kuhusu uchaguzi wa mwaka 2016

Siku ya Ijumaa, watu 32 wengi wao raia wa Urusi walishtakiwa bila wao kuwepo mahakamani kadhalika makampuni matatu na washauri wanne wa zamani wa Trump.

Mshauri wa masuala ya usalama wa zamani Michael Flynn na George Papadopoulos aliyekuwa mshauri wa sera za mambo ya nje walikutwa na hatia ya kusema uongo kuhusu mawasiliano na raia hao wa Urusi.

Aliyekuwa meneja wa kampeni za Trump Paul Manafort na makamu wake Rick Gates walishtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha kwa ajili ya kazi zao za kisiasa nchini Ukraine