Barack Obama aondoka Tanzania baada ya mapumziko Serengeti, atua Kenya na kukutana na Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Obama na Mahiga Haki miliki ya picha MSEMAJI WA SERIKALI TANZANIA
Image caption Bw Obama na Dkt Augustine Mahiga

Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama amehitimisha ziara yake nchini Tanzania ambayo ilikuwa ya mapumziko na kuelekea Kenya.

Bw Obama amekuwa kwenye hifadhi ya taifa ya Serengeti kwa usiri mkubwa, ingawa ilifahamika kwamba angewasili nchini Kenya na kuhudhuria sherehe ya uzinduzi wa kituo kimoja cha hisani eneo alikozaliwa babake Kogelo, Siaya magharibi mwa Kenya.

Msemaji wa serikali ya Tanzania ameandika kwenye Twitter: "Rais Mstaafu wa Marekani @BarackObama amehitimisha mapumziko ya siku 8 pamoja na familia yake katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini."

Baada ya kuwasili, alikutana na Rais Uhuru Kenyatta na baadaye akakutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Obama na wageni wake watahudhuria uzinduzi wa Sauti Kuu, Shirika lisilokuwa la kiserikali la kuwawezesha vijana lililoanzishwa na dadake wa kambo Auma Obama katika eneo la Kogelo kaunti ya Siaya siku ya Jumatatu.

Haki miliki ya picha MSEMAJI WA SERIKALI TANZANIA
Image caption Bw Obama na Dkt Augustine Mahiga

Picha zilizopakiwa mtandaoni na msemaji huyo zinaonesha alisindikizwa uwanja wa ndege na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Dkt Augustine Mahiga.

Bw Obama amelakiwa nchini Kenya na rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi.

Haki miliki ya picha UHURU KENYATTA/Twitter
Image caption Uhuru Kenyatta na Bw Obama ikulu, Nairobi
Haki miliki ya picha UHURU KENYATTA/TWITTER
Image caption Bw Obama (kati), dada yake Bi Auma Obama na Rais Kenyatta baada ya rais huyo wa zamani wa Marekani kuwasili Nairobi
Haki miliki ya picha UHURU KENYATTA/TWITTER
Image caption Bw Obama na Bw Kenyatta wakitembea ikulu, Nairobi. Nyuma yao ni Bi Auma Obama
Haki miliki ya picha RAILA ODINGA/TWITTER
Image caption Bw Obama na Bw Odinga
Haki miliki ya picha RAILA ODINGA/TWITTER

Maelezo kuhusu safari za Obama yamewekwa siri kuu kwa sababu ya maswala ya kiusalama.

Hii ni ziara ya nne ya Obama nchini Kenya.

Babake alizaliwa katika eneo la Kogelo mjini Siaya.

Waandalizi wa hafla hiyo wamedai ukosefu wa eneo kubwa la kufanyia sherehe hiyo Siaya kuwa sababu kuu ya raia wengi kutoruhusiwa kuhudhuria uzinduzi huo.

''Kutokana na udogo wa eneo, hafla hiyo itahudhuriwa na watu wachache huku vyombo vichache vya habari pia vikiruhusiwa'', ilisema taarifa ya waandalizi,

Mjini Kisumu skrini kubwa zitawekwa katika uwanja wa michezo wa Jomo Kenyatta ili umma kufuatilia ziara hiyo ya Obama.

Siku ya Jumatatu Obama anatarajiwa kuelekea Kisumu ambapo atapokewa na Gavana wa mji huo Anyang' Nyong'o kabla ya kuelekea Siaya.

Atakapowasili mjini Siaya rais huyo wa zamani wa Marekani atapokewa na Gavana wa Siaya Cornel Rasanga kabla ya kusafirishwa hadi katika kijiji cha Kogelo ambako familia yake ya kenya inatoka ili kuzindua wakfu huo wa Sauti Kuu.

Image caption Obama na dadake wa kambo Auma Obama

Wawakilishi , wasomi, viongozi wa dini na viongozi wa kijiji walikutana mjini Kogelo siku ya Ijumaa katika kile kiongozi wao alisema kwamba wanajadiliana jinsi ya kumkaribisha bwana Obama.

"Tulikuwa tukijadiliana kuhusu tutakavyomkaribisha. Pia tumejadiliana kuhusu mahitaji ya jamii ambayo tutataka kuwasilisha kwa Obama siku ya Jumatatu, Nicholas Rajula aliambia gazei la Daily Nation nchini Kenya.

''Tunataka kumkaribisha katika kijiji kwa njia ya Kiafrika. Hii itafanyika iwapo kutakuwa na raia wengi. Kwa sababu hiyo tunataka kutoa ombi kwa waandalizi kumruhusu mwana wetu kuhutubia umma kwa ufupi, sio lazima katika eneo la hafla hiyo kwa kuwa ni dogo mno kuruhusu kila mtu kuingia.

Baada ya ziara yake nchini Kenya Obama ataelekea Afrika Kusini.

Hii itakuwa ziara yake ya kwanza nchini Kenya tangu kuondoka madarakani mnamo mwezi Januari 20 mwaka 2017.

Amezuru nchini Kenya mara tatu 1987, 1992 na 2015 wakati alipokuwa akihudumu kwa awamu ya pili ya urais.

Mada zinazohusiana