Kombe la Dunia 2018: Fainali iliyoweka kikomo Kombe la kukata na shoka

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Paul Pogba akisherehekea ushindi na mama yake Yeo Pogba na ndugu zake Florentin Pogba na Mathias Pogba

Ni Fainali iliyoshuhudia mambo yote - maamuzi ya kutatanisha, mashabiki wa kuvuruga mechi, goli la kwanza la kujifunga wenyewe fainali ya Kombe la Dunia, chipukizi wa kwanza kutikisa wavu tangu Pele, na masihara ya kuchekesha ya kipa.

Ufaransa iliiadhibu Croatia 4-2 kutawazwa mabingwa wa dunia kwa mara ya pili na kulikunja jamvi la Kombe litakalosalia kuwa kumbukumbu kwa kipindi kirefu.

Kwa hakika, fainali ilikuwa kama muhtasari wa mechi zote Urusi.

Mchuano wenye mabao mengi

Imekuwa ni ada au kawaida kama sheria kwa fainali ya Kombe la Dunia kukumbwa na uhaba wa mabao.

Lakini fainali hii imekuwa ni ya aina yake kwa kuadikisha idadi sawa ya mabao na yale yote yaliyofungwa kwenye Makala manne yaliyoitangulia kwa jumla.

Mwisho ambapo mechi ya fainali ilisajili mabao mengi ilikuwa ni 1998 - wakati Les Bleus ilinyanyua Kombe la Dunia.

Aidha fainali ya 2018 imefikia idadi ya mabao yaliyoanikwa kimiani mnamo 1958 Brazil ilipoiliza Sweden 5-2.

Beki mstaafu wa England Rio Ferdinand ameiambia BBC: "Wakati mwingine mechi kama hizi huwa ni za kuchosha lakini fainali hii imekuwa ni tofauti kabisa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Refa Nestor Pitana wa Argentina, Kylian Mbappe na Pogba na Rakitic wa Croatia

Croatia nayo inastahili kongole kwa namna walivyoishambulia Ufaransa."

Nahodha wa zamani wa England Alan Shearer aliongezea: "Ingawa waliponea kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa kileleni, Ufaransa ilibadilika kabisa awamu ya pili.

Walipata namna ya kuwajumuisha na kujinufaisha kwa Antoine Griezmann na Kylian Mbappe mechini huku wakiimarisha safu ya ulinzi.

"Pongezi kocho kocho kwao, wamekuwa ni wa ajabu kweli."

Shindano hili limekuwa na magoli 169 - mawili tu chini ya magoli 171 yaliyoandikishwa 2014 nchini Brazil na 1998 nchini Ufaransa.

Kombe la Dunia 2018: Antoine Griezmann apachika penalti yenye utata iliyotolewa kupitia VAR.

Hili ni Kombe la kwanza kuamuliwa kutumia mbinu ya refa msaidizi kwa njia ya kiteknolojia maarufu (VAR).

Baada ya kutumika mara kwa mara mechi ya makundi, ilisahaulika kwa muda mechi za mchujo. Lakini ilishirkishwa tena baadaye katika fainali kuitunuku Ufaransa penalti.

Mlinzi Samuel Umtiti aliponyoa krosi iliyopeperushwa na Griezmann hadi kugusa mkono wa Ivan Perisic, refa hakupeana chochote.

Lakini,baada ya kipindi kirefu cha mazungumzo na mashauriano na VAR, alienda kutazama kwenye runinga - na kupeana penalti.

Ingawa wengi waliudhika na VAR, ni vyema kufahamu kuwa uamuzi wa kutoa penalti ulifanywa na refa Nestor Pitana, sio mtambo. Antoine Griezmann alifunga.

Uamuzi huu ulivutia hisia mbalimbali.

Wakati wa kipindi cha mapumziko, Shearer alikashifu vikali uamuzi huo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Antoine Griezmann wa Ufaransa akifunga penalti

"Ni aibu kubwa iwapo uamuzi huu utabadili mkondo wa mechi," alisema. "Perisic hakukusudia kuunawa na kwa hivyo haifai kuwa penalti. Awali refa hakutoa penalti hiyo, inakuwaje ghafla alihisi kuwa alikosea baada ya kutathmini VAR?

Ferdinand alikubaliana naye: "Maamuzi mawili duni yamebadili mechi nzima. Mpira ulikuwa karibu sana na Ivan Perisic na hata hakuwa na nafasi ya kuwaza. Asingeweza kukusudia kuunawa Mpira.

"Refa pia alichukua muda mrefu kumaanisha hakuwa na uhakika! Imekuwa ni kama utani na jambo la kuchekesha."

Mfungaji wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann alichangia: "Wakati unakosa uhakika au kujawa na wasiwasi,usipeane penalti. Ni uamuzi wa kimakosa."

Griezmann alitia kimiaini penalti ya 22 kufungwa kombe hili - ikiwa ni rekodi. Ilikuwa ni ya 29 kutolewa, na kuvuka idadi ya penalti zote za awali tangu 1966 tangu takwimu zilipoanza kusajiliwa.

Kwa mara ya kwanza goli la kujifunga lapatikana fainali ya Kombe la Dunia.

Kombe la Dunia 2018: Goli la wenyewe kutoka mfungaji wa Croatia Mario Mandzukic iliiweka Ufaransa mbele.

Hili lilikuwa Kombe la Dunia lenye mabao mengi ya kujifunga - 12 kwa jumla. Si vibaya fainali pia kushuhudia lake.

Mpira wa kichwa wa Mario Mandzukic baada ya Griezmann kungurumisha frikiki - iliyoipa Ufaransa uongozi 1-0 ilimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kujifunga pambano la fainali ya Kombe la Dunia.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kipa wa Ufaransa Hugo Lloris akijutia bao la Mario Mandzukic

Hii ina maana kuwa mabao ya kujifunga wenyewe yamekuwa maradufu na kumpiku mfungaji bora wa Kombe hili - Harry Kane aliyeweza kufunga sita Urusi.

Baada ya goli hilo, mchezaji mstaafu wa England Chris Waddle alifafanua Urusi 2018 kuwa Kombe la "krosi na vichwa".

Alikuwa na kauli muhimu - 73 kati ya mabao 169 yaliyofungwa Urusi yametokana na vichwa sawa na (aslimia 43%) - mengi zaidi tangu 1966 uandishi wa takwimu ulipoanza.

Kinda wa kwanza kutandika bao tangu gwiji Pele

Kombe la Dunia 2018: Goli la Kylian Mbappe lilizidisha uongozi wa Ufaransa

Kylian Mbappe alikuwa ni chipukizi wa tatu kushiriki mechi ya fainali Kombe la Dunia - na kuishia kuwa wa pili kujipa bao katika mechi hiyo - tangu Pele kubandika mawili dhidi ya Sweden 1958.

Awali kwenye shindano hili, Mbappe alipiga maonyesho ya kustajabisha mno kwa kuanika mabao mawili dhidi ya Argentina - na kumwezesha kuwa chipukizi wa kwanza kufanya hivyo tangu shujaa wa zamani wa Brazil.

Ingawa ni vigumu kujadili kuwa Mbappe, mchezaji aliyeigharimu Paris St-Germain pauni milioni £159m - alijitangaza rasmi katika shindano hili - lakini chipukizi huyu mwenye miaka 19 amedhibitisha ni kwa nini ameigharimu PSG pesa kiasi hicho - aliondoka Urusi na mabao manne na kukabidhiwa tuzo ya nyota mwenye umri mdogo Kombe la Dunia 2018.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kylian Mbappe akibusu Kombe la Dunia baada ya ushindi

Rio Ferdinand amemsifia kuwa ametosha kuwarithi Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambao walitamalaki soka kwa kugawana taji la Ballon d'Or ndani ya kipindi cha miaka 10.

"Tutamuona akisimama kwenye jukwaa hivi karibuni akiwa tayari kupokea Ballon d'Or miaka ijayo," alimaliza Ferdinand.

"Kufika Kombe la Dunia macho yote yakielekezwa kwako, na kufanya hivi ukiwa na miaka 19...sio rahisi....tena kuandikisha bonge la bao. Ni umahiri wake na uamuzi bora alionao mbele ya nyavu.

Kylian Mbappe ana mazoea ya kufanya uamuzi wa uhakika. Huu ni ukomavu unaomzidi umri."

Klinsmann naye amezidi: "Mengi yanasubiriwa kutoka kwake siku za usoni. Tayari ametetemesha soko la kuwasajili wachezaji.

Huku Ronaldo akikamilisha uhamisho wake naye Neymar akihusishwa na vilabu vingine, si ni vigumu kutabiri kinda huyu ataishia wapi?

"Kinachonivutia zaidi ni kuwa yuko kwenye kikosi cha Ufaransa ambacho ni kama familia moja. Anacheza kwa utulivu na kujiamini, utadhani amekuwa akiitumikia timu kwa miaka 10 hivi."

Masihara ya maudhi.

Kombe la Dunia 2018: Kosa la kijinga la kipa wa Ufaransa Hugo Lloris liliifufua Croatia

Katika msimu ambao kipa wa Liverpool Loris Karius alionekana kufanya kosa kubwa kuwahi kuonekana alipokuwa akicheza fainali ya Champions League kwa kumpa bao bilashi Karim Benzema, ni Hugo Lloris alikuwa na muda wa aibu kwa kujidhalilisha mbele ya maelfu uwanjani Luzhniki.

Samuel Umtiti alimpa pasi nahodha wake anayeichezea Tottenham. Lloris alijaribu kumla chenga Mandzukic - lakini ole wake, alifanikiwa tu kumpigisha mpira mfungaji huyo hadi wavu wake alioutelekeza.

Hugo Lloris anadhani alikuwa anafanya nini? Yuko katika fainali ya Kombe la Dunia na ameadhibiwa kwa utani wake usiostahili," alimkashifu beki wa zamani wa Arsenal na England Martin Keown.

Ndilo kosa kubwa zaidi lililoshuhudiwa Kombe la Dunia hata ingawa kipa wa Ujerumani Manuel Neuer alipoteza mpira akiwa yadi 80 mbali na lango na kuipa Korea kusini goli la pili lililowatema nje ya Kombe la Dunia katika hatua ya makundi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kipa wa Ufaransa Hugo Lloris akijutia baada ya kusababisha Croatia kufunga bao la pili

Goli hilo lilimfaa Mandzukic kwani alijizolea sifa baadaye.

Amejiunga na mabingwa waliomtangulia kwa kuwa kiungo wa tano kufunga katika fainali mechi ya Kombe la vilabu bingwa Ulaya pamoja na la Dunia - ni wa kwanza tangu enzi zake Zinedine Zidane.

Pia, ni mchezaji wa pili kujifunga goli la wenyewe na pia kutandika bao la kuondoa kosa mchuano wa Kombe la Dunia.

Kabla ya Kombe la Dunia kung'oa nanga, shindano lenyewe lilikabiliwa na wimbi la wasiwasi kuhusu uandaaji wa Kombe hilo Urusi hususan kuhusu ubaguzi wa rangi, fujo za mashabiki, na uwezekano wa wapenzi wa jinsia moja kuvamiwa.

Lakini mambo yaliishia kwenda nywee…hadi pale, wanaharakati wa Urusi wa kundi la 'Pussy Riot' walipoingia uwanjani mechi ya fainali.

Kundi hilo lililotangaza kuhusika kwake baadaye, lilieleza kuwa lilikuwa likiandamana kutokana na masuala ya kisiasa katika taifa hilo.

Lakini walinzi wa usalama walimakinika mapema na kuwatoa uwanjani - ingawa baadhi yao walijikuta wakikabiliana na wachezaji.