Obama aikumbuka safari yake ya kwanza nchini Kenya

Obama, Auma Obama (kushoto) Sarah Obama (kulia)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Obama, Auma Obama (kushoto) Sarah Obama (kulia)

Rais wa zamani wa Marekani Barack amewataka viongozi nchini Kenya kuhakikisha uwepo wa fursa sawa kama moja ya njia ya kupambana na umaskini.

Akizungumza akiwa kwa marehemu baba yake huko K'Ogelo, magharibi mwa Kenya, Obama amesema kuwa amefurahishwa na hatua za kisiasa zilizopigwa hasa baada ya mapatano yaliyoafikiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga,

Obama alisema licha ya Kenya kujipata njia panda kila baada ya uchaguzi mkuu, hali ni tofuati kwa sasa kwani kuna Rais na kiongozi wa upinzani waliokumbatiana na kuaihdi kuboresha ushirikiano kwa minajili ya taifa.

Aliongeza kuwa kile kinachostahili kufanywa kwa sasa ni kuangamiza umaskini na kila jamii kuitambua nyingine kama mshirika muhimu badala ya adui.

Obama pia aliongoza ufunguzi wa kituo cha vijana cha elimu kwa jina Sauti Kuu, ambacho kilianzishwa na dada yake Auma Obama, kilichofufua kumbukumbu ya safari yake ya kwanza kabisa nyumbani mwa baba yake akiwa miaka 27.

Alisimulia "baada ya kutua Nairobi nilipanda treni ya kasi ya chini sana kisha nikaliabiri basi lililokuwa limebeba kuku na viazi vitamu kando yangu," aliongeza kuwa alipanda gari la uchukuzi la umma lililokuwa limejaa watu kuliko basi kwenda nyumbani mwa Mama Sarah Obama.

Amekariri jinsi alivyooga nje na alivyomshika kuku kuwa kitoweo cha jioni alipohisi njaa wakati akiwa ameenda kuzuru kaburi la baba yake.

Maelezo ya picha,

Obama wakati wa ufunguzi wa kituo cha Sauti Kuu

Baada ya kuwasili nchini Kenya siku ya Jumapili Obama alikutana na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga.

Baba yake Obama Barack senior, ambaye Obama mwenyewe anakiri kutomfahamu kabisa, alikuwa mwana uchumi ambaye alifanya kazi katika serikali ya aliyekwa Rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta na baba ya rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

Barack senior aliachana na mama yake Obama wakati Obama akiwa na umri wa miaka miwili tu na akafariki kwenye ajali ya barabarani mjini Nairobi mwaka 1982 akiwa na miaka 46.

Maelezo ya picha,

Mchoro wa familia ya Obama