Trump shutumani kwa kuitetea Urusi kuhusu tuhuma za udukuzi

Rais Trump na Putin mjini Helsinki, Finland

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Trump na Putin mjini Helsinki, Finland

Rais wa Marekani Donald Trump ameitetea Urusi na tuhuma kwamba ziliingilia uchaguzi wa Rais nchini mwake mwaka 2016.

Baada ya mazungumzo yao, ya ana kwa ana na Rais wa Urusi Vladmir Putin, Rais Trump ameyapinga mashirika ya ujasusi ya Marekani na kusema hakukua na sababu yoyote ya Urusi kuingilia uchaguzi huo.

Kwa upande wake Rais Putin amesisitiza kwamba kamwe nchi yake haijawahi kuingilia mahusiano na Marekani.

Aidha kuhusiana na mkutano wa Helsinki, Kwa upande wake Rais Putin ameuelezea mkutano huo kama uliokuwa wazi bila ya kupangwa na wenye manufaa.

Mazungumzo hayo ya faragha ya viongozi hao, yalichukua karibu saa mbili katika mji mkuu wa Finland Helsinki hapo jana.

Katika mkutano na Waandishi wa Habari, baada ya mkutano huo, Rais Trump aliulizwa kama anayaamini mashirika yake ya ujasusi ama Rais wa Urusi, zinapokuja tuhuma za udukuzi katika uchaguzi.

Alijibu kwa kusema kuwa haoni sababu yoyote kwanini Urusi iweze kufanya hivyo.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Rais Trump na mkewe pamoja na Rais wa Urusi

Aidha amefahamisha kuwa uhusiano wa Urusi na Marekani haujawahi kuwa mbaya kama vile alivyoukuta, lakini kwa sasa hali hiyo imebadilika.

Mashirika ya upelelezi ya Marekani yalihitimisha mwaka 2016 kwamba Urusi ilihusika na kushindwqa kwa mgombea wa Upinzani Hillary Clinton katika uchaguzi huo, kutokana na uhalifu wa mitandaoni na taarifa za uongo zilizopandikizwa katika mitandao ya kijamii.

Baadhi ya viongozi nchini Marekani, wamekuwa wakimpinga Rais Trump, katika taarifa yake aliyoitoa Spika wa Bunge la nchi hiyo Paul Ryan amesema Rais Trump lazima atambue kwamba Urusi sio washirika wao. Huku akisisitiza kuwa hakuna swali, Moscow iliingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.