Rais Magufuli asema chama tawala cha CCM 'kitaongoza milele Tanzania'

Rais Magufuli Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Magufuli asema chama tawala cha CCM kitaongoza maisha Tanzania

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa chama tawala cha CCM kitakuwa madarakani maisha kulingana na ripoti ilioandaliwa na chombo cha habari cha AFP.

Matamshi ya bwana Magufuli yaliotangazwa katika radio Jumatatu jioni yanajiri siku chache baada ya kusema kwamba wafungwa wanafaa kufanya kazi kwa muda mrefu na wapigwe iwapo ni wazembe.

"CCM ni chama tawala na kitaendelea kutawala milele na milele, wanaohangaika watapata tabu siku zote. Chama hiki kipo na kitaendelea kuwepo na kitaendelea kuleta maendeleo kwa ajili ya Watanzania. Hakuna mbadala ni CCM hadi milele," amesema. "Wanachama wa CCM tembeeni kifua mbele tumeamua kuleta Tanzania mpya inayowapigania wananchi hasa wanyonge ili waweze kushiriki katika maendeleo."

Haki miliki ya picha ccm
Image caption Mkutano wa chama tawala cha CCM

Makundi ya wanaharakati wa haki za kibinaadamu yamemshutumu kwa kutowavumilia wengine na Magufiuli amepoteza umaarufu wake mkubwa kwa kuwakandamiza wanahabari na kuwalenga wanasiasa wa upinzani.

Bwana Magufuli sio kiongozi wa kwanza kutoa utabiri kama huo. Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma alisema 2008 kwamba chama tawala cha ANC kitakuwa madarakani hadi 'Yesu atakaporudi' na mwaka 2014 , alisema kuwa chama hicho kitaongoza maisha.

Nini siri ya nguvu ya CCM?

Haki miliki ya picha Ikulu/Tanzania

Siri ya kwanza ya nguvu ya CCM ni Nyerere, Rais wa kwanza ambaye Watanzania wanamkumbuka kwa mapenzi makubwa wakimuita 'Mwalimu, au 'Baba wa Taifa.' Anaweza kuwa hakufanikiwa sana katika nyanja ya uchumi, lakini Nyerere alijenga taifa na kuwaunganisha Watanzania.

Pia, Nyerere alijijengea heshima kwa kung'atuka mwenyewe madarakani akiwa bado ana nguvu na kusimamia mchakato wa kumpata mrithi wake, kinyume na wengine waliosubiri watolewe.

Nchi chache zina watu wa hadhi ya Nyerere na Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini.

Hakuna kati ya Jomo Kenyatta wa Kenya, Dkt Hastings Kamuzu Banda wa Malawi wala Kenneth Kaunda, aliyewahi hata kupokonywa uraia wa Zambia, anayeheshimiwa katika nchi zao kama anavyoheshimiwa Nyerere.

Kutokana na mapenzi ya Watanzania kwa Nyerere na CCM yake, haikushangaza kwamba, mwaka 1991, matokeo ya Tume ya Rais iliyopewa jukumu la kukusanya maoni ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama yalionesha kuwa asilimia 80 ya Watanzania walitaka chama kimoja kiendelee.

Bahati nzuri, mwenyewe aliunga mkono mfumo wa vyama vingi na sauti yake ikawa kura ya turufu. Hata hivyo, wananchi wengi hadi sasa wanaiona CCM kama urithi wa Mwalimu hivyo kuasi chama hicho ni usaliti wa kumbukumbu yake.

Hii inaonesha kuwa vyama vingi si mtindo wa maisha ya kisiasa uliochaguliwa na Watanzania, bali ulianzishwa kwa sababu ilikuwa 'fasheni' ya wakati ule katika siasa mpya za dunia baada ya kudondoka kambi ya Mashariki ya Wajamaa.

Katika hali hii, uzoefu wa miaka 25 wa siasa za vyama vingi unaonesha kuwa Watanzania wanavitumia vyama vya upinzani kama mahali pa kuonesha hasira zao pale serikali ya CCM inaposhindwa kukidhi matarajio yao katika kusimamia uchumi na kupambana na ufisadi.

Kwa lugha za mtaani, CCM ni mke, upinzani ni kimada.

Wimbi la hivi karibuni la viongozi wa upinzani kuhamia au kurudi CCM na kudai kuwa hakuna haja ya upinzani kwa sababu ya mafanikio ya Rais Magufuli inathibitisha nadharia hii.

Demokrasia ndani ya chama

Haki miliki ya picha AFP/getty

CCM ukilinganisha na kizazi cha vyama vyenzake vya ukombozi vilivyotimuliwa madarakani imekuwa ina demokrasia pana ya ndani ya chama na mifumo madhubuti ya kutatua migogoro na hivyo kukiwezesha kuhimili misukosuko.

Baada ya Nyerere kung'atuka, kumekuwa na kupokezana madaraka kwa marais watano mpaka sasa.

Kadhalika CCM imeweza kuvuka salama nyakati ngumu ikiwemo madai ya Serikali ya Tanganyika yaliyoibuliwa na wabunge 55 mwaka 1993 na shinikizo la wajumbe wa vikao vya halmashauri kuu na mkutano mkuu uchaguzi mkuu uliopita (2015) waliotaka Edward Lowassa awe mgombea urais wa chama hicho.

Ukiangalia vyama vya ukombozi katika nchi nyingine, vingi viliponzwa na ukosefu wa demokrasia na uwezo mdogo wa kushughulikia migogoro ya ndani.

KANU iliponzwa na Rais Daniel arap Moi aliyejaribu kuwachagulia Wakenya mrithi.

Naye, Dkt Banda wa Malawi alishajikabidhi uenyekiti wa chama na urais wa maisha wa nchi yake.

Wawili hawa walipalilia uasi ndani ya vyama vyao.

Huenda kiongozi mpya wa ANC, atakayemrithi Jacob Zuma atahitaji somo kutoka CCM kuepusha chama chake na zahma iliyovikumba vyama hivi.

ANC, kama CCM inajivunia muasisi, Nelson Mandela na uimara wa kitaasisi, lakini inahitaji Magufuli wake wa kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya Afrika ya Kusini.

Mustakabali wa CCM mpya

Hata hivyo, kwa upande mwingine, hadhi ya CCM inarejea kwa gharama kubwa kwa demokrasia changa ya Tanzania. Katika siku za hivi karibuni madiwani na wabunge wa upinzani wamekuwa wakihama vyama vyao kwa madai kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri.

Hata hivyo, wapinzani wanadai rushwa imekuwa ikitumika kuwashawishi wahamie CCM.

Kama hiyo haitoshi, Rais Magufuli amekuja na maagizo mapya juu ya namna ya kufanya siasa.

Hakutakuwa tena na mikutano ya siasa ya hadhara mpaka wakati wa uchaguzi isipokuwa kwa wabunge na madiwani katika maeneo yao.

Wakati huohuo, Rais Magufuli mwenyewe anafanya mikutano kama kawaida akichanganya shughuli za chama na serikali.

Kadhalika, viongozi wa upinzani wamejikuta matatani wakikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi pale wanapotoa matamshi mbalimbali, huku wengine wakihofia usalama wao baada ya kupokea vitisho.

Kwa ujumla tutegemee CCM mpya ya Magufuli kuimarika zaidi, lakini pia tutegemee kudorora kwa upinzani.

Si ajabu kwamba, baada ya miaka mitano ya Rais Magufuli, vyama vyaupinzani vitarejea katika hali yao ya miaka ya 1990 wakati wakipigania haki za msingi za kidemokrasia, badala ya kuzungumzia miradi ya maendeleo, mbadala wa ile ya CCM.

Bw Njonjo Mfaume ni mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Baada ya kupitia kipindi kigumu cha kushuka umaarufu wake hususan katika awamu ya pili ya uongozi wa Rais Kikwete, CCM inaelekea kurejesha hadhi yake, ikisaidiwa na faida ya mifumo imara wa uendeshaji wa chama, demokrasia ya ndani na historia iliyotukuka inayofungamanishwa na umaarufu wa muasisi wake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii