Eritrea: Mambo matano ambayo raia wanataka yatekelezwe kwa dharura

Bwana Afwerki aliwasili nchini Ethiopia siku ya Jumamosi -ikiwa ziara yake ya kwanza nchini humo baada ya miongo miwili
Maelezo ya picha,

Bwana Afwerki aliwasili nchini Ethiopia siku ya Jumamosi -ikiwa ziara yake ya kwanza nchini humo baada ya miongo miwili

Nchi ya Eritrea imekuwa katika hali ya tahahadhari kwa kipindi cha takriban miongo miwili tangu wakati wa vita vya mpakani

Lakini sasa inaonekana kama mambo yanaweza kubadilika.

Tarehe 8 mwezi Julai mwaka 2018 Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alifanya ziara muhimu sana mjini Asmara

Makubaliano yalitiwa saini kati ya nchi hizi mbili jirani kurejesha ushirikiano wa kidiplomasia na uchumi.

Tarehe 14 mwezi Julai, Rais wa Eritrea naye alitembelea waziri mkuu wa Ethiopia mjini Addis Ababa

Baada ya maendeleo haya chanya ya kisiasa, raia wa Eritrea wanatamani kama mabadiliko kati ya nchi mbili hasimu yangeletwa pia kusawazisha mambo ndani ya Eitrea yenyewe.

Haya ni mambo matano muhimu ambayo wanaharakati wanadai mabadiliko.

Maelezo ya picha,

Ramani ya nchi jirani

1. Katiba

Muda mfupi baada ya uhuru, Eritrea iliunda tume ya katiba mwaka 1994 kwa ajili ya kushughulikia uundaji wa katiba

Hatimaye katiba iliidhinishwa mwezi Mei mwaka 1997 na Baraza la kitaifa.Mwaka 1998 vita ya mpakani iliibuka na mchakato uliahirishwa na haukuwahi kurejeshwa tena.

Baada ya makubaliano ya kuleta amani yaliyotiwa saini mjini Algiers mwaka 2000, baadhi ya mawaziri wa serikali,majenerali wa jeshi na maafisa walitaka kuundwa kwa katiba.Hata hivyo, serikali ilipuuza madai yao na miongoni mwao watu 11 walikamatwa na mpaka sasa hawajulikani walipo.

Nchi hiyo bado haina katiba.Kiutendaji, ina maana kuwa hakuna taratibu ya chombo cha dola kinachoangalia utendaji wa rais wake, Isaias Afwerki -ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 25.

Hakuna uchaguzi wala ukomo wa rais kuwa madarani.

Mchakato wa kupatikana katiba unaitwa 'Quwam' unabaki kuwa kipaumbele kwa watu,ambao wanaendelea kutaka mabadiliko nchini humo.

Kutungwa kwa katiba, raia wa Eritrea wangependa kuona kunakuwa na katiba ya kidemokrasia ambapo mfumo wa vyama vingi unaanzishwa na kuhakikishiwa kunakuwepo na uchaguzi ulio huru

2. Vyombo vya habari vilivyo huru

Mwezi Septemba mwaka 2001 serikali ya Eritrea zilifunga magazeti yote ya wamiliki binafsi ili kuzima mjadala kuhusu mabadiliko ya kidemokrasia na masuala ya katiba. Kwa mujibu wa kamati ya kulinda waandishi wa habari, takriban waandishi wa habari 10 walikamatwa katika hatua ya kudhibiti vyombo vya habari.

Setit, Zemen, Kesete-Debena, Tsigenay, Meqaleh na Admas ni miongoni mwa magazeti yaliyofungiwa.

Hivi sasa vyombo vya habari vinavyofanya kazi nchini Eritrea ni vile vinavyoendeshwa na serikali,TV- Ere; Radio Dimtshi Hafash na magazeti manne yanayochapishwa kwa lugha ya Tingrinya, kiarabu, kiingereza na Tigre.

Kwa mujibu wa ripoti kadhaa za watetetezi wa haki za binaadamu, Eritrea ni moja kati ya nchi za Afrika ambazo zina uhuru mdogo wa vyombo vya habari.Wengi wanaita Korea Kaskazini ya Afrika. Wengi wana matuamaini kuwa hali hii itaisha.

Maelezo ya picha,

Mamia ya wakimbizi wa Eritrea wanaoishi nchini Ethiopia, waliandamana katika mji mkuu Addis Ababa, kuunga mkono ripoti ya hivi majuzi ya umoja wa mataiafa kuhusu haki za binadamu

3. Uhuru wa kuabudu

Serikali ya Eritrea inatambua dini nne tu.jamii ya dini ambayo haijasajiliwa nje ya Orthodox, uislamu wa sunni,kanisa katoliki na Lutheran yanahesabiwa kuwa batili na viongozi wa dini hizo wanaweza kushtakiwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na tume ya Marekani kuhusu uhuru wa kuabudu, maelfu ya raia wa Eritrea wanashikiliwa kutokana imani yao.

Kesi dhidi ya madhehebu ya mashahidi wa Yehova ilianza muda mfupi baada ya uhuru walipokataa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya uhuru.

Walikataliwa kupata uraia, vitambulisho na leseni za biashara.

Raia wa Eritrea wana matumaini kuon raia wanapata uhuru wa kuabudu.

4. Ulazima kwa raia wa Eritrea kujiunga na Jeshi la kujenga taifa

Mwanzoni, ilikuwa lazima kwa raia kujiunga na jeshi kwa kipindi cha miezi 18-ikiwemo miezi sita ya mafunzo ya jeshi,hata hivyo, masharti yake yalikuwa hayana mipaka tangu mwaka 2002.

Vijana wa Eritrea walijiunga na jeshi la taifa walipomaliza darasa la 11,kisha huenda kambi ya sawa kwa ajili ya kuendelea na darasa la 12 na kupatikwa mafunzo ya kijeshi wakati huo huo walipokuwa wakisoma.

Hakuna makubaliano kuhusu muda wa kumaliza,kwa wengi mafunzo yaliendelea kwa miaka kadhaa.

Mafunzo yalifanyika chini ya sheria na taartibu za jeshi.

Jeshi la taifa lilikuwa jambo la kujivunia, lakini sasa limekuwa sababu ya vijana wengi kulazimika kuondoka nchini humo.

5. Kuachiwa huru kwa wafungwa wa kisiasa na upatanishi

Wanaharakati raia wa Eritrea walio Ulaya na Amerika Kaskazini wanasema kuibadili Eritrea wanapaswa kuanza na kuwaachia wafungwa wa kisiasa,kuliko kitu chochote. Hatua hiyo itafungua njia kuelekea maridhiano .

Mengi yamezungumzwa kuhusu kukamatwa kwa kundi maarufu la G-15, kundi linalofahamika kuwa la wafungwa wa kisiasa, lakini maelfu zaidi wanashikiliwa na serikali bila kufunguliwa mashtaka.

Hali ya jela zinaripotiwa kuwa mbaya zaidi duniani.Kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa ni njia muhimu kuelekea mabadiliko ya kisiasa nchini Eritrea.