Mhadhara wa Mandela: Barack Obama aonya dhidi ya viongozi wababe, azungumzia timu ya Ufaransa

Barack Obama ndiye rais wa pili wa zamani wa Marekani kutoa mhadhara huo, baada ya Bill Clinton
Maelezo ya picha,

Barack Obama ndiye rais wa pili wa zamani wa Marekani kutoa mhadhara huo, baada ya Bill Clinton

Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama amesema ulimwengu umo kwenye njia panda na kwamba kuna mitazamo miwili tofauti kuhusu ubinadamu.

Amesema hayo akihutubu katika mhadhara wa kila mwaka wa Nelson Mandela nchini Afrika Kusini ambao huandaliwa kila mwaka kama sehemu ya maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini.

Bw Obama amesema enzi hizi ni za watawala walio na ubabe na kwamba demokrasia haitiliwi uzito sana.

Huku akionekana kumkosoa mrithi wake Donald trump, Bw Obama amesema watawala wenye nguvu wanahujumu karibu kila taasisi ya serikali ambayo huleta maana kwa demokrasia.

Bw Mandela alizaliwa 18 Julai mwaka 1918 na mwaka huu ni karne moja tangu kuzaliwa kwake.

Obama amesema kiongozi huyo aliyepambana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini alikuwa mtu shujaa kweli na anayefaa kukumbukwa katika historia.

Ametoa wito kwa watu kujifunza mengi zaidi kutoka kwa uongozi wake na kujenga jamii ya kuvumiliana ambapo demokrasia na tofauti baina ya jamii tofauti vinathaminiwa na kusema kwamba vijana wanafaa kutekeleza mchango muhimu katika kuangusha watawala wa kiimla.

Bw Obama amesema kuna kizazi kizima cha watu ambao wamekulia na kulelewa katika ulimwengu uliojaa uhuru zaidi na wa kuvumiliana.

"Hili linafaa kutupatia matumaini," ameongeza.

"Lakini ulimwengu unakabiliwa na tishio la kurejea katika mtindo wa zamani na hatari zaidi na katili wa kufanya mambo.

"Ni lazima tuanze kwa kukubali kwamba sheria zote ambazo huenda zilikuwepo kwenye vitabu …. Miundo ya zamani ya hadhi na mamlaka na unyanyasaji vyote viliangamizwa, lakini havikuangamizwa kabisa," amesema.

Uongozi wa kiimla

Bw Obama amesema kwamba Marekani changamoto dhidi ya utandawazi mwanzoni zilitoka kwa wanasiasa wa mrengo wa kushoto na kisha zikaanza kutokea kwa wanasiasa wa mrengo wa kulia.

Amesema madhara ya kudorora kwa uchumi wa dunia mwaka 2008 - na kutomakinika kwa wasomi na watawala - vilizifanya ahadi zilizotolewa kwa watu kuwa hewa tu.

"Siasa za kuwatia watu hofu na kutoridhika na kuwa na misimamo mikali zilianza kuwavutia watu. Na siasa za aina hiyo sasa zinashika kasi," Bw Obama amesema.

Maelezo ya picha,

Inakadiriwa watu 15,000 wamehudhuria mhadhara hu

Ameongeza kwamba hawatii watu wasiwasi lakini anaeleza ukweli uliopo.

Amesema katika enzi za viongozi wa kisiasa wenye mamlaka makuu, demokrasia huwa ni kivuli tu.

"Viongozi wenye nguvu kuu kisiasa wameanza kuchipuka...wale walio mamlakani hujaribu kuhujumu kila taasisi au utamaduni unaoipatia demokrasia maana," ameongeza.

Bw Obama pia amesema watu wanafaa kuondoka kwa mtazamo wa kusaidiwa tu na badala yake walio na mali na mamlaka wafikirie kuwekeza zaidi katika jamii zilizotengwa.

"Ni lazima tuwekeze katika maeneo hayo ya dunia yasiyobahatika. Kuna vipaji kila pahali," ameongeza.

Ubaguzi

Bw Obama amesema hushangaa sana kwamba wakati huu ni lazima kwake kuwakumbusha watu kuhusu kuwaheshimu watu wa rangi, asili, dini na wapenzi wa jinsia moja.

Amesema anashangazwa na hilo kwamba linafanyika miaka mingi baada ya Nelson Mandela kuondoka gerezani.

"Inaonekana ni kama tunaelekea kwa siasa za kukaripiana, mapambano ya kuhakikisha haki za msingi bado hayakamilika kwa kweli. Ni lazima tuwe macho dhidi ya watu wanaojaribu kujitukuza kwa kuwashusha hadhi wengine," amesema.

Bw Mandela aliachiwa kutoka gerezani mwaka 1990 na kuwa raia wa kwanza mweusi Afrika Kusini mwaka 1994.

Itazame timu ya Ufaransa

Barack Obama amesema usawa katika jamii huwezesha vipaji vya kila mmoja kuifaa jamii.

"Itazame timu ya taifa ya kandanda ya Ufaransa," amesema. "Si wote walionekana kama wa asili ya zamani ya Ufaransa, lakini wote ni Wafaransa - ni Wafaransa."

Ufaransa walishinda Kombe la Dunia Jumapili kwa mara ya pili katika miaka 20, wakiwa na kikosi ambacho wengi wa wachezaji ni wahamiaji au wazazi wao walikuwa wahamiaji.