Trump ajichanganya na kauli yake kuhusu Urusi

Rais Donald Trump wa Marekani na Vladmir Putin wa Urusi
Maelezo ya picha,

Rais Donald Trump wa Marekani na Vladmir Putin wa Urusi

Rais wa Marekani Donald Trump amesema anakubaliana na hitimisho lililotolewa na Taasisi za Ujasusi za nchi yake kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi mkuu wa nchi hiyo wa mwaka 2016.

Akikanusha kauli yake aliyoitoa siku moja iliyopita baada ya mkutano wake na Rais Vladmir Putin wa Urusi.

Amesema alieleweka vibaya siku ya Jumatatu na kwamba alikuwa akimaanisha kwamba hakuona sababu kwanini isiwe Urusi ambayo ilifanya udukuzi katika uchaguzi huo.

Ni Rais Trump akiitolea ufafanuzi na kuikanusha kauli yake ya awali, ambayo imezua sintofahamu na kukosolewa vikali. Hata kwa baadhi ya washirika wake wakitaka ufafanuzi zaidi na kusafisha kauli hiyo.

Amedai kuwa katika mkutano huo wa Helsinki alimaanisha kusema kwamba hakuna sababu ya kufikiria kuwa Moscow haiwezi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.

Amesema ana imani na kuunga mkono taasisi za usalama za nchi yake.

Maelezo ya picha,

Rais Donald Trump

''..Naanza kusema kwamba nina imani na kuunga mkono mashirika ya kijasusi ya Marekani na siku zote ni hivyo. Acha niweke wazi kabisa kwa kusema kuwa na nimekuwa nikisema hivyo mara kadhaa, nakubaliana na hitimisho lililotolewa wapelelezi wetu kwamba Urusi ilifanya udukuzi katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2016..'' Ameongezea Trump

Lakini hata hivyo baadhi ya wapinzani wake, wamesema hawana imani na utetezi huo alioutoa Rais Trump, Huku baadhi yao wakiionya Urusi kwamba kilichotokea mwaka 2016, kisitokee tena.

Maelezo ya picha,

Rais Vladmir Putin wa Urusi

Hata hivyo Kwa upande wake Mark Warner, Seneta kutoka chama cha upinzani nchini Marekani cha Democratic ameweka wazi kwamba hana imani na kauli za kiongozi huyo.

''...Sikubaliani na kauli alizotoa Rais leo. Kama angetaka kutoa kauli hizo, angepaswa kuwa na uwezo wa kufanya hivyo mbele ya Vladmir Putin. Huyu ni Rais ambaye alionesha udhaifu mbele ya kiongozi wa Urusi, alionesha udhaifu mbele ya dunia nzima...'' Alisema Seneta Warner