Kenya kuanzisha usafiri wa magari ya nyaya angani

  • John Nene
  • BBC News Swahili
Magari kama haya ya nyaya angani yanatarajiwa kurahisisha usafiri na pia kuwa njia moja ya kuwavutia watalii Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Magari kama haya ya nyaya angani yanatarajiwa kurahisisha usafiri na pia kuwa njia moja ya kuwavutia watalii Kenya

Serikali ya Kenya ina mpango wa kuanzisha usafiri wa magari ya nyaya angani mwakani. Hayo ni kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma za kivuko cha feri nchini Kenya - Bakari Gowa.

Gowa ameeleza kwamba tayari magari hayo yataanza kutengenezwa mwezi ujao huko Ujerumani.

``Itachukua kama mwaka mmoja hivi magari hayo kutengenezwa kisha yataletwa Kenya mwaka ujao yaanze kazi ya kubeba watu angani kuwavukisha katika kivuko cha Likoni,'' anasema Gowa.

Je, magari haya ya nyaya yatasafirisha watu vipi?

Magari haya yatakuwa juu ya hewa yakitumia umeme. Nyaya hutumiwa kuyavuta au kuyashusha kwa utulivu.

'Cable cars' - kama yanavyofahamika hayatumii injini na badala yake huvutwa kwa nyaya inayozungushwa kwa mota.

Kivuko cha Likoni
Maelezo ya picha,

Kivuko cha Likoni pwani ya Kenya

Magari hayo yanatarajiwa kuchukua takriban dakika tatu kuvukisha watu kwa kasi.

Tutakua na kituo kikubwa hapa karibu na afisi zetu Likoni na kituo kingine upande huo wa Mombasa mjini, ameeleza Gowa.

``Yatakua yanabeba watu thelathini na moja kwa kila safari, magari yote ni ishirini na nane. Kwa kila saa yatabeba watu elfu moja mia tano na kwa siku watu laki moja elfu mia nane.''

Kwa kawaida wasafiri wa kivuko cha feri katika eneo la Likoni pwani ya Kenya hawatoziw fedha, lakini Gowa anasema safari ya gari la nyaya haitakua bure.

``Tutawalipisha ada ya chini kabisa ya shillingi ishirini za Kenya, na endapo mtu ana mzigo atalipa zaidi lakini haitapita shillingi hamsini za Kenya.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma za kivukio cha feri nchini Kenya - Bakari Gowa.
Maelezo ya picha,

Mkurugenzi wa Kenya Ferry Services - Bakari Gowa.

Mizigo isiozidi kilo hamsini itakubaliwa katika magari hayo. Kupanda juu watatumia lifti kwa hivyo ni raha pia kutumia usafiri huo.''

Mpango huo unanuiwa pia kuwa njia moja ya kuwavutia watalii na Wakenya kwa jumla.

``Wasafiri wakiwa juu ya gari hilo la nyaya wataona kwa uzuri kabisa kisiwa cha Mombasa. Kuanzia chini hadi juu ni mita themanini. Watalii bila shaka watavutiwa na gari hilo.''

Usalama nao ukoje maanake miongoni mwa Wakenya watakua na hofu kusafiri kwa gari hilo la nyaya angani, wengine wakijiuliza nyaya hizo zikikatika itakuaje.

Magari hayo hutumika sana ng'ambo hasa bara Ulaya na Marekani.

Magari kama haya ya nyaya angani yanatarajiwa kurahisisha usafiri na pia kuwa njia moja ya kuwavutia watalii Kenya

Chanzo cha picha, Reuters

Gowa anawahakikishia wasafiri wasiwe na hofu kwa sababu watatilia maanani kabisa suala la usalama.

``Tutaangazia usalama wa wasafiri kwa kubadilisha nyaya mara kwa mara na kuweka nyingine mpya kama kuna tatizo.

Magari haya ni salama na ndio kwa maana tunatumia kampuni hiyo ya Ujerumani ambayo ni maarufu sana duniani. Binafsi sijasikia ajali yoyote inayohusu magari haya ya nyaya duniani.''

Kulingana na Gowa, Kenya litakua taifa la pili barani Afrika kutumia usafiri wa magari ya nyaya baada ya Afrika Kusini.

``Magari haya huko Afrika Kusini hutumiwa sana na watalii lakini sisi tutayatumia kusafirisha watu na kwa utalii pia. Hatimaye tutapanua usafiri huo hadi uwanja wa ndege mjini Mombasa na katika mji wa Malindi ikiwezena''.