Ruth Wanjiku Kamande: Malkia wa urembo gerezani ahukumiwa kifo Kenya kwa kumuua mpenzi wake

Ruth Kamande (kati) alitawazwa malkia wa urembo Lang'ata mwaka 2016
Maelezo ya picha,

Ruth Kamande (kati) alitawazwa malkia wa urembo Lang'ata mwaka 2016

Malkia wa urembo katika gereza kuu la wanawake la Lang'ata jijini Nairobi amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na kosa la kumuua mpenzi wake.

Ruth Wanjiku Kamande alipatikana na kosa la kumuua mpenzi wake Farid Mohammed katika mtaa wa Buruburu, Nairobi mnamo tarehe 20 Septemba, 2015.

Jaji Jessie Lessit amesema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo ya mauaji bila shaka yoyote.

Jaji huyo amesema hukumu hiyo inafaa kuwa funzo kwa vijana ambao wanafaa wafahamu kwamba "si vyema kumuua mpenzi wako, ni vyema kujiondokea ukaenda zako."

Wakati wa kukamatwa kwake, mwanamke huyo mwenye miaka 25 sasa alikuwa ndio tu amejiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kusomea Uanabiashara, kwa mujibu wa wakili wake.

Upande wa mashtaka ulikuwa umetoa wito kwa jaji kumhukumu kifo Bi Kamande wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo ukisema hakuonyesha majuto.

"Mwanamume huyo aliyeuawa aliyekuwa na miaka 24 wakati huo alikuwa yatima na alikuwa anategemewa na jamaa wengine, haki inafaa kutendeka," wakili wa mashtaka alisema.

Maelezo ya picha,

Ruth Kamande (wa pili kutoka kushoto)

Mahakama iliamua vitendo vya Kamande vilionyesha aliua kwa kukusudia.

Mwanamke huyo alikuwa amejitetea kortini na kusema mzozo kati yake na marehemu ulizidi baada yake kugundua kadi ya hospitali iliyoashiria kwamba Mohammed alikuwa anapokea matibabu ya Ukimwi.

Alisema alimkaripia kumwuliza ukweli kuhusu hilo na kwa mujibu wake, marehemu alimwambia wakati huo kwamba heri wafe wote kuliko hali yake ya Ukimwi itambulike hadharani.

Bi Kamande anasema mzozo wao ulizidi hata zaidi baada yake kugundua barua za mapenzi kutoka kwa wanawake wengine.

Alisema alimdunga kisu mpenzi wake baada ya kisu cha kutumiwa jikoni kumwangukia wakipigana na hapo akamdunga kisu mara kadha. Anadaiwa kumdunga kisu mpenzi huyo wake mara 22.

Bi Kamande alikuwa ameambia mahakama kwamba marehemu alijaribu pia kumbaka lakini mahakama ilisema uchunguzi wa madaktari ulionyesha hakukuwa na ukweli kuhusu madai hayo.

Mwanamke huyo amekuwa akizuiliwa rumande tangu 2015.

Mawakili wa Bi Kamande walikuwa wameiomba mahakama kumwonea huruma na kutompa adhabu kali.

Maelezo ya sauti,

Mwanamke malkia wa urembo gerezani Kenya

Wakili wake Joyner Okonjo alisema mfungwa huyo alikuwa amejenga "uhusiano wa karibu na Mungu" tangu kuzuiliwa mwaka 2015 na kwamba alikuwa amesilimu na huwa anaomba mara tano kwa siku.

Mahakama iliambiwa kwamba pamoja na hayo ameanza masomo ya dini akiwa gerezani, ishara kwamba amepata funzo akiwa gerezani.

Mahakama iliambiwa kwamba Bi Kamande ni mtoto wake pekee wa mama yake kwa sasa baada ya kaka yake mdogo kufariki.