Wanawake wachimba makaburi nchini Cameroon

Jamii ya wachache ya raia wa Cameroon wanaozungumza kiingereza wamekuwa wakilalamika kutengwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Jamii ya wachache ya raia wa Cameroon wanaozungumza kiingereza wamekuwa wakilalamika kutengwa

Nchini Cameroon ambako mzozo kati ya vikosi vya serikali na jamii inayozungumza lugha ya kiingereza umesababisha wanawake wengi kufanya majukumu ambayo kwa kawaida hufanywa na wanaume-majukumu hayo ni kuchimba makaburi kwa ajili ya kuzika waliopoteza maisha.

Haya yanatokea katika maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo,ambapo wanaume wengi wamekimbia jamii zao , wakiwaacha wanawake na wakinamama wakitafuta miili ya watoto wao na wana jamii wengine kwa ajili ya mazishi.

Taratibu za kimila ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu kuhusu jambo hilo zimevunjwa.Mwandishi wa BBC Joe Sa'ah anaeleza.

Mji wa Belo ulikuwa na jamii ya wafanyabiashara na wakulima.Kulikuwa na furaha, lakini sasa mambo yamebadilika.kumekuwepo na vitendo vya mauaji kila mahali.

Mamia ya familia zilikimbilia porini na kuhamia miji mingine ya mbali.

Vijana walijiingiza kwenye mapigano wakijiita wapigania uhuru wa Ambazonia.Lakini wanajeshi wa serikali walitawanywa katika maeneo hayo na madhara yake yameonekana kuwa mabaya sana.

Kumeripotiwa mauaji ambayo yanaelezwa kutekelezwa na pande zote mbili za mzozo huo.

Video ambayo inaelezwa kuwa pengine ilirekodiwa na wanajeshi ilionyesha wanaume wanne wakiteswa, miili yao baadae ilipatikana, ikiwa imeharibiwa.

Nawain Futun'gha ni mama wa miaka 60 mwenye watoto watano, aliyakimbia makazi yake, mjini Belo na sasa yuko Yaounde.

Aliamua kwenda huko baada ya kumshuhudia mtoto wake akiuawa mbele yake.

Katika mazingira ya namna hii wanawake sasa wanapaswa kuwajibika bila kuangaliaa tamaduni ambazo zimekuwepo.

Katika eneo hili masuala yanayohusu mtu aliyepoteza maisha yanawahusu wanaume.Wanawake hawapaswi kufanya chochote na viongozi wa mila kama vile Yerima Kini Nsom, mwana mfalme wa Kom anasema kuwa hali hii itasababisha mji huo kuwa na mustakabali mbaya zaidi.