Lowassa na Zitto Kabwe wajadili umuhimu wa kuwa na upinzani wenye nguvu kuikabili serikali

Edward Lowassa

Waziri mkuu wa zamani nchini Tanzania Edward Lowassa amekutana na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Bwana Zitto Kabwe mjini Dar es Salaam.

Kulingana na msemaji wa Lowassa Aboubakry Liongo, viongozi hao wa upinzani walikutana katika afisi ya Lowassa kuzungumzia hali ya kisiasa iliopo nchini humo pamoja na jukumu la upinzani katika kusaidia ajenda ya maendeleo ya taifa hilo.

Lowassa alijiunga na upinzani 2015 na kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Chadema.

Kulingana na gazeti la The Citizen, picha ya wawili hao wakiwa katika mkutano huo imesambazwa katika mitandao kadhaa ya kijamii lakini hakuna maelezo zaidi yaliosemwa kuhusu yale yaliojadiliwa.

Lakini alipopigiwa simu Zitto alisema: Udanganyifu unaoendelea katika chaguzi ndogo unatia wasiwasi na ishara ya kile tutakachokutana nacho uchaguzi mkuu wa 2020.

Kama upinzani na washikadau wa demokrasi huu ni wakati wa kuanzisha muungano wa upinzani ili kuzuia hatua zaidi za mmomonyoka wa demokrasia mbali na kuzuia taifa hili kutumbukia katika uongozi wa kiimla.

Chanzo cha picha, Bunge/Tanzania

Chama chetu kiko tayari kujadiliana na vyama vyengine kwa lengo hilo.

ACT-Wazalendo na Chadema wamekuwa wakifanya mikutano ya siri kwa lengo la kuwa na muungano wa upinzani ili kukabiliana na kile walichokitaja kuwa hatua ya serikali kukandamiza upinzani na demokrasia.

Vyama hivyo viwili vimeamua kuunga mkono wagombea wake katika uchaguzi wa eneo bunge la Buyungu mbali na viti 79 vya wadi uliotarajiwa kufanyika Agosti 12.