Wataalamu waonya juu ya HIV

Watafiti wakiwa maabara

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Watafiti wakiwa maabara

Jopo la Wataalamu wa Kimataifa limeonya kwamba maendeleo yanayopatikana katika mapambano dhidi ya HIV na ukimwi yanaweza kushindwa kuendelea kutokana na kile walichokiita hatari ya kubweteka ama kuridhika na kile kilichopo.

Jopo hilo la wataalamu limesema ukweli ni kwamba kumekuwa hakuna ongezeko katika kufadhili ama kutoa fedha kusaidia juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo, hali ambayo inaweza kuliibua tena gonjwa hilo wakati ambapo kizazi kipya cha vijana kikiingia katika rika la kutoka utoto kwenda ujana na ujana kwenda utu uzima.

Wakati maambukizo mapya ya HIV yakipungua, watu kutoka katika makundi yaliyowekwa pembeni ikiwemo wale wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, watumiaji wa dawa za kulevya na wanaofanya biashara za ngono wapo katika hatari kubwa.

Ugonjwa wa ukimwi umekuwa pia ukiongoza pia kuua wanawake wengi vijana, kusini mwa jangwa la Sahara.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Upimaji wa virusi vya ukimwi

Ripoti hiyo mpya imesema pia kwamba watu walioambukizwa ugonjwa huo na kuishi muda mrefu kutokana na kutumia dawa za kuongeza maisha matokeo yake ni kukumbwa na maambukizo ya magonjwa nyemelezi uzeeni kama vile Saratani na magonjwa ya moyo.

Takriban watu milioni 37 duniani kote wanaishi na virusi ama ugonjwa wav ukimwi na inakadiriwa kuwa kuna wagonjwa wapya milioni 1.8 kila mwaka.