Moto Serengeti: Tanzania yakanusha madai ya kuwazuia nyumbu kwenda Maasai Mara nchini Kenya

Serikali ya Tanzania imesema uchomaji moto kwenye hifadhi ni jambo la kawaida
Image caption Serikali ya Tanzania imesema uchomaji moto kwenye hifadhi ni jambo la kawaida

Serikali ya Tanzania imekanusha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa mamlaka za hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania zimefanya hujuma kuchoma moto eneo la hifadhi ili kuzuia nyumbu kuvuka kuelekea nchini Kenya.

Msemaji wa Wizara ya mali asili na utalii, Dorina Makaya amesema madai haya ''si ya kweli'' kinachoendelea ni uchomaji wa kawaida wa awali ambao unaoendelea kwa awamu, linalofanywa lina lengo kuzuia majanga ya moto kutoka nje ya hifadhi ambayo yanaweza kufikia ndani ya hifadhi.

Dorina amesema uchomaji wa moto unaofanyika hufanyika kitaalamu ili kuwezesha kuota kwa majani mapya kwa ajili ya malisho yao, pia kupunguza majani mengi ambayo huwafanya watalii kutoona vizuri wanapofika kutembelea hifadi ya Serengeti.

Pia inasaidia kuua wadudu mbalimbali kama Mbung'o na wadudu wanaoshambulia wanyama.

Msemaji wa wizara hiyo amesema hakuna uthibitisho wa Kisayansi kuwa kuchoma majani kunazuia Nyumbu kushindwa kwenda Masai Mara.

''Safari ya Nyumbu ni utaratibu wao wa asili , sababu pekee inayoweza kusababisha kuchelewa kwa Nyumbu kwenda Kenya inawezekana ni kutokana na mvua upatikanaji wa maji ya kutosha huwafanya kuendelea kubaki palepale kwa sababu wanapata maji ya kutosha''.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Watalii wakiwafuatilia nyumbu katika hifadhi ya taifa ya Maasai Mara

''Kwa kuwa Tanzania imepata mvua kwa kipindi kirefu hivyo inawezekana kabisa kuwa Nyumbu wanaweza kuchelewa kuhamia Kenya msimu huu," alieleza Dorina.

''Zoezi la uchomaji majani kwenye hifadhi ni la kawaida ambalo hufanyika Tanzania lakini pia hata Maasai Mara hufanyika hayo pia''.

Taarifa zilisema kuwa moto huo uliodaiwa kuwa mkubwa ulielezwa kuwa uliwaka kwa takriban juma moja, umezuia mamia ya Nyumbu kutoka Serengeti kuvuka mto na kuingia Kenya.

''Mamia ya ekari katika eneo hilo la hifadhi lililo Kaskazini mwa Tanzania bado yanateketea kwa moto na kuwazuia Nyumbu hao kuvuka'' Ilieleza sehemu ya taarifa .

Askari wa nyama pori na Hifadhi ya taifa ya Tanzania( TANAPA) wamenyooshewa kidole, wakishutumiwa kuwasha moto katika hifadhi ya Serengeti ili wanyama wasifike katika hifadhi ya Masai Mara, inayopakana nayo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii