Kashfa ya simu: Jinsi Wakenya wanavyoibiwa fedha na walaghai katika simu zao

wanaume wanaotumia simu za rununu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kenya ina idadi kubwa ya wateja wanotumia simu zao kutuma fedha ama kupokea.

Simu za rununu nchini Kenya ni sawa kama akaunti za benki- na sasa walaghai wameanza mbinu za kuzidukua

Sammy Wanaina alipokea ujumbe wa simu siku ya Jumapili uliomtaka kutoa neno lake la siri ili simcard yake ibadilishwe.

Alichanganyikiwa , kwa kuwa hakuwa ametuma ombi lolote la kutaka kupewa kadi mpya.

Na muda mfupi awali alikuwa amekata simu ambayo sasa amegundua ilikuwa ya wezi ambao walijifanya washauri wa huduma kutoka kampuni ya simu hiyo.

''Ilikuwa simu fupi na sikutoa maelezo yangu yoyote'', Bwana Wainaina aliambia BBC.

Alipigia kampuni ya huduma za simu Safaricom , ili kuripoti kwamba kulikuwa na mpango wa kumlaghai katika simu yake.

Licha ya kutoa maelezo yoyote na kuwaripoti walaghai hao kwa Safaricom, alipoteza udhibiti wa nambari yake kabla ya kuweza kuidhibiti tena baada ya siku tatu.

Alituma ujumbe wa Twitter kwamba swala hilo lote lilimtia uoga.

Bwana Wainaina anasema kuwa kampuni ya Safaricom iliwasiliana naye baada ya malalamishi yake na kumpatia sim card mpya kama tahadhari-bila ya kumpatia maelezo jinsi alivyopoteza udhibiti wa nambari yake ya simu.

Kampuni hiyo ilituma ujumbe ikisema kuwa inajizatiti kulinda habari za wateja wake na kwamba itafuatilia swala hilo hadi mwisho wake.

'Nilipoteza $18,000'

Habari yake iliwafanya wengine kuzungumzia swala hilo huku kila mtu akitoa kisa chake-wengi wakiwa ni wale walipoteza fedha zao katika kashfa hiyo.

Mwanasiasa Stanley Wanjiku alifichua kwamba alikuwa ametegwa na walaghai hao ambapo alipoteza $18.000 (£14,000).

Aliambia gazeti la The Daily Nation nchini Kenya kwamba tatizo lake lilianza baada ya kupata ujumbe kwamba hawezi kupata akaunti yake ya fedha na kwamba alitakiwa kupiga nambari fulani ili kuibadilisha -ambapo alifanya hivyo.

Baadaye aligundua kwamba nambtri yake ya siri ilikuwa imebadilishwa na kupatiwa nambari nyengine, hivyobasi hakuwezi kupata fedha zake.

Gazeti hilo halikusema ni huduma gani aliyokuwa nayo katika akaunti yake.

''Sijui vile neno langu la siri la simu yangu lilibadilishwa na kupewa wahalif''u.

''Nimepata hasara kubwa'' , alisema bwana Wanjiku, 'akiongezea kuwa akaunti yangu ya benki ambayo haihusiki na simu yake pia ilidukuliwa.

Mengi kuhusu akaunti katika simu za rununu:

Watu humiliki sim card kadhaa kutoka kampuni tofauti-kutokana na huduma tofauti . Hivyobasi kadi hizo za simu uharibika na sio swala la kushangaza kwamba watu hutaka kuzibadilisha.

Kenya ina idadi kubwa ya watumizi wa simu za rununu zenye akuanti za fedha duniani, ikiwa ndio sababu kuu ya kashfa hiyo ya sim card kuzua hisia kali miongoni mwa umma.

Takriban nusu ya idadi ya watu nchini Kenya- watu milioni 47 hutumia huduma ya M-Pesa ili kulipia huduma na kufanya biashara.

Kupitia ushirikiano na kampuni nyengine za simu pia zimefanikiwa kuweka huduma za fedha na benki hatua inayowafanya wateja kutoa fedha katika akaunti zao za benki na pia kurudisha.

William Makatiani , kutoka kwa kampuni ya usalama wa mitandaoni ya Serianu, aliambia gazeti la Daily Nation kwamba kashfa ya kudukua simu za rununu za Wakenya inaendelea kuwa kitu cha kawaida.

Ubadilishaji wa sim card umekuwa tatizo kubwa husuan nchini Nigeria tangu 2016.

''Ulianza nchini Kenya mwaka uliopita'' , alinukuliwa akisema.

Jinsi ya kujilinda dhidi ya walaghai katika simu yako

Haijulikani haswa ni vipi ulaghai huo unafanyika katika simu, lakini wiki hii mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya, shirika linalodhibiti sekta ya simu za rununu nchini humo imewataka watumiaji wa simu kujilinda:

  • Usitoa habari zako za kibinafsi.
  • Usitoe nambari yako ya neno lako la siri
  • Futa ombi la maelezo yako ya kifedha ama neno lako la siri
  • Jitahadharishe na ujumbe unaotiliashaka ama ambao hukutuma ombi.

Safaricom pia imewataka wateja wake kulinda maneno yao ya siri , siku zao za kuzaliwa pamoja na nambari zao za vitambulisho.

Pia ilisema kuwa wateja wao wanafaa kujua nambari rasmi ya huduma za simu ili kuwaepuka walaghai wanaotaka kuingia katika akaunti zao.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii