Hobby: 'Afisa' wa polisi aliyetoweka Tanzania yuko wapi?

Huyu ni mmoja wa mbwa ambaye Marekani iliipa tanzania 2016 Haki miliki ya picha Ubalozi wa Marekani Tanzania

Maafisa wa polisi nchini Tanzania bado wanaendelea kumsaka mbwa mpekuzi ambaye ametoweka kwa siku tatu kufikia sasa.

Mbwa huyo kwa jina 'Hobby' huweza kuwakamata wanaopenyeza bidhaa katika bandari ya Dar es salaam kupitia kunusa na kutambua bunduki, pembe za ndovu na mihadarati.

Waziri wa maswala ya ndani nchini humo Kangi Lugola amewapatia maafisa wa polisi siku moja kumsaka mbwa huyo , lakini wameshindwa kumpata kufikia sasa.

''Kile nilichosiki kuhusu mbwa huyu hakiridhishi. Naambiwa kwamba wengine hukodishwa kwa matumizi mengine. Nimehuzunika sana na ripoti hizi kwa kuwa mbwa hawa ni maafisa wa polisi'', waziri huyo alinukuliwa na Gazeti la The Citizen Tanzania akisema.

Mwaka 2016, serikali ya Marekani iliipatia Tanzania mbwa wanne waliofunzwa kutambua mihadarati, pembe za ndovu katika bandari kuu ya taifa hilo pamoja na uwanja wa ndege.

Haijulikani iwapo Hobby alikuwa mmoja wao.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mbali na mbwa huyo, Lugali amenukuliwa na gazeti la mwananchi akisema mbwa wengine 30 waliokuwa wakiondolewa na kurejeshwa kinyemela pia wanachunguzwa.

Lugola ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Julai 21, 2O18 wakati akitoa taarifa ya ziara aliyoifanya kuanzia Julai 11, 2O18.

"Nimemuagiza Sirro kuchunguza kwa undani na kubaini nini kimetokea kisha kuniletea taarifa. Wafanye uchunguzi kiundani zaidi kubaini nini kimetokea kwenye kikosi hicho na kunipa taarifa," amesema Lugola.

Julai 19, 2018 Lugola alisema anahitaji maelezo kutoka kwa Sirro kuhusu alipo mbwa huyo huku jana akibainisha kuwa hakuwa amepata maelezo yoyote kuhusu alipo mbwa huyo.

Lugola alitoa kauli hiyo alipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuona utendaji kazi wa jeshi la polisi bandarini hapo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii