Afrika Kusini waendelea kuomboleza mauaji ya madereva 11 wa teksi waliouawa kwa kupigwa risasi

Mabasi madogo ya abiria ni maarufu kwa usafiri nchini Afrika Kusini Haki miliki ya picha AFP/GETTY
Image caption Mabasi madogo ya abiria ni maarufu kwa usafiri nchini Afrika Kusini

Afrika Kusini inaendelea kuomboleza vifo vya madereva 11 wa magari madogo maarufu kama taxi waliouawa baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha.

Tukio hilo la aina yake limeacha simanzi kubwa kwa familia na watu karibu wa familia waliopoteza wapendwa wao.

Waathirika, na wengine walikuwa wamejeruhiwa vibaya, walikuwa wametoka kwenye mazishi ya mfanyakazi mwenzao katika mji wa pwani wa Kwa-Zulu Natal, Polisi walieleza.

Chanzo cha shambulio hilo hakijajulikana ingawa kumekuwa na hali ya uhasama miongoni mwa makundi yanayoendesha Mabasi hayo nchini humo.

Mabasi madogo ya abiria ni maarufu sana miongoni mwa raia wa nchi hiyo wanaofikia milioni 55.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Madereva hao waliuawa walipokuwa wametoka kumzika mwenzao

Msemaji wa Polisi Brigedia Jay Naicker amesema basi hilo lilishambuliwa katikati ya mji wa Coleso na Weenen.

''Gari lilishambuliwa, kulikuwa na vifo vya watu 11 na wengine wanne walikuwa wamejeruhiwa vibaya na wamekimbizwa hospitali'',aliwaambia wana habari.

''Kumekuwa na mzozo mara nyingi unaohusisha magari hayo lakini bado tunapeleleza kuwafahamu waliotekeleza mashambulizi''

Tukio hili limekuja siku kadhaa baada ya mashambulizi kufanyika Johannesburg,Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimeripoti.