Tafenoquine: Dawa mpya ya malaria ya aina yake yaidhinishwa Marekani

mosquito Haki miliki ya picha Science Photo Library

Dawa mpya ya kutibu Malaria, ambao ndiyo ya kwanza ya aina yake kuidhinishwa katika kipindi cha miaka 60, imeidhinishwa Marekani.

Dawa hiyo ni ya kutibu aina ya ugonjwa wa malaria unaojirudia mara kwa mara, ambao huathiri watu takriban 8.5 milioni kila mwaka. Viini vya ugonjwa huo huwa na uwezo wa kujificha kwenye ini na kumshambulia mtu mara kwa mara.

Aina hiyo ya ugonjwa ilikuwa hatari sana kuangamiza mwilini kwani ilikuwa na uwezo wa kusalia kwenye ini la mwanadamu kwa miaka mingi bila kusumbua, na kisha kumshambulia mara kwa mara.

Wanasayansi wameeleza tiba hiyo ya tafenoquine kama "mafanikio makubwa".

Mamlaka za kuidhinisha dawa katika mataifa mbalimbali duniani sasa zinatarajiwa kuchunguza iwapo dawa hiyo inaweza kutumiwa kutibu raia katika mataifa hayo.

Ugonjwa usioangamia

Malaria inayojirudia, ugonjwa ambao husababishwa na vimelea aina ya plasmodium vivax, ndiyo aina ya inayopatikana sana katika mataifa mengi nje ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Huwa hatari sana kwa watoto ambao wanaweza kuugua malaria marakadha baada ya kuumwa mara moja tu na mbu. Kuumwa huko mara moja tu kunaweza kuwasababisha kutohudhuria masomo na kudhoofika kila wanapoambukizwa.

Watu walioambukizwa wanaweza kuwa pia kama hifadhi au mwenyeji wa vimelea kwani kila viini hivyo vinapoibuka tena mwilini, mbu akiwauma basi anaweza kueneza viini hivyo kwa mtu mwingine.

Huwezi kusikiliza tena
Wanasayansi Kenya wamegundua dawa inayoangamiza mbu anayesababisha Malaria.

Hilo lilikuwa linaifanya vigumu sana kuangamiza aina hiyo ya ugonjwa duniani.

Lakini Mamlaka ya Dawa na Chakula Marekani (FDA) imetoa idhini ya kuanzakutumika kwa dawa hiyo ya tafenoquine, dawa ambayo inaweza kuangamiza viini hivyo vya malaria kutoka mafichoni hata kwenye ini na kuuzia watu kuugua tena.

Dawa hiyo inafaa kutumiwa pamoja na dawa nyingine ili kumtibu mgonjwa anapougua.

Tayari kuna dawa nyingine ambayo ilikuwa inatumiwa kumaliza viini vya malaria vilivyojificha kwenye ini inayofahamika kama primaquine.

Lakini tofauti na tafenoquine ambayo unainywa mara moja tu, primaquine ilifaa kutumika kwa siku 14.

Wataalamu walikuwa na wasiwasi kwamba watu hupatanafuu baada ya kunywa tembe hizo kwa siku kadha na hivyo basi huacha kuzitumia bila kumaliza kipimo kifaacho na hivyo kuvipa viini hivyo fursa ya kujikwamua na kuweza kuushamblia mwili baadaye.

Tahadhari inahitajika

FDA wanasema dawa hiyo inafanya kwa mafanikio makubwa na wameidhinisha itumike Marekani, lakini wamesema kwamba kuna madhara yake mengine ambayo watu wanafaa kuyafahamu.

Kwa mfano, mtu aliye na tatizo la vimeng'enya (enzyme), tatizo lifahamikalo kama ukosefu wa G6PD, hawafai kuitumia dawa hiyo kwa sababu inaweza kusababisha anaemia, au ukosefu wa damu ya kutosha mwilini.

FDA wamependekeza watu wawe wanapimwa kubaini iwapo wana hali hiyo kabla ya kupewa dawa hiyo, jambo ambalo linaweza kusababisha tatizo kubwa katika maeneo ya watu maskini ambapo malaria huathiri watu sana.

Kuna pia wasiwasi kwamba katika vipimo vya juu, watu wenye matatizo ya kiakili wanaweza kuathiriwa.

Haki miliki ya picha SPL

Lakini licha ya tahadhari hii, kuna matumaini makubwa kwamba kutumiwa kwa dawa hiyo pamoja na vyandarua vya kuzuia mbu na tahadhari nyingine, hivi vyote vinaweza kupunguza visa vya malaria aina ya vivax duniani.

Prof Ric Price, wa Chuo Kikuu cha Oxford ameambia BBC: "Kwamba itawezekana kumaliza viini hivi kutoka kwenye ini kwa dozi moja ya tafenoquine ni mafanikio makubwa sana na kwa maoni yangu ni moja ya mafanikio makubwa zaidi kupigwa katika kutibu malaria katika kipindi cha miaka 60 iliyopita."

Hayo yakijiri, Dkt Hal Barron, raia wa utafiti na maendeleo katika GSK, kampuni inayotengeneza dawa hiyo, amesema: "Kuidhinishwa kwa Krintafel [nembo ya tafenonquine], tiba ya kwanza ya malaria aina ya Plasmodium vivax katika zaidi ya miaka 60, ni haua kubwa sana kwa watu walio na malaria isiyopona.

"Kwa pamoja na washirika wetu, Medicines for Malaria Venture, tunaamini Krintafel itakuwa dawa muhimu sana kwa wagonjwa walio na malaria na kuchangia pakubwa katika juhudi zinazoendelea za kuangamiza ugonjwa huu."

Tafenonquine imekuwepo tangu miaka ya 1970 lakini kwa kushirikiana na Medicines for Malaria, GSK wameifanyia ukarabati dawa hiyo kuiwezesha kuondoa viini vya malaria kwenye ini.

Hatua itakayofuata sasa ni dawa hiyo kuchunguzwa na mashirika mengine ya kuidhinisha matumizi ya dawa katika mataifa mengine ambapo aina hiyo ya malaria hupatikana sana.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii