Tuzo za Beffta: Nani hawa wanaomtambua na kutaka kumpa Mange Kimambi tuzo ya wanawake na siasa Afrika?

  • Peter Mwai
  • BBC Swahili
Mange Kimambi

Chanzo cha picha, @mangekimambi_

Mwanamitindo Mtanzania aliyebadilika kuwa mwanaharakati wa kisiasa Mange Kimambi amekuwa haangaziwi sana mitandaoni tangu kutibuka kwa maandamano ya kupinga utawala wa Rais wa Tanzania John Magufuli yaliyokuwa yamepangiwa kufanyika Aprili.

Lakini kwa siku chache zilizopita, ameanza kuzungumziwa tena hasa mtandaoni, zaidi kutokana na taarifa kwamba ameorodheshwa kushindania tuzo ya wanawake waliowahamasisha watu zaidi katika siasa Afrika.

Taarifa zimetokana na ujumbe kwenye mtandao uliochapishwa na shirika linalojiita BEFFTA.

Beffta ni ufupisho wa Black Entertainment Film Fashion Television and Arts, (Burudani, Filamu, Mitindo, Televisheni na Sanaa ya Watu Weusi). Shirika hilo linasema huwa linaangazia maslahi ya watu weusi Uingereza, Canada, Marekani, Caribbean na barani Afrika.

Katika ujumbe wa shirika hilo Instagram, ambapo wana wafuasi 21,600, limewaorodhesha wanawake sita kushindania tuzo hiyo wanaoiita Tuzo ya Mwanamke Mhamasishaji zaidi Kisiasa Afrika.

Chanzo cha picha, @beffta

Beffta wamewaorodhesha:

Ellen Johnson Sirleaf - Liberia

Ellen Johnson Sirleaf ni mwanasiasa nchini Liberia aliyehudumu kama rais kati ya 2006-2018. Alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa nchi barani Afrika. Aliondoka madarakani mapema mwaka huu na nafasi yake ikachukuliwa na George Weah. Ingawa uongozi wa Sirleaf ulisifiwa kwa kudumisha amani, alikosolewa kwa tuhuma za ufisadi na mapendeleo. Siku chache kabla yake kustaafu baada ya kuongoza kwa miaka 12, alifukuzwa kutoka chama chake. Alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2011 kwa pamoja na mwanaharakati Leymah Gbowee.

Alengot Oromait -Uganda

Proscovia Alengot Oromait ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Uganda ambaye pia ni mwanasiasa. Alihudumu kama mbunge wa eneo la Usuk, katika wilaya ya Katakwi kati ya 2011 na 2016. Alichaguliwa mbunge akiwa na miaka 19 pekee na kuwa mbunge wa umri mdogo zaidi kuwahi kuchaguliwa nchini humo.

Joice Mujuru -Zimbabwe

Joice "Teurai-Ropa" Mujuru ni mwanasiasa nchini Zimbabwe ambaye alihudumu kama makamu wa rais kati ya 2004-2014 baada ya kuhudumu kwa miaka kadha kama waziri. Alikuwa miongoni mwa waliotazamiwa kumrithi Robert Mugabe kabla yake kufutwa. Alihudumu pia kama makamu wa rais wa chama cha Zanu-PF.

Mange Kimambi -Tanzania

Mwanamitindo Mtanzania aliyebadilika kuwa mwanaharakati wa kisiasa Mange Kimambi amekuwa aliyepanga maandamano ya kushutumu utawala wa Rais wa Tanzania John Magufuli yaliyokuwa yamepangiwa kufanyika Aprili 26.

Diane Shima Rwigara -Rwanda

Diane Shima Rwigara ni mwanamke mfanyabiashara nchini Rwanda na mwanaharakati aliyetaka kuwania urais kama mgombea wa kujitegemea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ambao Rais Paul Kagame alitangazwa mshindi. Alikamatwa pamoja na mamake na dadake na kushtakiwa kwa makosa ya udanganyifu na uchochezi tuhuma ambazo wameziita zenye kuchochewa na kisiasa. Wamekuwa kizuizini na kesi dhidi yao ilianza rasmi wiki hii.

Mbali Ntuli -Afrika Kusini

Mbali Ntuli mwenye miaka 30 ni mwanasiasa wa chama cha Democratic Alliance anayehudumu katika bunge la jimbo la KwaZulu-Natal. Alikuwa kiongozi wa vuguvugu la vijana wa Democratic Alliance Youth.

Mange Kimambi amesema nini?

Mwanaharakati huyo mwenyewe aliuchukua ujumbe huo na kuuweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, kwake akionekana kuwahurumia Beffta.

"Nahisi hawa @Beffta_award wamejuta kabisa kuniweka kwenye hiyo category sidhani kama washawahi kupata comments zote hizo 不不不. Watanzania kiboko kabisaaa 不不不... Thanks for the luv nawapenda sana!!!"

Ujumbe huo wake umetolewa maoni zaidi ya 10,000.

Watu wengi kwenye mtandao huo wa Instagram wamekuwa wakitumia kitambulisha mada hicho kumpigia Mange kura.

Mhusika mkuu

Dkt. Pauline Long

Mwanzilishi wa tuzo hizo ni Dkt Pauline Long ambaye anajieleza kama mjasiriamali na mhisani anayewasaidia wasiojiweza.

Katika tovuti ya Women Economic Forum (WEF), usichanganye na World Economic Forum (WEF) ambalo ni Shirika kuhusu Uchumi wa Dunia, anaelezwa kama mjasiriamali, mhisani, mmiliki wa vyomb vya habari, mwandaaji wa filamu na video na mtangazaji maarufu. Ndiye mwanzilishi na mmiliki wa Beffta na pia mmliki wa studio za East End studios, na nembo za Mr. na Miss Afrika Mashariki UK. Ndiye pia rais wa Wakfu wa Ujasiriamali wa Pauline Long, na Wiki ya Wanawake wa Afrika Duniani (GAWW). Kipindi chake cha The Pauline Long Show kinadaiwa kupeperushwa katika Sky Channel 182 -BEN TV.

Katika mahojiano na mtandao wa Mambo wa Uingereza, Bi Long yamkini alihamia Uingereza miaka 20 iliyopita na asili yake huenda ikawa Kenya.

Mwaka 2009, ananukuliwa na mtandao huo akisema alishinda tuzo ya Wakenya Waliofanikiwa Uingereza (UK Kenya Achievers Award).

Katika mahojiano hayo na mwandishi Taku Mukiwa anazungumzia jinsi wakati mmoja alivyokuwa na wazo la kuendeleza biashara Kenya na alikuwa akituma pesa nyumbani lakini usimamizi wa biashara hizo haukumridhisha na mwishowe akaamua kuangazia Uingereza.

Anasema wazo la kuwa na tuzo lilikuwepo akilini mwake kwa muda mrefu na alikuwa amekusudia mwanamuziki Michael jackson awe wa kwanza kwake kumtuza lakini akafariki hata kabla yake kuanzisha tuzo hizo na ndipo alipoamua kuzianzisha mara moja.

Anasema katika familia yao walikuwa watoto 11 na baba yao ni mtu aliyefahamika sana kijijini.

Shabiki wa Arsenal na Gor Mahia

Kwenye mahojiano hayo na tovuti ya Mambo ya Uingereza, anasema yeye huunga mkono timu inayoungwa mkono na mwanawe wa kiume Ligi Kuu England, klabu ya Arsenal. Yeye pia ni shabiki wa Gor Mahia FC ya Kenya. Anasema wakati mmoja alikwenda hafla ya Wakfu wa Didier Drogba lakini mwanawe akawa amemwambia apate saini za wachezaji wa Arsenal pekee, alibahatika kupata saini ya Thierry Henry.

Katika tovuti ya Beffta, kufikia mwaka 2011, wanachama wa shirika hilo la tuzo wameorodheshwa kama Sama Ndango ambaye ni mtangazaji mwigizaji na mtoa mafunzo ya kuwahamasisha watu. Makao yake ni Uingereza lakini anaonekana asili yake ni Cameroon. Alikuwa na kipindi cha televisheni kwa jina The Sama Ndango Show.

Kulikuwa pia na Christine Rugurika Kayisha ambaye ni mwandishi wa hadithi na mwelekezi wa vipindi na filamu na michezo ya kuigiza. Asili yake ni Burundi.

Mwingine ni mwanamuziki wa mtindo wa rap Chuka Royalty, mjasiriamali na mwanamitindo kutoka Zambia Ethel Elaka na Verona White ambaye ni mjasiriamali pia ambaye amekuwa akifanya kazi Uingereza kwa muda mrefu.

Tuzo hiyo ni ya aina gani?

Maswali ambayo baadhi ya watu mtandaoni wamekuwa wakijiuliza ni iwapo shirika hilo ni la kweli na iwapo tuzo yenyewe ipo.

Kwenye ujumbe wa Instagram, wameeleza sababu ambayo imewafanya 'kutoa' tuzo hiyo.

Kwamba kwa muda mrefu, mchango wa wanawake katika ufanisi katika fani mbalimbali Afrika umekuwa hautambuliwi.

"Hii ni kweli zaidi hasa unapoangazia masuala muhimu kama vile siasa na maendeleo. Kinyume na wenzao wa kiume, katika mfumo tulio nao sasa, wanawake wengi wanasiasa Afrika wamelazimika kukumbana na changamoto nyingi zikiwemo za kiuchumi na unyanyapaa," wameeleza.

"Barani Afrika, hudaiwa kwamba mwanamke nafasi yake ni jikoni. Hata hivyo, wanawake wanasiasa waliofanikiwa wamekuwa wakijaribu kubadilisha hili na kudhihirisha kwamba wanawake wanaweza kufanikiwa katika siasa na kuwa viongozi wema."

Kasoro inajitokeza kwenye ujumbe unaofuata, ambapo sentensi hiyo inaonekana kutokamilika. Inasema: "Katika visa vingi, wanawake ambao wanajiingiza kwenye siasa mara nyingi...(na kukomea hapo). Wanaandika tu, Piga kura hapa #befftaawards"

Kasoro katika majina na ujumbe

Katika mwanzo wa kueleza umuhimu wa tuzo hiyo, wameacha herufi 'A' wakiandika Afrika, wameandika 'frica'.

Ukichunguza zaidi unapata wamekosa pia katika kuandika jina la taifa la Zimbabwe. Ingawa Kiongozi wa upinzani Zimbabwe Nelson Chamisa ameapa kuwa atalibadilisha jina la nchi hiyo na kuwa "Great Zimbabwe" akieleza kuwa jina la sasa la nchi hiyo lina 'laana', bado halijabadilika. Kwenye ujumbe wa Beffta, badala ya kuandika Zimbabwe, wameandika Zimbambwe.

Jina la rais wa zamani wa Liberia ni Ellen Johnson Sirleaf, lakini jina lake la kwanza wameandika Elle badala ya Ellen.

Washindi ni wangapi? Wema Sepetu na Zari Hassan je?

Ujumbe mkuu ulio katika ukurasa wa kwanza ni wa tuzo za mwaka 2017 ambapo wameandika watakuwa na wiki maalum ya kuwaenzi watu mashuhuri kutoka maeneo mbalimbali duniani kati ya 23-28 Oktoba, 2017.

Shirika hili la Beffta halijaeleza mshindi atatangazwa lini wala utaratibu utaoafuatwa kumchagua mshindi. Wametoa wito kwa watu kuwapigia kura wanaotaka watunukiwe tuzo hiyo kupitia kitambulisha mada cha #befftaawards.

Aprili 6, Beffta walikuwa wametoa ujumbe mwingine wa waliokuwa wameorodheshwa kushindania tuzo ya Wanawake Wahamasishaji Bora zaidi Afrika. Walikuwa wameorodhesha mwigizaji na Miss Tanzania wa zamani Wema Sepetu na mfanyabiashara mzaliwa wa Uganda Zari Hassan.

Chanzo cha picha, @beffta_award

Hakuna taarifa iwapo mshindi ameshatangazwa kufikia sasa au shughuli hiyo itafanyika baadaye mwaka huu. Tofauti ya jina la tuzo hii ya Aprili na ya sasa ni kuongezwa kwa siasa.

Kutunukiwa kwa Raila Odinga

Mwezi Mei mwaka huu, kuliibuka taarifa kwamba kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga alikuwa ametunukiwa tuzo na Beffta kutokana na juhudi zake katika kupigania utawala bora.

Taarifa iliyoandikwa na gazeti la kibinafsi la Star la Kenya inasema alifika kwa sherehe ya kupokea tuzo hiyo lakini haina picha za tukio lenyewe. Mwandishi wa taarifa hiyo ananukuu taarifa nyingine ambazo anasema ziliripoti Bw Odinga alizungumzia hatua yake ya kusalimiana kwa mkono na kuridhiana na Rais Uhuru Kenyatta baada ya utata uliogubika taifa hilo baada ya uchaguzi mku wa mwaka jana.

Anadaiwa kusema kwamba kuridhiana kwake na Bw Kenyatta ni hatua ambayo inaweza kuigwa na mataifa mengine ya Afrika ambayo yamekumbwa na mizozo ya kisiasa.

Shaka kuhusu tuzo

Baadhi ya watu mtandaoni wametilia shaka uhalali wa tuzo hizo, mfano huyu Kennedy Mmari kwenye mtandao wa Twitter. Tumewaandikia Beffta ujumbe wa barua pepe tukitaka ufafanuzi zaidi lakini kufikia sasa hatujapokea jibu.

Chanzo cha picha, TWITTER