Meja Jenerali Qassem Soleimani wa Iran amuonya Trump kwamba vita 'vitaharibu kila anachomiliki'

Picha za Meja jenerali Qassem Soleimani (kushoto), Donald Trump (kulia) Haki miliki ya picha Getty/Reuters

Kamanda wa kikosi maalum cha Iran amemuonya rais Donald Trump kwamba taifa lake litaharibu 'kila kitu kinachomilikiwa na rais huyo' iwapo Marekani itashambulia Iran.

Meja Jenerali Qassem Soleimani aliapa kwamba iwapo bwana Trump ataanzisha vita, 'jamhuri ya Iran itamaliza vita hivyo', chombo cha habari cha Iran tasnim kiliripoti.

Matamshi yake yanafuatia matamshi ya Trump katika mtandao wa Twitter akimuonya rais wa Iran kutojaribu kutishia Marekani.

Hali ya wasiwasi imezuka tangu Marekani ilipojiondoa katika makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran ya mwaka 2015.

Meja jenerali Soleimani-ambaye anaongoza kitengo cha jeshi la Quds kutoka katika jeshi la Iran la elite Revolutionary Guards - alinukuliwa siku ya Alhamisi akisema, 'kama mwanajeshi ni wajibu wangu kujibu vitisho vyako'.

"Zungumza nami sio rais [Hassan Rouhani]. Sio heshima ya rais wetu kukujibu''

"Tunakukaribia , pale ambapo huwezi dhania. Njoo tuko tayari''.

"Iwapo utaanza vita, tutamaliza vita hivyo. Unajua kwamba vita hivi vitaharibu kila unachomiliki."

Pia alimshutumu rais huyo wa Marekani kwa kutumia lugha ya vilabu vya burudani na maeneo ya kucheza kamare".

Siku ya Jumapili, bwana Trump alituma ujumbe wa kumtishia rais wa Iran.

Lakini siku mbili baadaye , akizungumza na kundi la wakongwe , rais alisema , 'Marekani iko tayari kufikia makubaliano ya kweli na Iran'

Ujumbe mkali ya bwana Trump ulikuwa ukijibu onyo ambalo rais Rouhani alitoa kwa Marekani.

"Marekani inafaa kujua kwamba amani na Iran ndio amani kubwa zaidi duniani, na vita dhidi ya Iran ndio vita vikubwa zaidi duniani'', alisema mapema kulingana na chombo cha habari cha Iran Irna.

Mnamo mwezi Mei , Trump alitangaza kwamba Marekani inajiondoa katika makubaliano ya mpango wa kinyuklia ya Iran yaliotiwa sahihi na utawala wa rais Obama , ikiwa ni kinyume na ushauri uliotolewa na Ulaya.

Bwana Trump alisema kuwa mkataba huo wa Iran ulikuwa 'mbaya zaidi'.

Ikijibu, Iran ilisema kuwa inajiandaa kuanzisha mpango wa kuzalisha Uranium , ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa kawi ya nyuklia pamoja na silaha.

Washington sasa inaiwekea vikwazo vya mafuta na vyuma Iran licha ya pingamizi kutoka kwa Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Ujerumani ambao wote walitia saini makubaliano hayo ya 2015.

Lakini kuna maswala mengine pia. Marekani inaituhumu Iran kwa vitendo vibaya katika mashariki ya kati na inaungwa mkono na Israel pamoja na Saudia, mataifa ambayo yana uhasama na Iran.

Iran imesisitiza kuwa mpango wake wa kinyuklia ni wa amani na makubaliano hayo ya 2015 yamethibitishwa na kitengo cha kawi ya Atomiki duniani .

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii