Hezron Mogambi: Sababu za kuchomwa shule nchini Kenya

Zaidi ya shule 50 zimekumbwa na visa vya moto kote nchini Kenya tangu mwaka wa 2018 kuanza

Zaidi ya shule 50 zimekumbwa na visa vya moto kote nchini Kenya tangu mwaka wa 2018 kuanza - huku visa vingi vikihusishwa na wanafunzi wa shule husika. Ziaidi ya wanafunzi wapatao elfu 6,000 waliathirika kutokana na visa hivi shuleni nchini Kenya.

Ingawa sababu zinazohusishwa na visa hivi hazijabainishwa rasmi na uchunguzi wowote, ni bayana kuwa kuna maswala mengi ambayo yamechangia hali ya utata katika shule nyingi za sekondari nchini Kenya.

Huku haya yakijiri, ni bayana kuwa kama ilivyotangaza serikali ya Kenya kupitia kwa wizara ya elimu, wazazi ndio watakaolipia gharama ya marekebisho na ujenzi wa uharibifu ulioshuhudiwa kwenye shule zenyewe. Hata hivyo, wizara ya elimu ya Kenya bado haijabaini dhamani ya mali iliyoharibiwa katika visa hivi vya moto shuleni.

Pia, katika hatua ambayo ni tofauti na ilivyokuwa awali, wanafunzi wanaolaumiwa kwa visa hivi vya moto katika shule mbali mbali wamefikishwa mbele ya mahakama mbali mbali kujibu mashtaka. Mwendesha mashtaka nchini Kenya, Noordin Haji, na mkurugenzi wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) George Kinoti wamemesema kuwa wanafunzi watakaopatikana na hatia ya kuchoma shule zao watahukumiwa.

Wanafunzi husika mashakani

Tayari, wanafunzi wanne wa shule ya upili ya Kithimani HGM kaunti ya Machakos wamehukumiwa mwaka mmoja jela kwa kushiriki katika kuichoma bweni ya shule hiyo. Wanafunzi hao walidaiwa kuichoma bweni ya shule hiyo yenye dhamani ya Ksh.1.6 million mnamo 31, 2016.

Aidha, wanafunzi ambao wamerudi shuleni baada ya uchomaji wa majengo katika shule zao mbali mbali wametakiwa kulipia uharibifu waliotekeleza. Wanafunzi wamekuwa wakitakiwa kulipa kati ya Sh1,000 and Sh5,000 ili kufanyia marekebisho sehemu za shule zilizoharibiwa.

Zaidi ya haya, huku wakirejea shuleni mwao, wanafunzi wao hao wamejikuta wakilazimika kulala katika hali mbaya kwa kuwa shule nyingi zimeyageuza madarasa na kwingine, vyumba vya mankuli, kuwa mabweni ya muda.

Shule nyingi zilizoathirika na uchomaji wa baadhi ya nyenzo zake sasa zinajikuta katika hali ngumu kwa sababu muhula huu wa masomo unamalizika Agosti 3 na shule hizo zinahitaji pesa za kuweza kujenga upya baadhi ya mabweni ya kulala kabla ya muhula wa tatu utakaoanza mwanzo wa mwezi wa Septemba.

Matayarisho duni ya mitihani ya kitaifa

Moja ya sababu ambazo zimetolewa na wadau katika sekta ya elimu nchini Kenya ni kutokana matayarisho duni miongoni mwa wanafunzi kwa mtihani wa kitaifa ambao unakaribia. Itakumbukwa kuwa kuanzia mwaka wa 2016 wakati mabadiliko katika mfumo wa mitihani yalipoanzishwa na aliyekuwa waziri wa elimu wakati huo, Dkt Fred Matiang'i, shule nyingi zilikumbwa na visa vya moto.

Katika mabadiliko hayo yaliyolenga kuziba mianya ya wizi na ulaghai katika mitihani ya kitaifa, wizara ya elimu iliharamisha baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanyika shuleni muhula wa tatu ambao unaanza mwisho wa mwezi wa Agosti; pamoja na siku za maombi ya mitihani kwa wanafunzi wa kidato cha nne na likizo za nusu muhula.

Ilipofanya hivi, wizara ya elimu ilihoji kuwa ilikuwa inakatiza mawasiliano kati ya wanafunzi na watu kutoka nje ya shule kwani wakati huu ndio uliotumika kuwapa wanafunzi baadhi ya makaratasi ya mitihani iliyoibwa.

Chama cha walimu nchini Kenya, KNUT, kinasema kuwa kitaunga mkono wizara ya elimu katika juhudi zake za kupambana na visa hivi vya moto shuleni. KNUT imelalamikia hali ya wanafunzi kuharibu mahabara na nyenzo nyingine shuleni kwa kuwa visa vya wanafunzi vilikuwa vinawaadhibu wazazi kwa kuwa ni wazazi ambao hatimaye watakaogharamia hasara hizo.

Uhamisho wa walimu

Aidha, sababu nyingine ambayo imetolewa kueleza visa hivi ambavyo vimezidi kuongezeka ni sera mpya ya uhamisho wa walimu wakuu wa shule za sekondari ambayo ilianza kufanya kazi mwaka huu ambapo zaidi ya walimu wakuu 500 waliathirika kote nchini.

Baadhi ya jamii zinazoishi karibu na shule na wanasiasa wamekuwa wakipinga kuhamishwa huku kwa walimu wakuu lakini Tume ya Kuwaajiri walimu ilishikilia kamba na shughuli yenyewe imekuwa ikiendelea.

Baadhi ya walimu wakuu waliohamishwa kwenda kuhudumu katika shule nyingine wamelalamikia hali ya ya kuharakishwa kutoka shule walizokuwa wakihudumu hapo awali kwa haraka na pia kupelekwa kuhudumu mbali na familia zao zinapokaa.

Ufadhili wa Shule

Pia, hali ya serikali kukosa kutuma pesa za ufadhili wa masomo kwa shule mapema ni tatizo kubwa kwa shule nyingi za sekondari. Itakumbukwa kuwa wanafunzi wamekuwa wakitoa sababu kama kukosa vitu vya kimsingi shuleni kama chakula cha kutosha na hali nyingine kama sababu za kugoma na kuchoma mabweni shuleni.

Hali hii imepelekea baadhi ya walimu wakuu wa shule za upili kutisha kufunga shule mapema kwa kukosa pesa za kuendesha shughuli za kawaida katika shule zao.

Inakisiwa kuwa wizara ya elimu inadaiwa na shule zaidi ya bilioni 6 ambazo hazitolewa kwa shule zote nchini kufikia sasa, hali ambayo mwenyekiti wa walimu wakuu wa shule za upili nchini Kenya, Kahi Indimuli, anasema inavuruga kuendeshwa kwa shule katika hali ya kawaida.

Hali katika shule za upili za kutwa ni mbaya mno kwa kuwa serikali inagharamia masomo katika shule hizo kote nchini.

Chama cha walimu KNUT, kinasema kuwa ni sababu kama hizi hasa kutowahusisha wadau wengine katika sekta ya elimu ndiyo inayosababisha na kuchangia visa vya utovu wa nidhamu shuleni.

Aidha, KNUT inataja sera kuhusu ununuzi wa vitabu, masomo ya shule za kutwa, masuala kuhusu mitihani ya kitaifa na sera nyingine ambazo wizara ya elimu imefanyia marekebisho bila kuwahusisha wadau wengine.

KNUT ilihoji wiki hii kwamba data ambayo imekusanywa na chama chake kote nchini inaonyesha kuwa tume ya kuwaajiri walimu (TSC) na wizara ya elimu ndizo zenye kulaumiwa kwa sera ambazo walianzisha bila kuwahusisha wadau wengine. Kiongozi huyu wa walimu anahoji kuwa ikiwa wizara ya elimu na serikali haitabadilisha mwendo wake wa utendakazi na kuwahusisha wadau wengine, hali itaendelea kuzorota.

Baadhi wadau wameelekeza lawama kwa sera ya elimu iliyoondoa matumizi ya kiboko kama njia ya kuwaadhibu wanafunzi shuleni nchini Kenya. Baadhi ya walimu, wadau na wazazi sasa wanalalamika kuwa wanafunzi wamemea pembe kwa sababu ya walimu kukosa njia mbadala za kuwanidhamisha wanafunzi wanapofanya makosa shuleni kwa njia ya haraka.

Jambo hili limewaacha walimu bila la kufanya mbele ya wanafunzi wanaofahamu haki zao katika enzi hizi za mitandao ya kijamii na kusambaa kwa habari kwa haraka. Ingawa suala hili limewahi kuzuka miaka ya nyuma, serikali imekuwa ikisisitiza kuwa matumizi ya kiboko shuleni yaliharamishwa na haiwezi kurejeshwa tena kama njia ya kuwaadhibu wanafunzi.

Adhabu kwa wanafunzi na mitandao

Kwa sababu ya kuwa na wanafunzi ambao wanapata habari kwa njia za haraka kuliko ilivyokuwa zamani na walimu kukosa njia za haraka za kuwaadhibu wanafunzi, walimu wengi wamelitupilia mbali suala la adhabu na kuzingatia kazi zao za kufundisha darasani.

Hili hii ambapo wanafunzi wameonekana kutawala katika shule nyingi nchini pia kutoka na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kwa sababu ya mfumo wa shule za kutwa kulipiwa na serikali, imewafanya walimu wengi limepelekea idadi kubwa ya wanafunzi kuwa bila ushauri ama kushughulikiwa nje ya madarasa yao.

Mwenyekiti wa chama cha walimu wa shule za upili na taasisi anuwai, Akello Misori anaeleza kuwa hali hii inasumbua waalimu katika kutekeleza wajibu wao shuleni. Aidha, ukweli kuwa walimu wanaosimamia ushauri katika shule za upili kote nchini ni wachache na wana kazi nyingi shuleni inatishia kuchafua hali zaidi.

Hali hii ninatokana na ukweli kuwa walimu wanaowashauri wanafunzi wana majukumu mengi kama walimu kando na kuwa washauri shuleni mwao. Pamoja na kwamba shule nyingi hazina washauri na zile zilizonao, zina mmoja tu ambaye anawashauri wanafunzi zaidi ya 1,000.

Sasa, baadhi ya wadau wanapendekeza kuajiriwa kwa wataalam washauri ambao hawatakuwa na majukumu ya kufundisha katika shule bali watafanya kazi hiyo pekee ili kumudu hali iliyoko na kuwashauri wanafunzi inavyohitajika.

Pia, baadhi ya wadadisi katika sekta ya elimu nchini Kenya wanahoji kuwa hatua kama hii itasaidia pakubwa kwa sababu baadhi ya wazazi wamewaachia walimu kazi ya kuadibisha , kuwalea na kuwarekebisha wanafunzi jambo ambalo linavuruga hali zaidi katika shule nchini Kenya.

Ni wazi kuwa kuna maswala mengi sana amabyo yanahitaji kushughulikiwa katika sekta ya elimu nchini Kenya. Itambidi waziri Amina Mohamed na maafisa wakuu wa wizara kuchukua hatua ambazo zitasaidia kurejesha hali ya utulivu ili masomo kuendelea kama kawaida.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii