Ajuza wa miaka 80 ambaye ni fundi stadi wa redio za magari Kenya

  • Jason Nyakundi
  • BBC Swahili
"Kazi ni kazi, hakuna kazi ya kufanywa na mwanamume au mwanamke," anasema Cecilia
Maelezo ya picha,

"Kazi ni kazi, hakuna kazi ya kufanywa na mwanamume au mwanamke," anasema Cecilia

Cecilia Wangari au (Shosh) kama vile wengi wanavyomfahamu ni bibi wa miaka 80 ambaye amepata umaarufu kwa haraka hasa mjini Nairobi nchini Kenya.

Kinyume na bibi wengine walio na umri sawa na wake ambao mara nyingi huishi vijijini wakiwategemea watoto wao au hata wajukuu kuwalisha kwake Cecilia ni tofauti kabisa. Cecilia ni fundi wa radio za magari! ndio fundi wa redio za magari.

Maelezo ya picha,

Cecilia akiwa katika harakati za kuibadilisha redio ya mteja

BBC ilipomtembelea kwenye duka lake la kuuza, kurekebisha na kuweka upya radio za magari lililopo barabara ya Outering mjini Nairobi, ilimpata akiwa na shughuli nyingi huku wateja waliokuwa wakihitaji msaada wake wakiingia mmoja baada ya mwingine.

Maelezo ya picha,

Cecilia kazini

"Mimi nilizaliwa Nairobi na nimefanya biashara kadhaa tangu miaka ya sabini na hata nilikuwa na gari langu.

Nilikuwa nimeajiri dereva na kondakta lakini mara nyingi walikuwa wananilaghai wakinidanganya kuwa gari limeharibika ninawapa pesa lakini hawanunui vipuri. Ndipo nikaamua nifanye kazi ambayo nitakuwa naisimamia mimi mwenyewe".

Maelezo ya picha,

Jinsi kazi inakwenda

Cecilia anaonekana bayana kuwa na ujuzi wa juu kuhusu mambo ya radio za magari kulingana na jinsi anavyoelezea na kushughulikia wateja wake.

Anasema licha ya yeye kutokuwa na kisomo chochote alianza kujifunza taratibu kuanzia mwaka 1991 kukarabati na kufunga redio za magari kwa fundi mmoja mara nyingi kwa kuangalia tu jinsi kazi hiyo ilikuwa ikifanywa.

Maelezo ya picha,

Wakati wa kuifanyia redio majaribio

"Fundi aliyenifundisha aliniambia ninunue vifaa vichache tu ambavyo nilitumia kujifunzia hii kazi na tangu wakati huo nimeifanya kazi hii kwa miaka yote hii, ni kazi ninayoifurahia kwa saabu ninaipenda," anasema Cecilia.

Maelezo ya picha,

Cecilia akikarabati mitambo

Shosh ana vijana kadhaa wanaomsaidia na kazi kwenye duka lake na baadhi yao ni wajukuu wake ambao anasema anataka awasaidie kujimudu kimaisha na waweze kujitegemea siku za usoni. Wateja wengi wanaofika duka la Shosh hutaka huduma yake mwenyewe.

Maelezo ya picha,

Akihudumia wateja

Anasema siri kuu ambayo imechangia yeye kuwa kwenye biashara hii kwa kipindi kirefu kama hiki na wateja kumpenda ni kuwa mkweli kwa kazi yake na kuwaheshimu wateja.

"Kila wakati ninahakikisha kuwa wateja wangu wameridhika na huduma yangu na pia ninawazungumzia kwa njia nzuri ndio wapate kurudi tena".

Maelezo ya picha,

"Kazi ni kazi, hakuna kazi ya kufanywa na mwanamume au mwanamke," anasema Cecilia

Anasema biashara hii imemwezesha kujikimu kimaisha. Anawashauri watu wote, wanaume kwa wanawake, wasichana kwa wavulana wasichague kazi.

"Kazi ni kazi, hakuna kazi ya kufanywa na mwanamume au mwanamke, hata kama ni ya kupaka viatu rangi , ni kazi inayoweza kufanywa na kila mtu, kwa hivyo mtu asichague kazi".

Maelezo ya picha,

"Kazi ni kazi, hakuna kazi ya kufanywa na mwanamume au mwanamke," anasema Cecilia

Pia anasema kuwa kufanya kazi kwa uaminifu imekuwa nguzo muhimu kwa biashara kwa kazi yake. Ni lazima kila wakati ahakikishe kuwa ana leseni zote zinazohitajika kwa biashara yake ili kazi yake iweze kuendelea.

"Ni lazima nihakikishe kuwa duka langu lina leseni na hata bango lililo nje ya duka na ni lazima nililipie ili kuhakikisha kuwa ninafanya biashara bila ya usumbufu wowote".

Licha ya umri wa miaka 80 Cecilia anasema ana ndoto kubwa ya siku za usoni. "Ningependa siku moja niwe na shule ya kuwafunza vijana kazi hii ya ufundi wa redio. Niwe na shule ambayo mimi mwenyewe nitahakikisha kuwa nimempa mwanafunzi cheti baada ya kuhitimu vizuri".

Maelezo ya picha,

Angependa siku moja niwe na shule ya kuwafunza vijana kazi hii ya ufundi wa redio

Cecilia anasema hana mpango wa kuachana na hii kazi hivi karibuni. "Hata kama Mungu atakubali niishi miaka 200 hii kazi nitaifanya tu", anasema.

Maelezo ya picha,

Cecilia anasema hana mpango wa kuachana na hii kazi hivi karibuni. "Hata kama Mungu atakubali niishi miaka 200 hii kazi nitaifanya tu", anasema.

Unaweza kusoma pia: