Mugabe: Sitampigia kura Emmerson Mnangagwa

Mugabe alisema kuwa hatampigia kura mrithi wake Emmerson Mnangagwa Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mugabe alisema kuwa hatampigia kura mrithi wake Emmerson Mnangagwa

Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amefanya mazungumzo ya kushtukiza na vyombo vya habari wakati ambapo taifa hilo linafanya uchaguzi siku ya Jumatatu.

Mugabe amesema hatamuunga mkono Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa, baada ya kushinikizwa kuondoka madarakani na ''chama nilichokianzisha''.

''Siwezi kuwapigia kura walionitesa,'' alisema .''Nitafanya uamuzi wangu miongoni mwa wagombea wengine 22''.

Raia wa Zimbabwe watapiga kura Jumatatu, kura za kwanza tangu Mugabe alipoondolewa madarakani mwezi Novemba.

Akizungumza akiwa nyumbani kwake, mjini Harare, siku ya Jumapili, Mugabe alisema kuwa ''alifukuzwa'' ikiwa ni sehemu ya mapinduzi ya kijeshi na kuwa aliamua kuondoka madarakani ''kuepuka mogoro''.

Alisema sasa anamtakia kila la heri Kiongozi wa chama cha upinzani , MDC, Nelson Chamisa , katika kura za siku ya Jumatatu.

''Anaonekana kufanya vizuri, na kama atachaguliwa namtakia kila la heri'', Alisema bwana Mugabe.

Alipoulizwa na BBC kama atapenda kuona Bwana Chamisa akishika madaraka nchini Zimbabwe,Mugabe alieleza kuwa Chamisa ni mgombea pekee mwenye uwezo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Emmerson Mnangagwa mgombea urais kwa tiketi ya Zanu-PF

Mugabe alisema:''Nina matumaini kuwa uamuzi wa kupiga kura kesho, utatamatisha utawala wa kijeshi na kuturejesha katika utawala wa kikatiba.

''Acha kesho sauti za watu ziseme kuwa hatutakuwa na kipindi ambacho jeshi linakuwa na uwezo wa kumuweka mtu madarakani''.

Mugabe pia alikana kuwa, alipokuwa Rais, alikuwa na mipango ya kukabidhi madaraka kwa mkewe Grace, akisema kuwa ilikuwa ''Upuuzi mtupu'', na kusema kuwa waziri wa zamani wa ulinzi Sydney Sekeramayi angechukua nafasi yake.

Bwana Mugabe alisema,tangu aliposhinikizwa kuondoka madarakani mwaka jana,''Watu wa Zimbabwe hawajawa huru''.

Nyoka na 'Bundi wa miujiza', marufuku katika uchaguzi Zimbabwe

Zimbabwe yaomba kujiunga tena na Jumuiya ya Madola

Zaidi ya watu milioni tano nchini humo wanajiandaa kwenda kupiga kura kwa mara ya kwanza baada ya miaka 38 bila Mugabe kuwa madarakani.

Kura za maoni juma lililopita MDC na Zanu-PF zilikaribiana kwa alama 11 kwa 3, huku 20% ya wapiga kura wakiwa hawajaamua.