Biashara ya Benki Tanzania yasuasua kutokana na wateja kutolipa madeni

Mkurugenzi wa Benki ya CRDB,Dokta Charles Kimei Haki miliki ya picha The Citizen
Image caption Mkurugenzi wa Benki ya CRDB,Dokta Charles Kimei amesema unapokuwa na mikopo isiyolipika ni kikwazo kwa ustawi wa benki

Biashara ya Benki nchini Tanzania imeendelea kuwa ngumu kwa baadhi ya taasisi kubwa za kifedha ambapo faida ya benki hizo imekuwa ikisuasua kwa miaka miwili sasa.

Wiki hii benki nchini Tanzania zimechapisha ripoti ya mwenendo wa hali ya biashara kama wanavyopaswa kwa mujibu wa sheria.

Gazeti la kilasiku la Kiingereza la The Citizen limeripoti hii leo Jumanne kuwa mdororo huo wa faida umetokana kwa kiasi kikubwa na mikopo ya wateja isiyolipwa (Non-Performing Loans).

Benki ya NMB ambayo inatajwa kuwa ndiyo taasisi kubwa zaidi ya kifedha Tanzania faida yake imeshuka na kufikia Sh bilioni 66.8 za Tanzania kwa kipindi cha Januari 1 mpaka Juni 30 mwaka huu kutoka Sh bilioni 76.2 kwa kipindi kama hicho mwaka 2017.

Hata hivyo, NMB wamefanikiwa kupunguza idadi ya madeni hayo yasiyolipika kutoka 6.6% mwezi Machi 2018 mpaka 5% kufikia mwezi Juni 2018.

Benki ya CRDB inatajwa kuwa ya pili kwa ukubwa nyuma ya NMB, nayo pia faida yake imeshuka kutoka Sh bilioni 39.6 kwa nusu ya mwaka 2017 mpaka Sh bilioni 32.6 kwa nusu yam waka huu, 2018.

Huwezi kusikiliza tena
Biashara ya Benki Tanzania yasuasua kunani?

Kiwango cha riba chapunguzwa Kenya

Je Afrika iko wapi katika uchumi unaokadiriwa kukuwa duniani 2018?

Hivi Karibuni, BBC ilifanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Charles Kimei ambaye alisisitiza kuwa mikopo isiyolipika ni kikwazo kikubwa cha ustawi wa benki.

"Unapokuwa na mikopo isiyolipika, faida inashuka na kwa hivyo huwezi kukuza akiba yako ya limbikizo la faida ambayo inatumika kama sehemu ya mtaji na hilo ni tatizo kubwa sana," alisema Kimei.

The Citizen inaripoti kuwa sekta ya benki kwa ujumla wake nchini Tanzania iliingiza faida ya Sh bilioni 426 mnamo mwaka 2014, faida hiyo ilikuwa na kufikia Sh bilioni 438 kwa mwaka 2015. Hata hivyo kiasi hicho cha faida kilishuka mpaka Sh bilioni 423 mwaka 2016 na kuporomoka Zaidi mpaka Sh bilioni 286.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya uchumi, uwepo wa mikopo isiliyolipika unatokana na upungufu wa fedha katika mzunguko na hivyo kuathiri hali ya biashara na ulipwaji wa madeni.

Mada zinazohusiana