Uchaguzi Zimbabwe: Ghasia zazuka kati ya upinzani na maafisa wa usalama

Ghasia nchini Zimbabwe

Chanzo cha picha, Reuters

Ghasia zimezuka nchini Zimbabwe kati ya wafuasi wa upinzani na vikosi vya usalama katika mji mkuu wa Zimbabwe huku kukiwa na maandamano dhidi ya kucheleweshwa kwa matokeo ya uchaguzi

Magari yaliobeba maji ya kuwatawanya waandamanaji na vitoa machozi yalitumiwa katika barabara muhimu za mji wa Harare baada ya wafuasi wa chama cha upinzani cha MDC Alliance kuweka vizuizi katikati ya mji huo.

Mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi. Muungano wa Ulaya umeonyesha wasiwasi wake kuhusu kucheleweshwa kwa matokeo.

Maandamano hayo ya wafuasi wa chama cha upizani cha MDC mjini Harare yalibadilika na kuwa mabaya nyakati za mchana.

Chanzo cha picha, Reuters

Makundi ya waandamanaji yalikuwa katikati ya mji huo tangu alfajiri lakini habari zilipozuka kwamba Zanu Pf imeshinda viti vingi katika bunge na kwamba matokeo ya urais hayakuwa tayari , hali ilibadilika.

Walifanya maandamano katika barabara muhimu mjini Harare na kuelekea katika ofisi za zamani za chama cha Zanu Pf wakibeba mawe makubwa , fimbo na chochote kila ambacho wangeweza kubeba.

Kundi hilo lilisema 'tunamtaka Chamisa', wanaamini kwamba uchaguzi huo umekumbwa na udanganyifu na sasa wanataka mgombea wa MDC kutangazwa mshindi.

Matokeo yanaonyesha kwamba Zanu-PF inashinda viti vingi vya ubunge katika uchaguzi huo tangu kung'atuliwa madarakani kwa Robert Mugabe

Matokeo ya kura ya urais yanatarajiwa baadaye siku ya Jumatano.

Mapema , chama cha upinzani cha MDC Alliance kilikuwa kimesema kwamba kura hiyo ilifanyiwa udanganyifu na kwamba mgombea wake Nelson Chamisa alikuwa ameibuka mshindi.

Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe Zec imetangaza kwamba Zanu Pf kufikia sasa imejishindia viti 110 huku MDC ikijipatia viti 41 kulingana na chombo cha habari cha ZBC.

Kuna viti 210 katika bunge la taifa hilo.

Uchaguzi wa Jumatatu ulivutia asilimia 71 ya wapiga kura. Chombo cha habari cha ZBC kimesema kuwa Zec itatangaza matokeo ya uchaguzi wa urais mwendo wa 12.30 za Zimbabwe.

Waangalizi wa uchaguzi wanasemaje?

Muungano wa Afrika umesema kuwa uchgauzi huo ulikuwa huru na wa haki , akiongezea kuwa unaadhimisha wakati muhimu wa mabadiliko ya kisiasa.

Ripoti ya awali kutoka waangalizi wa SADC inasema kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa amani na ulifanyika kulingana na sheria.

Wawakilishi wake, waziri wa maswala ya kigeni nchini Angola Manuel Domingos Augusto ameutaja uchaguzi huo kuwa kidemokrasia.

Muungano wa Comesa ulisifu tume ya uchaguzi kwa kutumia kifaa cha Biometric kusajili wapiga kura akisema kuwa kimepunguza uwezekano wa watu kupiga kura zaidi ya mara moja.

Muungano wa EU na waangalizi wa uchaguzi kutoka Marekani wanatarajiwa kutoa ripoti yao baadaye siku ya Jumatano.

Je vyama pinzani vinasema nini?

Upinzani nchini Zimbabwe unasema kuwa mgombea wake wa urais Nelson Chamisa, ameshinda uchaguzi mkuu wa Jumatatu.

Chama cha upinzani cha MDC kinasema kuwa chama tawala cha Zanu-PF kinajaribu kufanya udanganyifu ili kumruhusu Emmerson Mnangagwa kushinda , na kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo hakutakubalika.

Tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuwa hakuna udanganyifu na inahitaji muda ili kuhesabu kura hizo.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari mjini Harare, Tendai Biti wa chama cha MDC Alliance amesema kuwa kuna jaribio la wazi linalofanywa na Zanu-Pf kuingilia chaguo la wananchi.

Zanu-Pf ambacho kimekuwa madarakani tangu 1980 kimeshutumiwa kufanya udanganyifu katika miaka ya nyuma ili kumweka Mugabe madarakani.

Hatahivyo msemaji wa chama amesema kuwa hajui kile bwana Tendai Biti anachozungumzia .

Alikionya chama hicho kutosababisha ghasia nchini humo.

Douglas Mwonzora ,afisa wa juu wa chama cha MDC hatahivyo aliambia BBC kwamba uungwaji mkono wa mgombea wao na kiongozi wa zamani Robert Mugabe ulikinyima kura chama hicho.

Aliongezea kwamba chama tawala kiliwahonga wapiga kura katika maeneo ya mashambani.

Waziri wa maswala ya ndani nchini humo Obert Mpofu alituma ujumbe wa twitter akisema kuwa wale waliokiuka sheria za uchaguzi wakitangaza kuwa washindi huenda wakakabiliwa na mkono mrefu wa sheria.

Rais Mnangagwa alituma ujumbe wa Twitter akisema kwamba ana matumaini na matokeo na kuwawataka raia wa Zimbabwe kusubiri tangazo la mwisho.

Wogombea wakuu

Emmerson Mnangagwa, Zanu-PF

Chanzo cha picha, AFP

Nelson Chamisa, MDC Alliance

Chanzo cha picha, Reuters