Tanzania: Ni hatua gani zichukuliwe kudhibiti utupaji wa taka barabarani

Taka zilizotupwa barabarani Haki miliki ya picha Getty Images

Imekuwa ni kawaida sana unapokutana na taka barabarani na hasa katika barabara kuu ya Morogoro. Barabara ambayo imekuwa ikitumika kwa ajili ya safari za kuelekea katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Lawama nyingi hutolewa kwa abiria na madereva wa mabasi ya mikoani na wale wa daladala wanaopita katika barabara hizo.

Na kumekuwa na kampeni kadha wa kadha huku kila halmashauri husika ikipambana kwa kuweka kanuni na tozo mbali mbali ili kudhibiti uchafuzi huo wa mazingira.

Siku moja iliyopita naibu waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na mazingira), Mussa Sima, akiwa katika ziara ya kikazi huko Kongwa Dodoma, aliwaagiza wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria kuhakikisha abiria hawatupi taka pembezoni mwa barabara ili kuzuia kuharibu mazingira pamoja kupoteza mifugo iliyokula taka hizo.

Kwa mujibu wa naibu waziri huyo alisema mifugo mingi inakufa kiholela kutokana na kula taka zinazotupwa na abiria wa mabasi.

Na alisisitiza kuwa ofisi ya makamu wa Rais haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika na ukiukwaji huo.

Hii si mara ya kwanza viongozi wa serikali ya Tanzania kukemea na kutangaza adhabu kali kwa watakaopatikana wakitupa takataka.

BBC imefanya mazungumzo na Fazal Issa mratibu wa asasi ya maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi Tanzania Forum CC.

"Serikali inaweza kuhamasisha ujasiriamali wa Taka. wafanyakazi wa kwenye mabasi wanaweza kuwa na vituo maalumu ambapo taka zinazo kusanywa wana zipeleka katika vituo hivyo na kuweza kutumiwa na wajasiriamali kwani kuna vikundi vingi na makampuni mengi sasa hivi yanafanya ujasiriamali kutokana na taka hivyo itakua vizuri kuhamasisha watu wa vikundi na watu wa mabasi," anasema Fazal.

"Mara nyingi tumekuwa tukiona kampeni zinafanyika lakini zinakuwa na muda mfupi, kwahiyo kampeni ziwe za muda mrefu ziendane na sheria ndogondogo na sheria mama ya mazingira", anaongeza Fazal.

Hata hivyo anasisitiza kuwa Udhibiti wa uchafuzi wa mazingira unaweza tumia njia mbili, njia hasi ya kumlipisha faini yule aliyetupa takataka katika eneo lisilo rasmi au njia chanya ya kumzawadia yule ambaye amekuwa akitoa taarifa juu ya uchafuzi wa mazingira.

Huwezi kusikiliza tena
Lihepa, Mtanzania anayebadilisha taka kuwa mapambo

Anasema ni muhimu wauzaji wa vyakula wakabadilisha vifungashio vya chakula na kutumia vifungashio mfano wa karatasi ngumu ambayo ni rahisi kuoza ili viweze kuendana na mazingira.

Pia kwa makondakta kupitisha mfuko wa kuweka taka kwa abiria huku abiria kwa abiria waki simamiana katika ulinzi wa mazingira.

Nchi jirani za Kenya na Rwanda wamefanikiwa sana katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira hasa barabarani.

Kwa Kenya ukionekana unatupa uchafu au karatasi hovyo sheria itakubana. Kwa Mkenya hulipa Shs. 200/= za Kenya kama faini na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki na hutumia zaidi mifuko ya karatazi kubebea chakula.

Katika sheria ya Tanzania ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 ibara ya 190 inasema mtu yeyote atakuwa anatenda kosa endapo, bila ya kuwa na sababu inayokubalika au uhalali- (a) anatupa takataka yoyote ndani au juu ya eneo lolote linalotumiwa na umma.

Hata hivyo sheria hiyo ime bainisha juu ya adhabu ya uchafuzi wa mazingira kwa ujumla kuwa kulingana na tukio, inaweza kuwa tozo ya faini isiyopungua shilingi elfu hamsini na isiyozidi shilingi milioni hamsini, au kifungo kisichopungua miezi mitatu au kisicho zidi miaka saba jela ama vyote viwili .

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii