UN: Korea Kaskazini inaendelea na mpango wake wa kinyuklia'

Urushaji wa silaha ya masafa marefu Haki miliki ya picha KCNA
Image caption Korea kaskazini ilitekeleza msururu wa majaribio ya silaha za masafa marefu 2017

Taifa la Korea Kaskazini halijasitisha mpango wake wa kinyuklia pamoja na ule wa kutenegeneza silaha , hivyobasi kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa , kulingana na ripoti iliotolewa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Ripoti hiyo inasema kuwa Pyongyang imeongeza idadi ya meli zinazosafirisha bidhaa za mafuta na imekuwa ikijaribu kuuza silaha ng'ambo.

Ripoti hiyo ya siri ilioandaliwa na jopo la wataalam iliwasilishwa kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa siku ya Ijumaa.

Korea Kaskazini hadi kufikia sasa haijatoa tamko lolote kuhusu ripoti hiyo.

Wiki iliopita maafisa wa Marekani walisema kuwa Pyongyang ilikuwa ikitengeneza silaha za masafa marefu licha ya mkutano wa kufana na rais wa Marekani Donald Trump ambapo iliahidi kufutilia mbali mipango yake yote ya kinyuklia.

Afisa mmoja ambaye hakutajwa jina aliambia gazeti la The Washington Post kwamba setlaiti za upelelezi ziligundua kwamba kuna maswala yaliokuwa yakiendelea katika kituo ambacho kilikuwa kikiunda silaha za masafa marefu.

Rais Donald Trump alikutana na rais Kim Jong Un nchini Singapore mnamo mwezi Juni na viongozi hao waliahidi kufanya kazi pamoja kwa lengo la kusitisha mipango ya kinyuklia bila kuelezea kuwa ni hatua gani zitakazofuatwa.

Pyongyang kwa sasa imewekewa idadi kubwa ya vikwazo vya kimataifa pamoja na vile vya Marekani kutokana na mpango wake wa kinyuklia na majaribio ya silaha.

Je ripoti ya Un inasema nini?

Ripoti hiyo iliandaliwa na wataalam hao waliokuwa wakichunguza utekelezwaji wa vikwazo dhidi ya Umoja wa mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.

Ilionekana na baadhi ya vyombo vya habari mapema siku ya Jumamosi.

Ripoti hiyo inasema kuwa Korea Kaskazini haijasitisha mpango wake wa Kinyuklia pampja na ule wa silaha na inaendelea kukaidi uamuzi wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kupitia ongezeko la meli zinazosafirisha bidhaa za mafuta pamoja na usafirishaji wa mkaa kupitia baharini katika kipindi cha mwaka 2018.

Imesema kuwa Pyonyang ilijaribu kuuza silaha ndogo ndogo na nyepesi pamoja na silaha nyengine za kijeshi kupitia mataifa mengine ya kigeni kuelekea Libya , Yemen na Sudan.

Wataalam hao walimaliza kwa kusema kuwa taifa hilo limefanya vikwazo vya kifedha kutofanya kazi.

Ripoti hiyo ilitolewa huku waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo akisema kuwa anatumai kwamba Korea Kaskazini itaafikia mpango wa kusitisha utengenezaji wa silaha za kinyuklia

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii