Tanzania: Mzee Kimweri Dafa apewa zawadi ya kusherehekea miaka 100 ndani ya ndege ya Dreamliner

Mzee Kimweri Dafa na mwanawe Wakili Imam Dafa ndani ya ndege
Image caption Mzee Kimweri Dafa na mwanawe Wakili Imam Dafa ndani ya ndege

Mzee wa miaka 100 amesherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa kwa kusafiri na ndege kwa mara ya kwanza, kama zawadi aliyopewa na mtoto wake.

Akizungumza na mwandishi wa BBC Halima Nyanza ndani ya ndege, huku jicho akilitupa dirishani mara kwa mara kupata mandhari nzuri ya anga, kwa sauti ya utulivu bila ya woga, mzee Kimweri Dafa Kivo amesema anasikia furaha kutokana na kuwa ni mara yake ya kwanza.

Isitoshe, amekuwa miongoni mwa Watanzania wa mwanzo mwanzo walioabiri ndege mpya iliyonunuliwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) na kupokelewa mwezi uliopita.

''Mwanangu namshukuru sana kwa sababu aameweza kunipandisha kwenye ndege, nimefurahi sana..'' amesisitiza mzee Kimweri.

Akizungumzia zawadi aliyompa baba yake mtoto wa mzee Kimweri, Imam Dafa anasema ilimchukua muda kufikiria juu ya nini cha kumpa baba yake.

Image caption Mzee Dafa na Marubani wa ndege

''Nilikuwa nafikiria kwa kumshukuru Mungu na kumpa baba zawadi kwa kufikia umri huo nifanye nini, nilifikiria sana, basi nikaona nimpe baba zawadi ya kupanda ndege kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 100...'' alisema Imam.

Mataifa ya Afrika yaliyo na Dreamliner

Ethiopia (Ethiopian Airlines )*- 19

Kenya (Kenya Airways) - 8

Morocco (Royal Air Maroc) - 5

*Ethiopia pia wana Boeing B787-9 tatu, ambayo ni ndege kubwa kuliko 787-8 na inaweza kuwabeba abiria 290

Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya aina gani?

Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya kisasa. Bei yake inakadiriwa kuwa $224.6 milioni (Sh512 bilioni za Tanzania) kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti ya kampuni ya Boeing.

Ndege hiyo ya Tanzania ilisafiri kutoka uwanja wa Paine mjini Seattle, Washington safari ya umbali wa saa 22 siku ya kupokelewa kwake Julai.

Ndege hiyo hutumia injini ya kisasa zaidi aina ya Trent 1000 TEN

Injini hiyo inatumiwa katika ndege zote mpya aina ya Boeing 787 na huhifadhi mafuta, ambapo huwa inachoma mafuta kwa kiwango cha asilimia tatu chini ukilinganisha na ndege za aina hiyo na kuyatumia vyema zaidi.

Hilo huiwezesha kupunguza matumizi ya mafuta ukilinganisha na ndege nyingine za ukubwa kama wake kwa asilimia 20-25, aidha hupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kiwango sawa na hicho.

Aidha, huwa haipigi kelele sana. Ni ndege ambayo imechukua uwezo na kasi ya ndege kubwa aina ya 'jet' na kuuweka kwenye ndege ya ukubwa wa wastani.

Ina uwezo wa kubeba abiria 262 ni ya kisasa zaidi kuwahi kumilikiwa na serikali ya Tanzania. Mataifa mengine kama vile Kenya na Ethiopia hata hivyo yamenunua ndege kama hizo kadha.

Haki miliki ya picha IKULU
Image caption Rais Magufuli akiwa ndani ya ndege hiyo

Ndege hii ina uwezo wa kusafiri kiilomita 13,620 kwa wakati mmoja na urefu wake ni mita 57. Upana wa mabawa yake ni mita 60. Urefu wake kutoka chini hadi juu ni mita 17.

Rais Magufuli aligusia hilo alipokuwa anaipokea uwanja wa wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam aliposema: "Ndege hii ni ya kisasa na kote walikopita walikuwa wana uwezo wa kunipigia simu na kuongea nao angani."

Ethiopia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kando na Japan kuanza kutumia ndege aina ya Boeing 787-8 Agosti 2012.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 262, tayari ishaanza kutoa huduma kwa safari za ndani katika vituo vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza.

Mwezi Septemba itaanza safari zake kwenda Bombay nchini India, Guangzhou nchini China na Bangkok nchini Thailand.

Mada zinazohusiana