Mambo makuu kuhusu makubaliano mapya ya amani Sudan Kusini

Rais Kiir (kulia) na Riek Machar Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Kiir (kulia) na Riek Machar

Mahasimu nchini Sudan Kusini wameweka saini makubaliano ya kugawana madaraka huku Rais Salva Kirr akitoa wito wa kutaka kuwepo amani kwenye nchi ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Rais Kiir na hasimu wake Riek Machar walikuwa kwenye taifa jirani la Sudan kusaini makubaliano, ambapo kiongozi wa waasi Machar anatarajiwa kurejea kama makamu wa rais wa kwanza kati ya makamu wa rais watano kwenye serikali ya umoja.

Makubaliano hayo yenye lengo la kumaliza vita kwenye taifa hilo janga zaidi duniani yalitiwa sahihi mbele ya rais wa Sudan Omar al-Bashir na wenzake kutoka Kenya, Uganda na Djibouti wakiwemo pia wanadiplomasia wa kigeni.

Baada ya kusainiwa mukubaliano ya mwisho, mahasimu hao watakuwa na miezi mitatu ya kuunda serikali ya mpito ambayo itakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitatu.

Vita vya karibu miaka mitano nchini Sudan Kusini vilianza wakati Kiir alimlaumu aliyekuwa makamu wake wa rais Machar kuwa alikuwa anapanga mapinduzi mwaka 2013.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Vita vya Sudan Kusini vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, vikawalazimu watu milioni nne kuhama makwao

Pande za Kiir na Machar tayari zimekubaliana kuondoa kabisa vikosi vyao kutoka mijini kwenye mazungumzo ya hivi majuzi yaliyoongozwa na Bashir.

Mpangilio ya ugavi wa mamlaka unaeleza kuwa kutakuwa na mawaziri 35 kwenye serikali ya mpito wakiwemo washirika 20 wa Kiir na 9 wa Machar wakiwemo pia washirika wa makundi manne ya waasi.

Bunge litakuwa na wabunge 550 wakimemo 332 kutoka upande wa Kiir na 128 kutoka upande wa Machar.

"Makubaliano yaliyo kwenye karatasi ni makubaliano mazuri lakini utapata kuwa katika utekelezani ndio kuna changamoto na kulikuwa na makubaliano kuwa ikiwa hawangekubaliana kwenye mazungumzo hayo ilikuwa waje nchini Kenya lakini kwa wakati huu wameshakubaliana mikakati iliyopo ni kuhusu vipi yatatelezwa," kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya Sudan na Sudan Kusini Mohammed Jaffar.

Tayari Kiir ameonya kuwa ukubwa wa serikali itakuwa ni changamoto, "Ona ukubwa wa bunge, ona ukubwa na baraza la mawaziri. Utawalipa aje? alisema, akiongeza kuwa ana wasi wasi kuhusu ni kwa njia gani atawapa makao, maofisi na magari maafisa wapya.

Hata hivyo Marekani imetilia shaka mafanikio yatakayotokana na makubaliano ya hivi punde kutokana na uhasama uliopo kati ya Kirr na Machar.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kiongozi wa waasi Riek Machar, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Sudan Omar al-Bashir na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Mwezi uliopita Ikulu ya Marekani ilionya kuwa makubaliano madogo kati ya viongozi hayawezi kutatua changamoto zinazoikumba Sudan Kusini.

Umoja wa Mataifa ulisema makubaliano ya ugavi wa mamlaka ni hatua kubwa. "Kwa kuweka sahihi makubaliano, bunduki ni lazima zikae kimya," alisema Nicholas Hayson mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, vikawalazimu watu milioni nne kuhama makwao na kusambaratisha uchumi wa taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

Mada zinazohusiana