Kangi Lugola: Watanzania ndio waliotulazimu kuweka masharti ya kuondoka nchini

Kangi Lugola: Watanzania ndio waliotulazimu kuweka masharti ya kuondoka nchini

Tanzania imeanza kutekeleza agizo linalowataka Watanzania wanaopata kazi nje ya nchi kupata nyaraka kadhaa na idhini kutoka kwa idara ya uhamiaji.

Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola alikuwa amesema: “Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, pamoja na kwamba wanaweza watanzania wenzetu wakawa wamepata kazi kule nje, usiwaruhusu kuondoka, narudia, usiwaruhusu kuondoka bila kujiridhisha na maelekezo ya serikali.”

“Moja, lazima wawe na mikataba ya kazi ya huko walikopata kazi, lakini pia tuwe na uthibitisho wa balozi wetu aliyeko kule kwamba nchi ile na kampuni hiyo wanayoenda kufanyia kazi yapo maelewano ya kuwapokea Watanzania kufanya kazi katika mazingira hayo.”

Alisema wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu kwa mara yake ya kwanza kabisa nchini Tanzania ambayo yalifanyika Dar es Salaam.

Bw Lugola alisema wapo wahanga wa biashara hiyo, mfano India, Thailand na Hong Kong na taratibu za kuwarejesha nchini Tanzania zinaendelea.

Suala hilo limeibua mijadala katika mitandao ya kijamii na limekuja wakati baadhi ya raia wa Tanzania wanaofanya kazi katika mataifa kadhaa ya Asia wakilalamika kutendewa vitendo vya udhalilishaji.

Watanzania wafanyao kazi ughaibuni huchangia takriban dola milioni 500 kwa taifa kila mwaka.

Mwandishi wa BBC Halima Nyanza amezungumza na Bw Lugola kupata ufahamu zaidi kuhusu agizo lake.

Waziri huyo amesema lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anayeajiriwa nje ya nchi anakua katika mikono salama na kwamba serikali haina nia ya kuwatia hofu raia wake.

Amesema Watanzania ndio wanaoilazimu serikali kuweka mwongozo wa aina hiyo kwani kila wanapopatwa na matatizo huilimbikizia lawama serikali.