Mambo ya kushangaza kuhusu tendo la ndoa duniani

Pop Art illustration - Female lips and a speech bubble saying 'sex', comic book style

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mambo ya kushangaza na itikadi kuhusu tendo la ndoa duniani

Tendo la ndoa huaminika kuwa miongoni mwa mambo ya kale zaidi. Bila shaka, binadamu hawangeendelea kuwepo bila kujamiiana. Lakini jinsi jamii mbalimbali zinavyoshiriki katika tendo hili pamoja na imani zinazohusiana na tendo hili ni tofauti kutoka eneo moja hadi jingine duniani.

Tukiangazia maeneo mbalimbali duniani, kuanzia sababu ya Korea Kusini watu kukataa kuzaa, watu wanaocheza na matufaha makwapani na itikadi nyingine za kushangaza duniani.

1. Wahawaii wa asili huwa na majina ya viungo vyao vya uzazi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wahawaii wa asili huwa na majina ya viungo vyao vya uzazi

Katika utamaduni wa watu wa jamii ya Hawaii, walikuwa wanaabudu na hata kubandika majina ya kupendeza viungo vyao vya uzazi. Wote, bila kujali kama ni mtu wa kawaida au wa familia ya kifalme, kila mmoja alikuwa na jina lake maalum ya kiungo chake cha uzazi. Wakati mwingine wangetunga hata wimbo na mashairi. Mashairi haya yalikuwa yanaeleza kwa kina kiungo husika hadharani. Dkt Milton Diamond, mtaalamu wa utamaduni wa ngono wa wakazi wa Hawaii kabla ya kuingiliwa na Wazungu, anaeleza jinsi Malkia Lili'uokulani alivyokuwa na wimbo wake ambapo alikuwa anasema kiungo chake kilikuwa na 'Chachawa', kwamba 'kilipenda kuruka ruka juu na chini'.

2. Wajapani hawashiriki tendo la ndoa sana

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wajapani hawashiriki tendo la ndoa sana

Japan ni taifa jingine ambalo linashuhudia kushuka kwa kiwango cha watoto wanaouzaliwa. Matumizi ya mipira ya kondomu, tembe za kuzuia kushika mimba na visa vya maambukizi ya magonjwa ya zinaa vyote vinashuka. Kunio Kitamura, ambaye ni mkuu wa chama cha uzazi wa mpango nchini Japan anasema, "Ufafanuzi pekee wa kueleza hili ni kwamba Wajapani wameanza kupunguza ushiriki wao wa tendo la ndoa."

Ripoti ya hivi majuzi ilibaini kwamba idadi ya wanandoa ambao wanaishi pamoja bila kushiriki tendo la ndoa imeongezeka sana. Theluthi moja ya wanaume walisema huwa wanachoka sana kiasi cha kutokuwa na hamu ya kushiriki tendo la ndoa. Robo ya wanawake walisema huwa hawafurahii tendo la ndoa. Utafiti mwingine uliangazia vijana wa miaka kati ya 18 na 34 na kubaini kwamba idadi ya mabikira imeongezeka sana katika mwongo mmoja iliyopita. Asilimia 45 kati ya waliohojiwa kwenye utafiti huo walisema hawajawahi kushiriki ngono.

3. Wanawake Korea Kusini hawataki kupata watoto

Chanzo cha picha, LeoPatrizi

Maelezo ya picha,

Wanawake Korea Kusini hawataki kupata watoto

Kwa wastani mwanamke Korea Kusini anatarajiwa kujaliwa watoto 1.05 maishani mwake. Lakini taifa hilo linahitaji kiwango cha watoto 2.1 kwa kila mwanamke ndipo kudumisha uthabiti katika idadi ya watu nchi humo. Kiwango hiki ni maradufu ya kiwango cha sasa. Ili kujaribu kutatua shida hiyo, serikali imewekeza mabilioni ya dola katika kampeni ya kuwahamasisha wanawake wazae, lakini kiwango kimeendelea kushuka.

Huenda ikawa inatokana na kupanda kwa gharama ya maisha na gharama ya kuwalea watoto, lakini pia huenda inatokana na muda mrefu ambao watu hufanya kazi kwa siku nchini humo.

Kwa kuwa wanawake ndio bado hutegemea kukidhi mahitaji ya mtoto na kushughulikia malezi yake, kupata mtoto kuna maana kwamba mwanamke atakosa kuangazia kazi yake - na wanawake wanakataa hilo.

4. Urusi kuna siku ya Kutungwa kwa Mimba

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Urusi kuna siku ya Kutungwa kwa Mimba

Jimbo moja nchini Urusi limeanzisha njia ya kipekee ya kusaidia watu kuzaana kwa wingi baada ya kugundua kwamba idadi ya watu inapunguza kwa kasi. Gavana wa jimbo la Ulyanovsk, mashariki mwa Moscow alitangaza 12 Septemba kila mwaka kuwa Siku ya Kutunga Mimba. Hii ni siku ya mapumziko ambapo wanandoa huhamasishwa kukaa nyumbani kwa lengo moja pekee, kuhakikisha wanatunga mimba na kuzaa watoto zaidi. Wanandoa wanaojaliwa watoto miezi tisa baada ya siku hiyo hupewa zawadi nono. Baadhi hupewa kamera, majokofu na wengine mashine za dobi (za kufua nguo na kuosha vyombo).

5. Kijiji cha Mehinaku, Brazil wanaume hutongoza kwa samaki

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Brazil wanaume hutongoza kwa samaki

Katika kijiji kidogo cha Mehinaku, katikati mwa Brazil, wanawake huwa na njia rahisi ya kuchagua nani wa kumkubali kati ya wanaofika kuwatongoza. Wanaume wanaomshindania mwanamke fulani hufika wakiwa na samaki. Mara nyingi, aliyefika na samaki mkubwa kabisa huwa ndiye mshindi!

6. Austria wanawake huweka matufaha kwenye makwapa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Austria wanawake huweka matufaha kwenye makwapa

Maeneo ya mashambani Australia, ni utamaduni wa miaka mingi wanawake kuyapasua matufaha, kuyaweka kwenye makwapa yao na kisha kuwapa wanaume wanaowachumbia wakati wa ngoma ya kitamaduni.

Iwapo mwanamume atalifurahia tufaha hilo baada ya kulinusia na kuwa anampenda mwanamke huyo, atamega kipande cha tufaha hilo lililojawa na jasho.

7.Colombia wanaume hupigwa ngwala

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Colombia wanaume hupigwa ngwala

Katika jamii ya Guajiro, mwanamke hujipatia mwanamume wa kumuoa baada ya kumpiga ngwala na kumwangusha wakati wa kucheza ngoma ya kitamaduni. Kutokuwa na nguvu bila shaka kwa wanaume hawa ni nafuu. Iwapo mwanamke atafanikiwa kumwangusha mwanamume kwa kumpiga ngwala, basi wawili hao ni lazima washiriki tendo la ndoa. Hii nayo si ni maana mpya ya 'kuanguka katika penzi'?

8.Denmark ndio stadi wa kutungisha mimba wakiwa likizoni

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mapenzi hufanyika likizoni Denmark

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni moja ya safari za kitalii, raia wa Denmark hushiriki tendo la ndoa kwa wastani asilimia 46 zaidi wakiwa likizoni na kwenye safari za kitalii. Asilimia 10 ya watoto wote Denmark mimba yao hutungishwa wazazi wao wakiwa ziarani. Mwaka 2014, kampuni hiyo ya Spies Travel iliahidi zawadi ya mahitaji ya mtoto ya miaka mitatu pamoja na likizo murua kwa wanandoa ambao wangethibitisha kwamba mimba yao mtoto wao ilitungwa wakiwa kwenye likizo iliyopangwa na kampuni hiyo. Makubwa hayo!

9.Wagiriki ndio hushiriki tendo la ndoa mara nyingi zaidi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Eros, mungu wa mapenzi wa wagiriki

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa duniani na kampuni ya mipira ya kondomu ya Durex, ambapo walishirikisha watu karibu 30,000 wa miaka zaidi ya 16 katika mataifa 26, Wagiriki wanaongoza kwa kushiriki ngono. Kwa wastani, Wagiriki hufanya tendo la ndoa mara 164 kwa mwaka.

Ukizingatia hali ya hewa nchini Ugiriki, ambapo hakuna baridi sana au joto linalopita kiasi, na ukumbuke kwamba wana bustani na mizeituni, si ajabu. Filamu nyingi pia huonesha utamaduni wao kama watu wenye kupenda ngono sana. Hata kwenye hadithi na ngano zao za miungu wa kale na binadamu wa kale. Huoneshwa kama watu wasiojali kushiriki ngono hadharani, na wenye kupenda kufanyia majaribio mambo mengi na njia nyingi za kukoleza mahaba wakati wa kushiriki tendo la ndoa.

Kwako ni jambo gani la kushangaza kuhusu tendo la ndoa umekumbana nao au kufahamu maishani? Twandikie katika ukurasa wetu wa Facebook, BBC Swahili!