Vikwazo vya Iran: Trump awaonya washirika wa kibiashara wa Iran

Rais Donald Trump na Hassan Rouhani

Rais wa Marekani Donald Trump ametoa onyo kali kwa mtu yeyote anayeshirikiana kibiashara na Iran kufuatia hatua yake ya kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

''Yeyote atakayefanya biashara na Iran hataruhusiwa kufanya biashara na Marekani'' , rais huyo alituma ujumbe wa twitter.

Vikwazo vikali vilianza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo na vingine vikali vinavyohusiana na mafuta vitaanza mwezi Novemba.

Rais wa Iran amesema kuwa hatua hizo ni vita vya kiakili ambavyo vinalenga kuleta mgawanyiko miongoni mwa raia wa Iran.

Vikwazo hivyo vinafuatia hatua ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya kinyuklia ya Iran mapema mwaka huu.

Makubaliano hayo , yalioafikiwa wakati wa utawala wa rais Barrack Obama ,yaliilazimu Iran kusitisha mpango wake wa kinyuklia huku vikwazo dhidi yake vikiondolewa.

Rais Trump ameyataja makubaliano hayo 'yanayopendelea upande mmoja'' kuwa mabaya zaidi kuwahi kufanyika.

Anaamini kwamba shinikizo mpya za kiuchumi zitailazimu Iran kuingia katika makubaliano mapya.

Muungano wa Ulaya, ambao bado unaunga mkono makubaliano hayo ya Iran , umezungumza dhidi ya vikwazo hivyo ukiapa kulinda kampuni zinazofanya biashara halali na Iran.

Ni nini chengine kilichosemwa na Trump katika ujumbe wake wa Twitter?

Alivipongeza vikwazo vikali vilivyowekwa na kusema kuwa vitangozwa hadi kufikia kiwango cha juu mnamo mwezi Novemba.

''Ninaomba amani duniani, sio chengine,'' alisema.

Siku ya Jumatatu alikuwa amesema kuwa Iran ilikuwa inakabiliwa la chaguo la kubadili vitisho vyake na tabia yake ya kuzua uhasama na kuingiliana na uchumi ama isalie katika njia ya vikwazo na kutengwa kiuchumi.

''Nimesalia tayari kuafikia mkataba ambao utajadili vitendo vyote vibaya vya Iran, ikiwemo mpango wake wa kutengeneza silaha za masafa marefu na kuunga mkono ugaidi'', alisema.

Vikwazo hivyo ni vipi?

Bwana Trump alitia saini agizo kuu ambalo lilirudisha vikwazo dhidi ya taifa hilo siku ya Jumanne. Vikwazo hivyo vinalenga:

  • Ununuzi wa noti za Marekani unaofanywa na Iran.
  • Biashara ya dhahabu na vyuma vingine
  • Graphite, aluminium, chuma, mkaa na programu zinazotumiwa katika sekta ya viwanda
  • Ubadilishanaji wa fedha unaohusishwa na sarafu ya Iran
  • Vitendo vinavyohusishwa na ulipaji madeni ya Iran
  • Sekta ya magari ya Iran

Awamu ya pili ya vikwazo hivyo vitaanza kutekelezwa mwezi Novemba ambavyo vitakuwa na athari katika sekta ya kawi na ile ya uchukuzi wa majini nchini Iran bila kusahau bishara ya mafuta, na biashara kati ya taasisi za kifedha za kigeni na benki kuu ya Iran.

Hatua hiyo imesababisha hisia gani?

Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema kuwa Marekani imekataa kutumia njia ya kidiplomasia.

''Walienda kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya taifa la Iran .Majadiliano na vikwazo hayaleti maana yoyote. Kila mara tunapendelea diplomasia na mazungumzo... lakini mazungumzo pia yanahitaji uaminifu''.

Mawaziri wa maswala ya nchi za kigeni , Uingereza na Ufaransa walitoa taarifa siku ya Jumatatu wakisema kwamba makubaliano hayo ya kinyuklia bado ni muhimu kwa usalama duniani.

Pia walizindua sheria zao za kulinda makampuni ya Ulaya yanayofanya biashara na Iran licha ya vikwazo hivyo vibaya vya Marekani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii