Kangi Lugola: Waziri 'mwiba' mwenye maamuzi makali Tanzania

Tangu kuapishwa kwake amekua akitoa maagizo na kuwawajibisha viongozi wa idara mbalimbali zilizo chini ya wizara yake Haki miliki ya picha Ikulu
Image caption Kangi Lugola akila kiapo mbele ya Rais Dokta Magufuli

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Kangi Lugola ameonekana mwiba kutokana na maamuzi na kauli zake dhidi ya viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya mambo ya ndani.

Bwana Lugola aliingia kwenye majukumu hayo mapya kwa kishindo. Aliteuliwa ukiwa ni mchakato wa mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Tanzania, Dokta John Magufuli.

Mabadiliko hayo yalitangazwa huku Rais Magufuli akieleza pamoja na mambo mengine kutoridhishwa na namna ambavyo suala la ajali za mara kwa mara linavyoshughulikiwa, watu kutowajibika kutokana na matukio hayo.

Katika kipindi cha majuma machache tangu kukabidhiwa majukumu mapya maafisa kadhaa wamejikuta katika wakati mgumu wakipata maonyo makali na hata kushushwa vyeo walivyokuwa wakivitumikia.

Kwa mfano tu siku kadhaa zilizopita waziri Lugola alimpa siku mbili Zitto ajisalimishe kwa Jeshi la Polisi mkoani Lindi kutokana na madai kuwa alitoa kauli za uchochezi.Kauli ambayo hata hivyo ilipuuzwa kwa madai kuwa si halali.

Lugola aliteuliwa Julai mosi mwaka huu na kuapishwa Julai 2, mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam akichukua nafasi ya Mwigulu Nchemba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Dokta John Magufuli kwa sababu mbalimbali.

Kangi Lugola amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutokana na kauli zake, pia aina na mwenendo wa utendaji kazi wake.

Ni kutokana na Amri na maagizo zaidi ya 10 aliyoyatoa katika kipindi kifupi tangu ashike wadhifa huo.

Tamko la kwanza

Mara tu baada ya kuapishwa, Julai 3 alifanya ziara mkoani Mbeya kwa lengo la kufanya uchunguzi wa sababu za kukithiri kwa ajali za barabarani kwenye mkoa huo.

Lugola aliagiza kuvunjwa kwa Balaza la Taifa la Usalama Barabarani pamoja na kamati zake zote nchi nzima.

Alisema kuwa aliamua kufanya hivyo kutokana na kushindwa kupambana na ajali.

"Nilikuwa namuuliza mwenyekiti wa baraza la usalama barabarani nikabaini hajui hata sheria inayoliweka baraza hilo nahata kanuni zake hazijui, hii inaonyesha hatuna baraza na kuanzia sasa kwa mamlaka niliyonayo nalivunja baraza hili na nitaliunda upya,". Alisema Lugola.

Tamko la pili

Bwana Kangi Lugola, alimpa maagizo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, akihoji kwanini mabasi hayatembei usiku huku biashara mbalimbali zinafungwa saa 12 jioni.

"IGP aje aniambie mabasi kutotembea usiku ni kwa sababu Jeshi la Polisi limenyoosha mikono kwa majambazi, biashara mbalimbali ikifika saa 12 watu wanafunga wanakwenda majumbani ukiwauliza wanasema ni kwa sababu za usalama, hatuwezi tukakubali kupewa amri na majambazi ni masaa mangapi tufanye shughuli za kiuchumi''.

Tamko la tatu

Huwezi kusikiliza tena
Lugola: Watanzania ndio waliotulazimu kuweka masharti ya kuondoka nchini

Julai 6, mwaka huu, Waziri huyo wakati akizungumza na vyombo vya habari pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalana na idara zilizo chini ya wizara hiyo alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwashusha vyeo, Mkuu wa Usalama Barabarani Mbeya, Mrakibu wa Polisi, na Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, George Mrutu ambaye alikuwa tayari ameshaenguliwa katika nafasi hiyo.

"Hivyo lazima nichukue hatua kali ili kunusuru maisha ya watu kwani Rais amechoka kutuma salamu za rambirambi,".

Tamko la nne

Katika mkutano huo pia aliwaagiza wakuu wa vyombo vya usalama chini ya wizara yake, kubeba Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kile alichodai kuwa wanafanya kazi ya chama kilichopo madarakani, hivyo ni lazima waitumie katika kuweka mipango kazi.

Tamko la tano

Julai 12 waziri huyo alitembelea Idara ya Uhamiaji na kuzungumza na watendaji wakuu wa idara hiyo huku akiagiza na kuwataka askari wa uhamiaji waliopo mipakani kujitafakari kwa maelezo kuwa utendaji wao hauridhishi.

''Tatizo liko wapi, inakuaje magari yaliyobeba wahamiaji yanatokea mpaka wa Himo (Kilimanjaro), yanapita Arusha na Manyara, yanakwenda kukamatwa Dodoma?'',Uhamiaji mnakuwa wapi? Inasikitisha watu hawa wanapita mikoa hiyo bila kukamatwa.Watu wa mipakani wajitafakari hatuwezi kukubali hali hii''.

Haki miliki ya picha KAJUNASON
Image caption Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania, Kangi Lugola, akizungumza na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye

Tamko la sita

Wakati waziri huyo akikagua mabanda ya maonyesho katika maadhimisho ya kupinga usafirishaji wa binadamu papo hapo alimwondoa, Inspekta wa Polisi Kitengo cha Uhamiaji, Abubakar Yunusi katika ujumbe wa Sekretarieti ya Kuzuia Biashara Haramu ya Binadamu.

Sababu iliyozalisha uamuzi huo ni afisa huyo wa Polisi kutoajua takwimu za vyombo vilivyotumika kusafirisha binadamu ambavyo vimekamatwa na vinasubiri kutaifishwa.

"Wewe umejitambulisha kuwa ni mjumbe wa kamati ya kudhibiti usafirishwaji haramu wa binadamu, umesema kuna vyombo vimetumika, huna idadi yake. Unafanya kazi ya ubabaishaji hapa? Huwezi kuja kwenye maonyesho hujui idadi yake. Kazi yako ya ujumbe hakuna."

Tamko la saba

Baada ya Lugola baada ya kubaini kuwa mbwa maalum wa kikosi cha bandari hayupo mahala pake pa kazi alitoa agizo kwa IGP Sirro akimtaka afuatilia alipo mbwa huyo na kumpa ripoti katika muda ambao ulikuwa hauzidi saa 10.

"Nimesikitishwa kwa kitendo cha mbwa huyu mmoja mpaka sasa haonekani namaelezo niliyopewa hayajaniridhisha kwa sababu kwenye kitabu haijulikani huyumbwa jana alivyotoka alikwenda wapi na alilala wapi na leo haijulikani yupo wapi,kwetu sisi mbwa ni askari," alisema na kuongeza:"Namwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwamba nitakapomaliza ziara yangumajira ya saa 12:00 anipigie simu akiwa na huyo mbwa pale polisi Bandari ilimwenyewe niweze kufika pale na kumwona huyo mbwa ambaye ni askari."

"Ifikapo saa 12:00 jioni IGP lazima awe na huyu mbwa anionyeshe ili nijiridhishealikuwa wapi na alikuwa amekwenda kufanya nini," alisema.

Tamko la nane

Julai 21, mwaka huu waziri huyo alipokutana na wanahabari aliagiza kulazwa mahabusu kwa dereva yeyote atakayesababisha ajali na kama ikibainika ajali hiyo ilisababishwa na ubovu wa gari basi hata mmiliki alale ndani kabla ya kupandishwa kizimbani.

Alisema ikitokea dereva yoyote akafikishwa Mahakamani kabla ya kulazwa mahabusu, basi huyo aliyefanya hivyo atashughulika nae.

Tamko la tisa

Lugola aliagiza jeshi la Magereza kuhakikisha wafungwa wanajilisha na kulisha mahabusu, na kwamba hataki kuona wafungwa nchini wanaishi kama ndege wa angani.

Alisema wafungwa hawalimi ila wanakula bure, badala yake wanatakiwa wafanye kazi na kujitafutia chakula wao wenyewe badala ya kusubiri kupewa chakula na Serikali.

Aliyesema hayo Julai 16 wakati akihojiwa katika kipindi cha Tuambie kilichorushwa na kituo cha televisheni ya taifa, TBC 1 na kueleza kuwa amewaagiza wasaidizi wake kupitia sheria vizuri na kumpelekea mpango mzuri wa utekelezaji wa agizo la Rais, la kuwatumia wafungwa kufanya kazi za kilimo na ufugaji na kujitafutia chakula wao wenyewe.

"Hata kama ni meno, lazima walimie meno, watatumia meno yao kulima mahindi, kulima maharage ili wajilishe, na nimemwambia Inspekta Jenerali wa Magereza, katika hili sitaki kisingizio cha aina yoyote".

Tamko la kumi

Julai 23, mwaka huu, Waziri huyo aliagiza kuwekwa Mahabusu kwa Askari Polisi aliyekuwa katika kituo cha polisi cha utalii na Diplomasia baada ya kushindwa kuelezea vitabu muhimu vinavyotakiwa kuwa kwenye chumba cha mashitaka.

"Nimeingia kwenye chumba cha mashtaka, nikamkuta askari nikamuuliza vitabu muhimu kwenye chumba hicho akabaki ameduwaa, nikamuagiza RPC (Kamanda wa Polisi) amuweke ndani. Lakini baadaye nikaamuru atolewe kwani yawezekana askari huyo hana elimu ya masuala ya utalii,"

Waziri Lugola amekuwa akikosolewa kwa kiasi kikubwa na wapinzani mbalimbali pia wanasheria kuhusu amri na maagizo ambayo amekuwa akiyatoa kwa watendaji mbalimbali wa serikali, huku wengine wakikosoa uteuzi uliofanywa na Rais Magufuli kumteua Lugola baada ya kumuweka kando Mwigullu Nchemba.Wengine wanaona hakuna mabadiliko makubwa ya kutarajiwa kutoka kwake.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii