Je maji ya madafu yana umuhimu gani katika mwili wa mwanadamu?

Mzee Mwajita akiwa na wateja wake nje ya soko la Market Mombasa

Madafu ni kinywaji maarufu sana pwani ya Kenya hasa mjini Mombasa. Kuanzia wenyeji mpaka watalii wote wanapenda madafu, maji ya nazi ambayo haijakomaa.

Baadhi ya Wapwani wanategemea madafu kwa kipato chao, mmoja wao ni Mzee Mwajita Khamis ambaye anauza madafu yake barabara ya Digo karibu na soko la Mackinnon ama Marikiti ukipenda.

``Mimi nimeuza madafu tangu mwaka wa 1984, hii ni kama ofisi yangu na hapa ndio mategemeo ya kila kitu,'' anasema Mwajita.

``Madafu ni zao kubwa ambalo tunategemea sisi Wapwani, halafu haya madafu ni tiba kubwa sana kwa sababu maji ya madafu kazi yake ni kuosha mwili wa mwanadamu sehemu ya figo huwezi pata shida hapo.''

Huku nami nikiwa nanywa madafu nikizungumza na Mwajita, mteja wake wa kila siku Musa Zimbwe anaunga mkono asemayo Mwajita kuhusu madafu kuosha mwili.

``Madafu yanasaidia mwili, hasa haja ndogo na kwa upande wetu yanatusaidia kwa nguvu za kiume, ng'ome inaimarika tu sana ukinywa madafu,'' anasema Zimbwe

``Mimi kila siku sikosi hapa kwa Mzee Mwajita, nimetumia madafu kwa zaidi ya miaka hamsini, nimezaliwa nikiyaona, kuna madafu ya kunywa pekee, na madafu mengine yana nazi changa hivi ndani watafuna.''

Mwajita anasema biashara ya madafu ni ya familia anayofanya akisaidiwa na wanawe wa kiume.

``Hii ni kama royal family, inanifaidisha, nalea na ndio kila kitu kwa maisha yangu yetu. Sisi Wadigo madafu mhimu kwetu, hapa ni kama kiwanda chetu. Mimi mwenyewe mbali na kuuza nanywa madafu kama tano ama sita kila siku. Ukiniangalia mimi mbali na nywele nyeupe nina nguvu na ngozi yangu laini kwa sababu ya madafu.''

Utafiti ambao nimeiufanya kwa mtandao unathibitisha asemayo Mwajita kuhusu umuhimu wa maji hayo ya nazi changa.

Pamoja na kulainisha ngozi, madafu ni tiba ya figo, yanasafisha uchafu mwilini, husaidia wanawake waja wazito na kupunguza presha mwilini miongoni mwa manufaa yake.

Mtaalam wa lishe Joe Lewin ameambia BBC madafu yana umuhimu sana kwa mwili wa binadamu na kwamba uzuri wake kiwango chake cha sukari kiko chini tofauti vinywaji vingine kama vile soda na juici.

Lewin hatahivyo anasema hamna ukweli wa madai kwamba madafu husaidia wana riadha kufanya vyema zaidi, na isitoshe ingekua hivyo basi maji hayo yangewekwa kundi moja na dawa zingine za kuongeza nguvu zilizopigwa marufu na shirikisho la kimataifa, IAAF.

Mtaalam huyo wa lishe hatahivyo anasema madafu husaidia moyo wa binadamu na madini ya potassium.

Utafiti uliofanywa kwa kutumia panya unaonyesha unywaji wa madafu unashusha kiwango cha cholesterol lakini Lewin anaeleza bado hakuna ushahidi wa kutosha kwa upande wa binadamu.

Kwa upande wa kuimarisha nguvu za kiume kama anavyosema Musa Zimbwe wa Mombasa hilo ni suala la kibinafsi lakini ni dhahiri kwamba madafu ni kinywaji mhimu sana pwani ya Kenya.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii